JOHN ONDOLLO CHACHA:- Mtoto wa mwanamuziki aliyerithi soka.
INAWEZEKANA kabisa nyoka akazaa mjusi?
Sidhani; mara nyingi nyoka huzaa nyoka.
Lakini imetokea kwani nyoka amezaa mjusif
Msemo huo unaweza kwenda sambamba na
aliyekuwa mchezaji mahiri wa zamani, John
Ondolo Chacha ambaye alicheza katika timu
ya Lipuli ya Iringa msimu wa 1991-92
akitokea jijini Dar es Salaam.
Chacha ambaye alipachikwa majina ya Niva,
Pembe ya Ndovu na Thobias Ocholla
kutokana umahiri wake wa kucheza beki
namba nne katika timu alizowahi kucheza,
baba yake alikuwa ni mdau mkubwa wa
sanaa.
Akizungumza na mwandishi wa makala hii,
anaanza kwa kuelezea tofauti iliyoko kati ya
soka la sasa na la miaka waliyocheza wao.
Anasema, ilikuwa ni kwamba, wao
walijituma katika mazoezi binafsi, kuliko wa
sasa ambao ni wavivu.
Anaongeza kuwa, sababu ya uvivu wa
mazoezi, inasababisha kupozesha mpira
katika mashindano ya kimataifa, ambayo
Watanzania wengi wanajitokeza
kuwashangilia.
Chacha anasema, anashukuru elimu kubwa
aliyoipata kutoka kwa Kocha Abdallah
Kibadeni King Mputa, ambaye mara nyingi
alimpa mawazo mengi, ambayo yalimsaidia
katika kucheza soka.
Anaeleza, katika safari yake ya soka, alipata
elimu kutoka kwa aliyekuwa Naibu Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
Joel Bendera, ambaye aliwafundisha wakiwa
katika timu ya Shekilango huku Bendera
akiishi katika ghorofa za Shekilango.
Pamoja na kupata elimu kutoka kwa
makocha ambao wazoefu, lakini alitatizwa
na suala la uvumilivu wa kukaa katika timu
moja zaidi ya miaka minne.
Ananasema, alianza kusakata soka mwaka
1986-87 alipoajiriwa katika kiwanda cha
Alminium Africa kilichopo Temeke, ambako
alicheza msimu mmoja na kukutana na
kocha Kibadeni katika timu ya Future,
iliyokuwa na maskani yake Urafiki jijini Dar
es Salaam.
Akiwa Alminium, alikutana na wachezaji
wengi ambao baadhi yao walicheza Ligi
daraja la kwanza (sasa hivi Ligi Kuu
Tanzania bara), mmojawapo akiwa ni
kiungo Suleimani Ally aliyewahi kucheza
Yanga miaka ya 1987-88.
Hakudumu sana Alminium, akarejea timu
iliyoko karibu na nyumbani kwao
Shekilango ya Future, iliyokuwa na vijana
wengi ambao walikuja kuwa tishio katika
medani ya soka la Tanzania.
Alipokuwa Future, timu hiyo ilikuwa chini ya
Kibadeni kipindi hicho, ambako alikuwa ni
mfanyakazi wa kiwanda cha nguo cha
Urafiki akiwa ametokea masomoni nchini
Ujerumani kwenye kozi ya ukocha.
Kutokana na umahiri wake uwanjani,
Kibadeni alimpeleka kiwanda cha Urafiki na
kupata kazi kitengo cha ufundi wa magari,
akiwa pia ni mchezaji.
Akiwa Urafiki, alifundishwa pia na Salum
Madadi ambaye ni Ofisa wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), na kukutana na
wachezaji wengine kama Wema Juma,
Kenny Mwabulambo, Habibu Kondo, Muhesa
Kihwelu, Jumanne Ucheche ambaye baadaye
walihamia Lipuli ya Iringa na John Ngunde
ambaye sasa hivi ni mmojawapo ya Maofisa
Watendaji wa Mitaa jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo ilikuwa mojawapo ya timu ngumu
katika ligi ya soka Mkoa wa Dar es Salaam,
lakini iliishia ligi ya Kanda ya Dar es Salaam.
Kutokana na umahiri wa ufundishaji,
Kibadeni alichukuliwa na Chama cha Soka
Tanzania (FAT), sasa TFF kuifundisha timu ya
Taifa ya Tanzania Taifa Stars, hapo Chacha
akahamia Nyota Nyekundu yenye maskani
yake Kariakoo Mtaa wa Congo jijini na
kukutana na Faustine Kibingwa, Rosta
Ndunguru, Ayoub Mzee na John Bosco,
ambako aliendelea kupata uzoefu mkubwa,
kwa sababu mara kadhaa timu hiyo ilicheza
mechi za kirafiki na Taifa Stars.
Mara nyingi, Kibadeni alimweleza Chacha
kwamba, kwa jinsi anavyocheza soka,
atafika mbali zaidi ya Tanzania, ila kikubwa
zaidi ni kuzingatia miiko ya mchezo huo na
kuwa na uvumilivu.
Mwaka 1989, alichukuliwa na timu ya
kiwanda cha Twiga Cement kilichopo Wazo
Hill jijini Dar es Salaam, kutokana na umahiri
akiwa uwanjani, akapewa ajira kiwandani
hapo na kukutana na ofisa wa TFF hivi sasa,
Idd Mshangama akiwa kocha.
Mwaka 1991, alihamia Lipuli ya Iringa baada
ya kuonekana katika mashindano ya ligi
daraja la pili ambako alikutana na akina
Peter Lugenzi, Willy Komakoma, David Kika,
Elisha John, Nurdin Gogola na Hassan
Mwajeki.
Kipindi hicho kikosi cha Lipuli kilikuwa chini
ya kocha Mzambia, Donald Phiri ambaye
aliwahi kuwa mchezaji wa timu ya Taifa ya
Zambia na Pascal Bella, ambako alikutana na
viwango zaidi, kwa sababu alipata nafasi ya
kucheza na timu kama Simba, Yanga, Coastal
Union, African Sports na Milambo ya Tabora.
Pamoja na timu yao kuwa bora katika ligi
daraja la kwanza, lakini anaikumbuka mechi
waliyofungwa mabao 5-0 na Pamba ya
Mwanza, ambayo ilikuwa na wachezaji
mahiri kama Kitwana Seleman, Nteze John
Lungu, Madata Lubigisa na wengineo.
Anasema, cha kushangaza baada ya mchezo
huo uliochezwa jijini Mwanza, tajiri wa
machimbo ya Mgusu aliialika timu hiyo kwa
gharama zake kucheza na timu yake ya
mgodini.
Katika mchezo huo, alikutana na
mshambuliaji mahiri wa timu hiyo, Eliud
Ngessa ambaye alicheza naye utafikiri
wanawania nafasi ya kufuzu kombe la
dunia, hadi mwamuzi wa mchezo aliwatoa
nje kwa kadi nyekundu.
Anaongeza kuwa, cha kushangaza zaidi
baada ya kutolewa wachezaji hao, mpira
ulipooza sana, hali ambayo ilisababisha
mwamuzi huyo kuwaita na kuwaamuru
warejee kwa mara nyingine uwanjani, hali
ambayo hakuelewa refa huyo alitumia
sheria ipi, kwani mchezaji akitolewa nje kwa
kadi nyekundu haruhusiwi kurejea
uwanjani mara nyingine.
Kwa kuwa tamaa yake ilikuwa ni kucheza
nje ya mipaka ya Tanzania, akatoka Lipuli na
kurejea Dar es Salaam msimu wa 1992-95,
ambako baadhi ya viongozi wa timu ya
Konde ya Pemba, wakamtaka akachezee
timu yao katika ligi kuu kisiwani humo.
Akiwa na wachezaji wenzake sita kutoka
Dar es Salaam, Abdul Ramadhani Mashine,
Mohamed Mwape, Abdallah Mohamed, Omar
Mbweza na Ramadhani Abdallah, baadaye
timu hiyo ilifuzu kucheza ligi ya Muungano
katika mashindano ya kila mwaka.
Wakati akiwa katika hatua za mwisho za
mkataba wake, timu za Jamhuri na Kipanga
ambazo zote ni za Jeshi la Wananchi
zilimuhitaji, alikataa na kurejea Dar es
Salaam, ambako alikutana na Kibadeni kwa
mara nyingine, ambaye alimwelekeza
kwamba, kutokana na umahiri alionao
katika soka, asubiri kidogo atamtafutia timu.
Kwa kuwa hakuwa na uvumilivu, alielekea
Kenya na kufanya majaribio timu za AFC
Leopards, Kenya Breweries na Mumias Sugar
ambako ndipo alipofanikiwa timu hiyo
iliyokuwa ikifundishwa na kocha Dennis
Munyendo na kukutana na nyota kama
akina Mark Serengo na Nika Hammer.
Mwaka 1996-98 akajiunga na Posta ya
Kakamega nchini humo, ambako akiwa
katika timu hiyo, alipata hisia ya kumrejea
Mungu kwa kenda chuoni kupata elimu ya
dini katika chuo cha Mtakatifu Makarios cha
Kenya na kufanikiwa kupata cheti cha
uchungaji.
Anasema, kipaji chake katika soka, alikirithi
kutokea kwa babu yake, aliyekuwa akiitwa
John Alyango, ambaye aliwahi kucheza
Kombe la Gossage.
John Chacha, ni mtoto wa pili kuzaliwa kati
ya 12 wa marehemu Mzee Ondolo John
Chacha, ambaye alikuwa ni mojawapo ya
wadau mahiri wa muziki na sanaa hapa
nchini, ambaye aliweka mikakati ya kukuza
na kuendeleza sekta hiyo kwa kujenga kituo
kikuu nyumbani kwake Shekilango jijini Dar
es Salaam.
John aliyezaliwa miaka 45 iliyopita, hivi sasa
ana mke na watoto wanne na ni mchungaji
wa kanisa la Full Categro lililopo katika kituo
cha Sanaa Shekilango jijini Dar es Salaam.
Anasema, mipangilio iliyopo kwa sasa ni
kukuza na kuendeleza sanaa sambamba na
michezo mignine kama soka na kuwa kituo
cha kusaka vipaji na kuviendeleza kimataifa.
Anatoa wito kwa TFF, kufanya mabadiliko
makubwa ya Kamati ya Ufundi, ambayo
inaonekana kuelemewa na mzigo, kutokana
na kwamba, hivi sasa Tanzania hakuna timu
inayoeleweka ya Taifa.
Anapendekeza, Kamati hiyo inaweza
kuongozwa na Watanzania kama Kibadeni,
Adolf Rishard na Charles Boniface Mkwasa,
ambao wana elimu ya kutosha ya kuifanya
kazi hiyo.
Anatoa wito pia kwa mawakala, kuwaandaa
wachezaji kisaikolojia ili wawe mfano bora
katika timu za nje na kuwataka pia
wachezaji wa sasa, kuacha uvivu na
kumuiga Mohamed Ngulungu ambaye
alicheza timu ya Taifa miaka 10 bila ya
kupoteza uwezo wake.