OFISA Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Fred Kaombwe (28), amejiua kwa kijipiga risasi kichwani baada ya kumkuta mkewe akiwa na mwanamume mwingine katika baa mojawapo mjini Dodoma.
Baada ya hapo, Kaombwe inadaiwa alimkimbiza mkewe huyo Vicky Kaombwe (34) na baadaye alimpiga risasi na kumjeruhi sehemu za mbavu.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Elizabeth Masiaga alisema ,Kaombwe alijipiga risasi juzi saa 3.00 usiku katika mtaa wa Madole eneo la Kigamboni mjini Dodoma.
Kamanda Masiaga alisema, Kaombwe alifariki dunia wakati akipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kupatiwa matibabu wakati mkewe Vicky amelazwa katika hospitali hiyo.
Hata hivyo, hali ya majeruhi huyo anayefanya kazi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana mjini Dodoma bado si nzuri na Kamanda Masiaga aliahidi kutoa taarifa zaidi mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi.
Akizungumza na gazeti hili, mkwe wa marehemu, Thadei Nghwaya, alidai kulikuwa na ugomvi wa kifamilia na kwamba, Kaombwe alijipiga risasi kifuani na si kichwani baada ya kuhisi kuwa amemuua mkewe.
Nghwaya alisema, baada ya vipimo, ilibainika na wataalamu kuwa risasi aliyojipiga Kaombwe ilipitiliza na haikubaki mwilini.
Akizungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa jina, mmoja wa mashuhuda alidai kuwa, kabla ya mauaji hayo Kaombwe alimkuta mkewe akiwa na mwanamume mwingine katika baa.
Alidai kuwa, baada ya hapo, Vicky alikimbilia katika gari lake na kuondoka nalo huku akifukuzwa na mumewe katika gari lingine hadi walipofika nyumbani kwao eneo la Kigamboni.
Shuhuda huyo alidai kuwa, Vicky aliposhuka katika gari kwa lengo la kufungua geti, Kaombwe alikuwa ameshafika akatoka ndani ya gari lake na kumpiga risasi mkewe.
Kaombwe alisafirishwa jana kwenda Tabora kwa maziko.
source: habari leo
MAONI; sasa hapa kuna nafuu gani?
anyway wamama na wadada jamani kuna wanaume ni dhaifu sio vizuri kuchakachua
mali zao, wanaume kujiua kwa ajili ya penzi, inaingia akili kweli