Nini kilichotokea kati ya Kolimba na Nyerere?

Nini kilichotokea kati ya Kolimba na Nyerere?

jijayetu

JF-Expert Member
Joined
Jul 15, 2016
Posts
727
Reaction score
563
HORACE Kolimba ni miongoni mwa viongozi waandamizi nchini ambaye Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alitofautiana naye na baadhi ya wenzake kuhusu masuala ya msingi katika uongozi na mwelekeo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lakini mbali na Mwalimu, Kolimba alitofautiana na chama chake (CCM), angali Katibu Mkuu, akiweka bayana chama hicho kimepoteza dira.

Kwa ujumla, hakuna ubishi kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa akifahamu mifumo yote ya uongozi wa nchi kwa sababu ameshiriki kuibuni n kuiridhia, akiwa kiongozi mkuu.

Bila shaka, alielewa wapi apate taarifa ipi na kuhusu nani au nini. Kubwa zaidi, watoa taarifa katika vyombo nyeti nchini walijitolea kumdokeza kwa kadiri ilivyowezekana wakiamini ndiye mtu wa uhakika asiye na hila kwa nchi yake. Asiye na mikono michafu dhidi ya nchi.

Lakini pia hakuna ubishi Mwalimu huyo huyo, alifahamu tabia na mienendo ya viongozi karibu wote waandamizi nchini. Ikumbukwe, asilimia kubwa ya viongozi ‘aliwalea’ baada ya kuwaingiza katika mfumo wa uongozi.

Kwa hiyo, ni sahihi kusema Mwalimu alitambua uhodari na udhaifu wao na alijenga mazingira ya kuingilia majukumu yao kwa kadiri mambo yanavyoanza kwenda kombo katika ofisi alizowakabidhi chini ya kauli mbiu; “cheo ni dhamana.”

Na pengine tatizo lililokuwapo ni kwamba wakati mwingine; ‘ndoto’ nzuri alizokuwanazo Mwalimu kuhusu Tanzania bora isiyotegemea wahisani kujiendesha na isiyoongozwa na mchanganyiko wa viongozi wezi na waadilifu wanaovumiliana na hata kuwa genge moja dhidi ya umma, hazikusambaa vizuri kwa baadhi ya viongozi wenzake.

Na kwa hiyo basi, pengine alikuwa akihisi wenzake wanavuruga ‘ndoto’ yake bila kujua kwamba ndoto hiyo haieleweki kwao au inaeleweka lakini kwao haina ‘mashiko’. Kwamba wakati yeye akiwa ameridhia hata mshahara wake upunguzwe ili kukabili hoja za mgomo wa wanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) bila kulalamika maisha yake yatakuwa magumu (Msasani sio Dodoma kama sasa), wenzake wengi walitamani mshahara mkubwa zaidi.

Na kwa mantiki hiyo kutokana na baadhi ya hatua alizokuwa akichukua kama kiongozi wa nchi na hata baada ya kustaafu, wengi wanaamini ilikuwa vigumu kwa viongozi wengi waandamizi kubishana hadharani na Mwalimu Nyerere.

Ni kama vile uadilifu wa Mwalimu ulikuwa kikwazo au silaha kwa baadhi kumshambulia hadharani, ingawa kwa nadra ilijitokeza wachache kufanya hivyo huku wengine wakiishia kulalamika pembeni (mitaani).

Kati ya ambao miongoni mwao hawakuridhiki na walitumia mbinu nyingine za kumjibu Mwalimu ni pamoja na Horace Kolimba, kama tutakavyoona katika mfululizo wa makala hizi.

Kimsingi, inawezekana viongozi wengi waandamizi waliamini kwamba mbele ya umma, nguvu za Nyerere ni kubwa zaidi hasa kwa kigezo cha uadilifu na kwa hiyo, si rahisi kumpinga katika hali ya kumdhalilisha na ukabaki salama.

Imani hii ya uadilifu wa Nyerere ndiyo bila shaka, iligeuzwa na Watanzania kuwa dhamana kwa Benjamin Mkapa asiyekuwa ‘mwenyeji’ kwao, na wakampigia kura za urais 1995.

Urais ambao baadhi ya machapisho yanabainisha kuwa Kolimba naye alikwishaonesha nia mapema zaidi, takriban miezi 10 kabla (mwishoni mwa mwaka 1994).

Lakini hata hivyo, ni dhahiri kuwa nyuma ya nguvu hizi za Mwalimu Nyerere katika jamii aliyoshiriki kusaka uhuru wake dhidi ya watawala wa kigeni, kulikuwa pia na nguvu za dola zilizokuwa na jukumu la kusukuma na kusimamia hoja zake za kitaifa.

Wengi mtakumbuka jinsi Mwalimu alivyotofautiana dhahiri na aliyekuwa Waziri Mkuu, John Malecela, achilia mbali Katibu Mkuu wa CCM (chama tawala), Horace Kolimba.

Na kwa namna ya kipekee, Mwalimu pia alitofautiana kuhusu namna Mzee Ali Hassan Mwinyi alivyokuwa akiongoza nchi katika baadhi ya masuala ya msingi, ingawa wakati mwingine alimtetea kuwa anashauriwa vibaya.

Nini hasa kilitokea?

Kutokana na tofauti hizo na hasa kwa kuangalia viongozi hao watatu, Kolimba, Malecela na Mwinyi, itakumbukwa Mwalimu aliandika kitabu; Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania.

Sijui kwa sababu zipi hasa ambazo pengine Mzee Ali Hassan Mwinyi na Mzee John Malecela wanaweza kuzieleza kwamba hawakutaka kujibishana na Mwalimu Nyerere, tofauti na alivyofanya Horace Kolimba.

Hata hivyo, Kolimba naye hakufanya majibizano na Mwalimu moja kwa moja hadharani, anadaiwa kutumia vyombo vya habari vya Chama cha Mapinduzi (magazeti ya Uhuru na Mzalendo) akiwa Katibu Mkuu, kumjibu Nyerere.

Inaaminika katika hali inayothibitisha nia ya Kolimba kuwania urais mwaka unaofuatia (1995), mwaka 1994 mwanasiasa huyo alijipanga kwanza kujinasua na mashambulizi ya Mwalimu Nyerere kwake na hata kwa wenzake (Mwinyi na Malecela ambao walikaa kimya). Mashambulizi hayo yamo kwenye kitabu cha Nyerere; Uongozi wetu na hatima ya Tanzania.

Maswali zaidi yanajitokeza katika mkakati huo wa Kolimba kama ambavyo pia tutazidi kubaini katika mufululizo wa makala hizi.

Kwa mfano, wakati Kolimba akidaiwa kutumia vyombo vya chama kumjibu Nyerere katika ‘staili’ ya kipekee ambayo ilifichuliwa na magazeti mengine nchini, Mzee Mwinyi akiwa Mwenyekiti wa chama, alikaa kimya.

Kupitia magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Kolimba anadaiwa kuwatumia waandishi ambao inadaiwa pia walikuwa wakitumia majina tofauti, kama ilivyopata kufichuliwa na gazeti jingine la binafsi baadaye.

Baadhi ya makala hizo ni zile zilizotolewa katika gazeti la Uhuru la Novemba 8, mwaka 1994 ukurasa wa saba na Novemba 18, mwaka huo huo, pia ukurasa wa saba. Makala hizi inaelezwa ziliandikwa na Kolimba lakini kwa jina la mwandishi aliyejiita Alex Kowe.

Makala hizi (ambazo nitazichambua siku zijazo) ziliandikwa katika wakati ambao kwanza ni mwaka mmoja kuelekea Uchaguzi Mkuu huku Kolimba akidaiwa kutaka kuwania urais.

Lakini pia ni yeye ambaye kuelekea uchaguzi huo huo wa 1995, aliweka bayana chama anachokiongoza kimepoteza dira, ikielezwa angegombea kwa chama kingine.

Na kwa namna ya kipekee katika kile kinachoelezwa ni kujibu mapigo ya Mwalimu Nyerere kwa kitabu chake cha “Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania” Novemba 4, mwaka 1994, Kolimba alijigamba mbele ya waandishi kuwa; hajioni kuwa na kasoro kama Mtendaji Mkuu wa CCM na kwamba uamuzi ni wa wananchi.

Kauli yake kwamba; “uamuzi ni wa wananchi” ilizua maswali mengi kwa baadhi ya watu na hasa waliopata kuhisi au kuelezwa kuwa Kolimba anataka kuwania urais mwaka 1995. Kwamba alitaka awe Amiri Jeshi Mkuu wa tatu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Maswali ni mengi na miongoni mwa hoja zilizoibuka ni kwanza; Kolimba ambaye si kiongozi wa kuchaguliwa (mteule) ni kwa vipi aseme wananchi wawe waamuzi wakati hawakuwahi kumchagua?

Je, alitaka kwenda kujipima kwa wananchi kwa njia ya kupigiwa kura baada ya kuachana na wadhifa wa kuteuliwa? Na je, kupigiwa kura katika nafasi ipi ya uongozi? Je, ni urais?

Swali kubwa zaidi ni; je, kwa kauli hiyo kama Kolimba angekwenda kugombea urais, asingeungwa mkono na Mwalimu Nyerere? Kama jibu ni hapana, je, angeungwa mkono na Mwinyi pamoja na viongozi wengine waliotofautiana na Mwalimu kuhusu uongozi wa nchi na hususan kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995?

Lakini katikati ya kile kinachoelezwa kuwa ni majibu ya Kolimba kwa Nyerere kupitia vyombo vya habari vya chama, wapo waandishi wa habari waliodokezwa kuhusu mipango ya Kolimba na ‘wakachochewa’ ili kwenda kumuuliza Mwalimu.

Wamuulize kwanza; kama amesoma mfululizo wa makala kwenye magazeti ya chama ambazo ingawa zimeandikwa na ‘waandishi’ (kwa majina mengine si Kolimba) lakini zinamjibu na hata kumshambulia.

Pili, nini majibu yake. Tatu, anadhani Kolimba anapata wapi ‘ujasiri’ huo wa kutumia hata vyombo vya chama kwa maslahi yake kisiasa? Yalikuwa maswali ya kumchokoza Mwalimu na hata kupima upeo wake wa busara.

Majibu ya Mwalimu Nyerere ambayo pia yamenukuliwa katika baadhi ya machapisho nchini yanaeleza kwa kifupi lakini katika hali ya upeo mkubwa wa busara, pengine kinyume cha hata matarajio ya wanahabari hao kwamba Mwalimu angehamaki.

Mwalimu Nyerere ananukuliwa kuwajibu waandishi waliomfuata katika hali ya utulivu akitamka maneno sita tu. Akawajibu akisema; mwacheni aendelee, tutajibizana hoja kwa hoja.”

Majibu haya ya Mwalimu bila shaka hayakukidhi matarajio ya waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia sakata hilo kwa kina, na hapa bila shaka, Katibu Mkuu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa KIPINDI KILE, Kajubi Mukajanga, anafahamu hili kwa namna fulani, wakati huo akiwa Mhariri wa gazeti la kila wiki la WAKATI ni HUU.

Lakini pia maneno hayo sita tu ya Mwalimu katika suala pana la mgogoro wa kiuongozi, yalithibitisha Mwalimu alikuwa na taarifa za Kolimba kutumia vyombo vya chama kumjibu, kisichojulikana dhahiri ni je, ‘wakubwa’ gani walikuwa kambi ya Kolimba dhidi ya Nyerere?

Kwa kuzingatia mazingira hayo, wanahabari walizidi kuhoji kwa mfano; pamoja na kwamba Rais Ali Hassan Mwinyi, ni Mwenyekiti wa CCM na ameelezwa kuhusu ‘matatizo’ hayo ya Kolimba kutumia vyombo vya chama kwa kadiri anavyotaka, kwa nini hafanyi lolote?

Maswali hayo na mengine yaliongeza joto na kwa kipekee, ukali wa joto uliongezwa na majibu ya Nyerere; mwacheni tutapambana kwa hoja. Hatimaye, kutokana na joto hilo Mzee Mwinyi akapewa tafsiri kuwa alikuwa akimuunga mkono Kolimba na hasa ikieleweka kuwa naye ni majeruhi katika kitabu cha Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania.

Wiki ijayo tutaangalia hoja za Kolimba katika kujibu mapigo ya Mwalimu Julius Nyerere, akitumia magazeti ya chama angali akiwa Katibu Mkuu, huku kimya cha Mwenyekiti wa chama, Ali Hasssan Mwinyi kikizidi kubeba tafsiri ya kumuunga mkono Kolimba.

Inaendelea
 
wiki ijayo imekuwa miaka,au mwandishi alifariki
 
Back
Top Bottom