Nyuma ya pazia kuendelea tatizo upungufu matundu ya vyoo shuleni

Nyuma ya pazia kuendelea tatizo upungufu matundu ya vyoo shuleni

UTPC

Journalists' Union
Joined
Apr 17, 2026
Posts
51
Reaction score
38
Licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali katika kuwekeza na kuboresha sekta ya elimu nchini, hali halisi bado inaonyesha uwepo wa pengo kubwa la miundombinu.

Katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, shule nyingi za msingi na sekondari, zinakabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa matundu ya vyoo, hali hii sio tu kwamba inavunja utu wa wanafunzi, bali inaendelea kuhatarisha afya zao kila siku kutokana na tishio la milipuko ya magonjwa yanayotokana na uchafuzi wa mazingira kwa kujisaidia vichakani.
Screenshot 2026-10-09 173428.png

MWANTINI.JPG

Muonekano wa Vyoo vya Shule ya Msingi Mwantini, Manispaa ya Shinyanga.​

Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Nipashe kwa kipindi cha miezi mitatu, umebaini shule nyingi licha ya upungufu huo, pia zina vyoo vilivyochakaa na visivyo na mifumo rafiki, na hakuna vyumba maalumu vya kujistiri na hedhi kwa wanafunzi wa kike.

Ukosefu huu wa faragha unawanyima mabinti haki yao ya msingi ya hifadhi ya nafsi na unadhorotesha mahudhurio yao darasani, jambo linaloonyesha wazi kutowajibika kikamilifu kwa mamlaka husika katika kutatua kero hii.

Ukirejelea Mwongozo wa Taifa wa Maji, Usafi wa Mazingira na Afya Shuleni (SWASH) wa mwaka 2009, serikali iliweka viwango rasmi kuwa shule inapaswa kuwa na uwiano wa tundu moja la choo kwa wanafunzi wa kike 20 (1:20) na tundu moja kwa wavulana 25 (1:25). Viwango hivi viliwekwa ili kuhakikisha afya na usalama wa watoto vinazingtiawa.

Pia soma ~ Afya za wanafunzi wengi Manispaa ya Shinyanga ipo hatarini, upungufu wa vyoo unavyowasukuma kujisaidia vichakani

Hata hivyo, pale ambapo viwango hivyo havifikiwi kama ilivyo katika Manispaa ya Shinyanga, afya, na usalama wa wanafunzi huathirika moja kwa moja.

Mbali na tatizo la uchache wa matundu, shule nyingi zinakabiliwa na ukosefu wa maji tiririka kwa ajili ya kunawa mikono na sabuni, baada ya kutoka chooni pamoja na kusafisha vyoo na kuendelea kuwa vichafu, na hivyo kuchochea zaidi maambukizi .

Athari za changamoto hii imekuwa ikiwakumba sana wanafunzi wa kike, hususan wanapokuwa katika hedhi na kushidwa kujistiri vizuri sababu ya vyoo kuwa vichafu, licha ya ukosefu wa vyumba maalumu, na wengi hulazimika hulazimika kuondoka shuleni na kurudi nyumbani kujihudumia.

Uchunguzi wa kina unabaini kuwa chanzo kikuu cha kuendelea kwa tatizo hili ni ufinyu wa bajeti zinazotengwa na serikali, kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya usafi wa mazingira mashuleni (SWASH), nakusabisha idadi kubwa ya wanafunzi kujisaidia vichakani, ukosefu wa vyumba vya hedhi na kutarisha afya zao.

Ofisa Takwimu wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Bopali Mwakiluma, anakiri kuwa fedha zinazotengwa katika kukabiliana na upungufu wa matundu ya vyoo shuleni na vyumba maaalum vya kujistiri na hedhi kwa wanafunzi wa kike hazikidhi hata robo ya mahitaji yaliyopo.

Anasema, wana upungufu wa matundu ya vyoo 1,145, mahitaji 2009 na yaliyopo ni 864, huku wakiwa na jumla ya wanafunzi 43,078 wa shule za msingi, wavulana 21,233 na wasichana 21,845.

“Katika mwaka wa fedha 2026/2027, halmashauri imetenga kiasi cha sh. milioni 118.8 pekee, fedha ambazo zimepangwa kujenga matundu 54 tu ya vyoo na vyumba maalum vya kujistiri hedhi, ukilinganisha takwimu hizi na upungufu wa matundu 1,145, ni wazi kuwa kasi ya utatuzi wa tatizo hili ni mdogo,”amesema Mwakiluma.

Diwani wa Kolandoto Manispaa ya Shinyanga Moses Mshagatila, anasema kutokana na ufinyu wa bajeti wa halmashauri katika utatuzi wa matundu ya vyoo, wao kama viongozi wa Kata wameanza kuwajibika kutatua tatizo hilo kwa kushirikiana na wananchi, kuchangia nguvu kazi, mifuko ya saruji ili kuokoa afya za wanafunzi.

Anasema changamoto hiyo ya upungufu wa matundu ya vyoo ipo hasa katika shule ya msingi Wame yenye wanafunzi zaidi ya 400, na shule ya msingi Mwamagunguli “A” yenye wanafunzi zaidi ya 300.

Analeleza kuwa wanafunzi katika shule hizo mbili, wamekuwa wakijisaidia vichakani, na wakati mwingine wakibanwa na haja kubwa, hukimbilia kwenye makazi ya watu yaliyopo jirani na shule.

“Hili zoezi kuchangishana tumeshalianza katika shule ya Msingi Kolandoto, na tumepanga kujenga matundu manne ya choo, mawili ya walimu na mawili ya wanafunzi wa kike, tukiwa na lengo la kuanza kupunguza tatizo hilo katika shule zetu za Kata ya Kolandoto wakati tukiendelea kusubili bajeti ya serikali,” amesama Mshagatila

Diwani wa Kata ya Kizumbi Rubeni Kitinya, anasema, wao kama viongozi wamekuwa wakiwajibika kutatua tatizo la upungufu wa matundu ya vyoo shuleni kwa kushirikiana na wananchi pamoja na kutafuta wadau.

Anasema, Kata hiyo ina shule za msingi za serikali tano, lakini vyoo vyake vikizamani na vimechakaa.

“Mfano, shule ya msingi Lyandu ,vyoo vyake vimechoka na havifai kwa matumizi ya wanafuzi, shule ya msingi Mwamashele yenyewe vyoo vyake vimejaa na mpaka sasa wanafunzi wanajisaidia vichakani, hali ni mbaya sana,” anasema Kitinya.

“Sisi kama viongozi ngazi ya kata, tumekuwa tukiwajibika kutatua changamoto hizi ambazo zipo ndani ya uwezo wetu, lakini matumaini yetu makubwa ni bajeti ya halmashauri, hata wananchi wakichangia nguvu kazi, bado kuna vifaa vitahitaji pesa tu,” amesema Kitinya.

Anatolea mfano katika shule ya Msingi Buyambelele, ambayo wanafunzi wake walikuwa katika hali mbaya zaidi ya kiafya, kwamba licha ya juhudi za wananchi, pia waliibana Halmashauri na ikatoa sh.milioni 8.6, na kujengwa matundu manne ya choo, yakiambatana na chumba maalumu cha kujistiri na hedhi, na chumba cha wanafunzi wenye ulemavu.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, akisoma taarifa ya utekelezaji ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Julai ya kuanzia Novemba 2025 hadi Juni 2026, amesema mkoa huo umeshapokea sh.milioni 205.2 kwa ajili ya kuboresha miundombinu mbalimbali ya sekta ya elimu, yakiwamo matundu ya vyoo.

Anasema, kutokana na fedha hizo, anasisitiza halmashauri zote za mkoa huo, kuweka kipaumbele katika bajeti zao, kwa kujenga vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, pamoja na vyumba maalumu vya kujistiri na hedhi kwa wanafunzi wa kike, ili wasome katika mazingira salama na rafiki.

Daktari wa Magonjwa ya dharura na Mlipuko kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Kambi Buteta, anasema msongamano wa wanafunzi kwenye vyoo vichache, unachochea maambukizi ya magonjwa ya mfumo wa chakula.

Anasema, vyoo salama shuleni ni muhimu pamoja na miundombinu ya kunawa mikono, kwamba mwanafunzi wakati wa mapumziko akitoka chooni wengine huenda kununua vitafunwa na kuanza kula, hapo tayari atakuwa ameshakula kinyesi, na kusababisha magonjwa ya matumbo na minyoo,” amesema Dk. Buteta.

Shule ya Msingi Mwantini ni miongoni mwa shule ambayo lifikiwa na uchuguzi wa Nipashe, ambayo ina idadi kubwa ya wanafunzi, lakini vyoo ni vichache na hakuna chumba maalum cha kujistiri na hedhi kwa wanafunzi wa kike, na kuhatarisha afya zao.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule ya Msingi Mwantini Pili Mbogo, anasema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 768, wavulana 364 na wasichana 404, na ina matundu ya choo 14, huku uhitaji ukiwa ni 17, na haina chumba maalumu cha kujistiri na hedhi kwa wanafunzi wa kike.

Anasema, upungufu huo wa matundu ya choo umekuwa ukisababisha mrundikano wa wanafunzi wanapokwenda kujisaidia wakati wa mapumziko, huku wengine wakijisaidia vichakani na nyuma ya majengo ya vyoo.

“Kipindi cha masika wanafunzi huwa wanaugua sana magonjwa ya tumbo na kuharisha, na huwa tunawapa ruhusa ya kwenda nyumbani,” anasema Mbogo.

Mwalimu wa Afya, Lishe na Mazingira shuleni hapo, Emmanuel Lushu, anasema matundu 14 ya choo katika shule hiyo hayakidhi mahitaji ya wanafunzi, ikilinganishwa na idadi iliyopo ya wanafunzi 768, na kwamba suala hilo walishalifikisha serikalini, lakini hadi sasa hakuna utekelezaji wowote uliofanyika.

Mwanafunzi Geofrey Charles wa Shule ya Msingi Mwantini, anasema kutokana na upungufu wa matundu ya choo shuleni hapo, baadhi ya wanafunzi hujisaidia pembeni na kuchafua mazingira, jambo linalowasababishia kuugua magonjwa ya tumbo mara kwa mara.

Charles ambaye ni Mwenyekiti wa Klabu ya Mazingira katika shule hiyo, anasema licha ya kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa wanafunzi wenzao, lakini kikwazo kikubwa kimekuwa ni upungufu wa matundu ya vyoo na kuendelea kuwa hatarini kiafya.

Kwa mujibu wa kanuni za elimu Masharti kuhusu miundombinu, usafi wa mazingira, na ukaguzi wa afya shuleni za mwaka 2002, zilizotungwa chini ya sheria ya elimu, shule zinapaswa kuwa na vyoo vilivyojengwa kwa kuzingatia viwango, na maelekezo ya wizara inayohusika na elimu, pamoja na kuwa na maji safi na salama.


Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.
 
Back
Top Bottom