Nyumba ya tajiri yateketea kwa moto
Na Christina Gauluhanga, Polisi
MOTO mkubwa umezuka ghafla katika nyumba inayomilikiwa na Reginald Mengi (62), ambaye ni Mwenyekiti wa Kampuni za IPP na kuteketeza mali yote iliyokuwemo ndani.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kanda Maalum Dar es Salaam, Pius Sheka amesema kuwa tukio hilo limetokea jana saa 5 usiku, Kinondoni Hananasif.
Amesema nyumba hiyo ya ghorofa ina vyumba sita ambapo viwili vilivyokuwa ghorofani viliteketea vyote na mali iliyokuwemo ndani.
Chanzo cha moto huo inadaiwa kuwa ni hitilafu ya umeme iliyoanzia chumba kikuu (Master bedroom) kwenye kiyoyozi.
Moto huo ulizimwa na Kikosi cha Zimamoto cha Jiji kwa kushirikiana na wananchi na thamani ya mali iliyoteketea bado haijafahamika.
Nao, watoto wawili wamekufa na wengine wawili wamejeruhiwa baada ya moto kuzuka ghafla chumbani kwao wakiwa wamelala Manzese Midizini.
Kamanda Sheka amesema tukio hilo limetokea leo alfajiri saa 7 usiku, Manzese Midizini.
Amesema nyumba hiyo ina vyumba tisa ambavyo vinakaliwa na wapangaji ambapo chumba cha mpangaji Getrude Mwiru (40), kiliteketea chote na kusababisha vifo cha watoto hao wa ndugu yake waliokuja jijini wakitokea Dodoma kusalimia.
Amewataja watoto hao kuwa ni Allex Mtenda (7) na mwingine Baraka. Waliojeruhiwa ni Getrude na Farida Brigthon (22).
Majeruhi wamelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na maiti wamehifadhiwa chumba cha maiti ya Hospitali ya Mwananyamala.
Katika tukio lingine, mtoto Samiha Mohamed (2), mkazi wa Mwananyamala kwa Manjunju amekufa baada ya kushika mlango wa chuma katika kibanda cha biashara kilichopo nje ya nyumba yao.
Kamanda Sheka amesema kuwa tukio hilo limetokea jana saa 1 asubuhi, Mwananyamala.
Amesema mtoto huyo alifikwa na mauti hayo baada ya kushika mlango wa chuma uliokuwa na hitilafu ya umeme katika kibanda cha biashara cha Shaban Hozza.
Maiti wamehifadhiwa chumba cha maiti Hospitali ya Mwananhyamala na polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi wa tukio hilo.
Naye, mwanaume mmoja ambaye hakuweza kufahamika mara moja jina wala makazi yake anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 na 30 amekufa baada ya kugongwa na gari wakati akivuka barabara ya Bagamoyo.
Kamanda Sheka amesema kuwa tukio hilo limetokea jana saa 1 asubuhi, Basihaya.
Marehemu alikuwa amevaa shati la maua maua na suruali nyeusi.
Maiti imehifadhiwa chumba cha maiti hospitali ya Mwananyamala.
finito...