NTA IMESHAYEYUKA
Nilitunza nta yangu, isiweze kuyeyuka,
Niliweka kwenye jungu, isije ikaibika,
Leo ninao uchungu, inta yote meyeyuka,
Nta imeshayeyuka, japo litunza vizuri.
Imetoweka amani, nta yangu kuyeyuka,
Nilikuwa na imani, ufukara ungetoka,
Ningeiuza mjini, kwa Muarabu wa Makka,
Nta imeshayeyuka, japo litunza vizuri.
Nta haifai tena, kunipatia dolali,
Nabaki nakunaguna, nina uchungu mkali,
Kweli maisha ya jana, kwa leo sio ya kweli,
Nta imeshayeyuka, japo litunza vizuri.
Nimetunza nta yangu, tangu nikiwa mtoto,
Tegemeo kubwa langu, nije pate maokoto,
Niligawa kwa mafungu, liweka mbali na moto,
Kusudi la nta yangu, isiyeyuke kwa joto,
Nta imeshayeyuka, japo litunza vizuri.
Nasikitika jamani, nta imeshayeyuka,
Hata wa bei ya chini, hataki ameniruka,
Nitafanya mimi nini, nta yangu meyeyuka,
Niliiweka kichwani, siku moja tajirika,
Nta imeshayeyuka, japo litunza vizuri.
Sinayo njia nyingine, kupata nta mwanana,
Yangu ilikuwa nene, tena ya thamani sana,
Rangi yake ya senene, ningefika mbali sana,
Nta imeshayeyuka, japo litunza vizuri.
Bwana kisicho riziki, hata ungefanya nini,
Kwako hakikamatiki, chatoweka mkononi,
Kwako hakituliziki, chaenda kwa majirani,
Nta imeshayeyuka, japo litunza vizuri.
Denny Jeremias kitumbika
Mtunzi wa mashairi na ngano za Kiafrika
Mufindi Tanzania 13.3.2025