Nusura Muungano Unipe Mrembo wa Kihabeshi

Nusura Muungano Unipe Mrembo wa Kihabeshi

Kantomku

JF-Expert Member
Joined
Jul 25, 2021
Posts
430
Reaction score
899
Mwaka 2014 nikizurula kwenye mtandao wa Facebook kama ilivyo kawaida kwa vijana wengi nilikutana na binti mmoja mrembo raia wa Ethiopia aitwaye Liya . Liya alikuwa msichana mdogo tu mwenye umri wa miaka 19 ambaye kwa maelezo yake alikuwa kaishia elimu ya sekondari tu.

Haikuwa rahisi mrembo huyu kunikubali. Nilimtumia meseji karibia miezi mitatu bila kunijibu chochote. Siku moja alinitolea uvivu akanitumia message ikisema “you are so stubborn, where are you from”. Baada ya kumwambia mimi ni Mtanzania alifurahi na kuniomba radhi kwa kutonipa ushirikiano hapo kabla. Baada ya kuzoeana kidogo nilimwuliza swali ambalo huwa napenda kuwauliza “strangers” wasio watanzania ninao kutatana nao kwenye mitandao ya kijamii.

Swahili lenyewe nililo mwuuliza ni jambo gani analijua kuhusu Tanzania. Liya alijibu kwamba jambo kubwa anajua kuhusu Tanzania ni nchi inayo tokana na muungano wa nchi mbili ambazo ni Tanganyika na Zanzibar.

Hakuuishia hapo alisema mwalimu wao aliwaambia ndio muungano pekee ambao umedumu mpaka sasa barani Africa. Aliongeza kuwa anaipenda sana Tanzania kutokana na historia hiyo nzuri. Nilimuuliza alisoma kuhusu Muungano wa Tanzania katika hatua gani ya elimu alijibu amesoma akiwa shule ya msingi. Niwe mwazi, kwa jinsi alivyo elezea na kuupamba Muungano toka wakati huo nawapenda na kuwaheshimu raia wa Ethiopia.

Mwaka 2014 nilio kutana na Liya Facebook ndio mwaka ambao suala la Muungano lilijadiliwa zaidi kwa miaka ya hivi karibuni kutokana na mchakato wa marekebisho ya Katiba yaliyo anzia Tume ya Jaji Warioba na hatimaye Bunge la Katiba Mpya.

Wakati Liya akinipenda na kunipa heshima kwa sababu ya Muungano wetu Bunge la Katiba pale Dodoma liligeuka uwanja wa sarakasi na vihoja hivyo lilipoteza fursa adhimu ya kuujengea Muungano misingi imara ya kikatiba.

Kwa bahati mbaya Penzi letu na Liya la kwenye mtandao halikudumu sababu nilikuwa tayari nina mke, kule Facebook nilikuwa naingia kujifurahisha tu. Liya mpenzi wangu najua upo hai, ninafurahi kukutaarifu kuwa ule Muungano wa Tanzania unao upenda ulivuka salama mwaka 2014 na bado unadunda; ila hatima ya Muungano huu huko mbeleni namwachia Mwenyezi Mungu na Rais Samia.

Kwa kiasi fulani hivi sasa suala la Muungano halizungumzwi sana. Kwa tafsiri ya haraka ni kwamba mambo yako shwari, Muungano hauna kero wala changamoto zozote. Kwa maelezo ya viongozi wetu kero nyingi na za muda mrefu zimetatuliwa zimebaki tatu tu. Pengine utatuzi wa kero nyingi ndio sababu imefanya watu wengi sasa kuridhika na Muungano wetu.

Binafsi naona ukimya huu sio wa kawaida, iweje ghafla katika miaka ya hivi karibuni Muungano wetu umekuwa “ Sakramenti Takatifu” hadi unaimbwa kwa mazuri tu?. Ukimya huu ni jambo jema endapo umeletwa na suluhu endelevu. Hofu yangu ni kwamba huu ukimya wa muda usije kuwa umeletwa na uwepo wa Rais Samia na baadae akiondoka madarakani Zanzibar wasije wakaliamsha kama kawaida yao na hivyo kusababisha hali ya Muungano kuwa mbaya zaidi.

Ni ukweli ulio wazi kwamba kwa muda mrefu Wazanzibari ndio wamekuwa wakishutumu zaidi kutotendewa haki na Muungano. Hii imepelekea mpaka kuifanyia marekebisho makubwa Katiba ya Zanzibar. Kabla ya Rais Samia kuwa Rais kero za Muungano ndizo zilikuwa zinatawala siasa za Zanzibar. Hata vijiwe vya Zanzibar vilikuwa vinatawaliwa zaidi na mazungumzo yahusuyo Muungano. Hivi sasa hali imegeuka, ukifuatilia kwa umakini Wazanzibari wanausifia zaidi Muungano huku Watanganyika wakibaki kunung’unika na kugugumia kwa maumivu.

Historia ya hivi karibuni inaonesha nchi nyingi zinatengana zaidi kutoka kuwa nchi moja na kuwa nchi mbili ama zaidi. Orodha ya majimbo yaliyojitenga na kuwa nchi ni ndefu; achilia mbali orodha ya majimbo ambayo yanafanya michakato na harakati za kujitenga. Nitakuwa sahihi nikisema hivi sasa ni mwendo wa nchi kutengana tu, kuungana ilikuwa zamani.

Kwa hiyo tusijidanganye kuwa hali ni shwari tukasahau changamoto zinazo ukabili Muungano wetu; ukweli ni kwamba pepo mchafu wa kujitenga yupo. Pengine amenyamaza tu kwa muda kwa sababu aidha anamwogopa Mchungaji anaye endesha Ibada au amejenga makao kabisa hatishwi na ibada anasubiri muda muafaka alianzishe.
Wakati tukisherekea miaka 61 ya Muungano wetu adhimu tukumbuke kuwa nyumba nzuri na imara inajengwa wakati wa amani.

Huu Wakati ambao Bara na Visiwani hali imetulia ndio Wakati mzuri kurekebisha Muungano wetu. Tusijidanganye kuwa Watanzania wanaridhishwa na huu Muungano, yapo mambo mengi ambayo ni vema yakashughulikiwa haraka mfano usimamizi na mgawanyo wa rasilimali za taifa, mgawanyo wa nafasi za ajira unao zingatia uhalisia, umiliki wa rasilimali ardhi, ukusanyaji wa mapato na mgawanyo wake, nafasi za uteuzi, haki za binadamu na uwakilishi kimataifa.

Watu mliopo karibu na Rais Samia mshaurini endapo atachaguliwa katika uchaguzi wa mwaka huu Katiba mpya ambayo pamoja na mambo mengine itatatua kero za Muungano iwe kipaumbele chake. Akisubiri mpaka 2029 atakuwa amechelewa sana na anaweza akajutia kuwa Rais wa Tanzania.

Haijalishi atakuwa amefanya mazuri kiasi gani lazima itafikia mahali atachokwa ndani na nje ya chama pengine pengine kiubinadamu tu vile vile kutoka na jinsia yake, Uzanzibari na hata dini. Ikija kutokea watu wakamchoka Rais na akakosa msaada kutoka kwa viongozi waandamizi wa chama chake hoja za Muungano lazima zitakuja kuibuka na kumyumbisha sana na inaweza kuleta dhahama kwa Taifa letu.

Tukumbuke G55 walivyo myumbisha Hayati Rais Mwinyi. Isingekuwa nguvu ya kisiasa aliyo kuwa nayo Mwalimu Nyerere sasa hivi Muungano ungekuwa na sura nyingine kabisa na pengine usingekuwepo. Sote tunakumbuka hivi karibuni kusu suala la bandari sura iliyo ibuka zaidi suala la kikatiba na Uzanzibari wa Mama. Kwa hiyo Mama wahi kufanyia kazi manung’uniko ya Muungano yanayo wakwaza wengi kabla hayaja kukuta ya Rais Mwinyi sababu najua unajua kwamba wapinzani wako watatoka bara ndani ya chama chako.

Serikali isifanye kosa kupuuza malalamiko na hoja za Watanzania kuhusu mambo yanayo wakwaza kuhusu Muungano wetu. Vile vile serikali itoe mfafanuzi kwa wakati kwa yale masuala ambayo watanzania watahitaji kuelimishwa sababu kuna baadhi ya mambo watu wanalalamika kutokana na kukosa elimu ama taarifa. Mfano watu wengi mpaka sasa wanajua ili kwenda Zanzibar Mtanzania wa bara sharti awe na passport jambo ambalo siyo kweli. Mara kadhaa nimesikia madai ya aina hii.

Wakati nasoma kidato cha sita katika Seminary moja, mwalimu alimuuliza swali mwanafunzi mwenzetu ambaye sasa hivi ni Padre ni jambo gani Tanganyika tutalikosa endapo Muungano utavunjika. Yule Mwanafunzi alijibu kuwa yapo mengi lakini kubwa zaidi atamisi sana jina Tanzania; tulicheka sana.

Ninachotaka kueleza ni kwamba kwa umri wa Muungano wetu ni ukweli usio pingika unamgusa kila Mtanzania, kila mmoja anauthamini kwa namna yake. Kwa hiyo wanao hoji mambo mbalimbali ya Muungano isitafsiriwe hawautakii mema ama wavunja amani.
 
"Kwa bahati mbaya Penzi letu na Liya la kwenye mtandao halikudumu sababu nilikuwa tayari nina mke, kule Facebook nilikuwa naingia kujifurahisha tu. Liya mpenzi wangu najua upo hai, ninafurahi kukutaarifu kuwa ule Muungano wa Tanzania unao upenda ulivuka salama mwaka 2014 na bado unadunda"

🤣🤣🤣🤣🤣


Ila vijana wa Bongo mna vituko basi tuu
 
Back
Top Bottom