Hivi ni kweli kuwa nyama nyekundu ya mifugo kama ng'ombe, mbuzi na kondoo humletea matatizo mgonjwa wa kisukari?
- Tunachokijua
- Myoglobin ni aina ya protini inayopatikana kwenye misuli ya wanyama. Pamoja na kazi zingine, protini hii husaidia kuhifadhi kiasi cha kutosha cha hewa safi ya oxygen pamoja na kuamua mgawanyiko wa nyama ambao huwekwa kwenye makundi mawili ya nyama nyeupe na nyama nyekundu.
Nyama nyekundu kwa kiasi kikubwa hujumuisha kundi kubwa la wanyama wanaofugwa mfano Nguruwe, kondoo na Ng'ombe.
Faida za nyama nyekundu
Nyama nyekundu ni chanzo kizuri cha protini, mafuta, madini chuma, zinc na aina mbalimbali za vitamini B.
Madini chuma huwezesha usafirishaji wa oxygen, Madini ya zinc huboresha mfumo wa kinga za mwili pamoja na kuzalisha vinasaba (DNA), Vitamini B12 huimarisha mfumo wa fahamu na protini ikisaidia kuponya majeraha ya mwili, kuzalisha kinga mwili, vimeng'enya na homoni za mwili pamoja na kuzalisha nishati.
Hivyo, pamoja na uwepo wa athari kadhaa zinazotajwa kuhusishwa na ulaji wa nyama nyekundu, bado kuna faida lukuki zinazohitajika katika kuimarisha afya ya binadamu.
Madhara kwa watu wenye kisukari
JamiiForums imezungumza na wataalam wa lishe pamoja na Madaktari ili kupata ufafanuzi wa athari za ulaji wa nyama hii kwa watu wenye kisukari. Katika mazungumzo hayo, tumebaini mambo yafuatayo;
- Inapotumika kwa kiasi kikubwa, huongeza ukubwa wa tatizo pamoja na kuongeza hatari ya kuugua kwa watu wasio na ugonjwa huo.
- Nyama nyekundu huongeza pia uwezekano wa kuugua magonjwa ya moyo, kiharusi na saratani.
Ushauri
Nyama nyekundu siyo mbaya inapotumika kwa kiasi. Kwa mujibu wa Taasisi ya World Cancer Research Fund International, unashauriwa kutumia kiasi cha gramu 700-750 kwa wiki.
Kwa lugha rahisi, uzito huo ni sawa na wastani wa robo tatu ya kilo.