Kwa kifupi ninavyoelewa, inasemekana kuwa wakati mataifa mengine ya Kiafrika yalipopata uhuru baada ya WWII, mengi kati yao yalichukua rangi za bendera ya Ethiopia, ambayo ilikuwa haijawahi kutawaliwa. Nchi hiyo ilivutia mataifa mengi mapya ya Afrika na mji mkuu wake Addis Ababa ukawa makao makuu ya mashirika na jumuiya za Kiafrika.
Ufalme wa Ethiopia (Ethiopian Empire) ulitumia rangi hizo katika bendera yake. Hata baada ya utawala wa kifalme kuisha, Ethiopia imekuwa ikitumia rangi hizo na imekuwa ikitafsiri rangi hizo hivi: Kijani inawakilisha utajiri na rutuba ya ardhi yao; Njano inawakilisha matumaini, na Nyekundu inawakilisha kujitoa kwa wananchi wake ambao walimwaga damu yao katika kulinda uhuru wa Ethiopia.
Ukichunguza utagundua kuwa rangi hizo zinabeba tafsiri kama hizo au zinazokaribiana na hizo kwa mataifa mengine ya Afrika yanayozitumia katika bendera zao.
Kijani, njano na nyekundu pia zimekuwa zikitumika kuwakilisha itikadi ya Umajumui wa Afrika (Pan-African ideology). Rastafari, kwa mfano, wanatumia rangi hizo wakizihusisha na Uafrika. Bendera wanayotumia Rastafari ni ile iliyokuwa ikitumika na Ufalme wa Ethiopia kuanzia miaka ya 1870s hadi 1974 ambayo inabeba picha ya Simba wa Yuda (Lion of Judah) ambayo ni nembo ya kitamaduni ya Kiyahudi.
Rasta wanaamini kwenye uhusiano wa mtu mweusi na Ethiopia. Kwa wengi ni Nchi ya ahadi.
Wakati Haile Selassie alipotoa ardhi huko Shashamane ili Waafrika walio utumwani warudi kwenye ardhi yao, si Rastafari pekee waliolengwa, lakini waliishia kuwa kundi kubwa zaidi la watu waliohama kutoka Jamaica na nchi zingine kwenda Shashamane. Harakati za kwanza za Rastafari kwenda Shashamane zilianza mwishoni mwa miaka ya 60 na katikati ya miaka ya 70.