Inadaiwa kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi, amekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kusitisha mkutano wake uliopangwa kufanyika kesho Julai 23,huko Buriaga, Temeke jijini Dar es Salaam.
Barua inayodaiwa kuandikwa na Sisty Nyahoza, Naibu Msajili wa vyama.
- Tunachokijua
- Mamlaka ya Ofisi ya Msajili ni kama yalivyoainishwa na taarifa iliyochapishwa tarehe 22/04/2016 kwenye Gazeti la Serikali No 143 & 144 hufanya majukumu ya uratibu wa uhusiano katika vyama vya siasa na Serikali.
Ofisi hii imejikita katika usimamizi wa Sheria ya Vyama vya Siasa Na 5 ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama za uchaguzi ya mwaka 2010 ili kuhakikisha uwepo na ukuaji wa demokrasia ya vyama vingi nchini.
Madai ya Kuzuiwa kwa Mkutano wa CHADEMA
Yakiwa yamebaki masaa machache kabla ya kuanza kwa Mkutano un anaohusu masuala ya Uwekezaji Bandarini unaoihusu Serikali ya Tanzania na Kampuni ya DP World ya Dubani, taarifa zinazodai kuzuiwa kwa mkutano huu zimeanza kusambaa mtandaoni.
Julai 22, 2023, saa 5:17 usiku, Kurasa za Mitandao ya kijamii inayomilikiwa na Maulid Kitenge ilichapisha habari hiyo ikisema:
Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi, amekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kusitisha mkutano wake uliopangwa kufanyika kesho huko Buriaga, Temeke jijini.
Akizungumza leo, Jaji Mutungi amekikumbusha Chama hicho kuheshimu na kufuata sheria za nchi zinazosimamia usajili wa vyama huku akiwaita ofisini Jumatatu.
Baadae, Barua inayotajwa kuandikwa na Naibu Msajili wa vyama, Sisty L. Nyahoza yenye wito huo huo wa kusitisha mkutano ilianza pia kuonekana mtandaoni.
Barua hiyo ilienza mbali zaidi kwa kuwaita viongozi wakuu wa CHADEMA walifike kwenye ofisi yake, Julai 24 kwa ajili ya mazungumzo.
Sehemu ya barua hiyo inasema:
“Hivyo, Msajili wa Vyama vya Siasa akiwa ndiye mwenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa yenye masharti ya yanayokataza masuala hayo na akiwa ni mlezi wa vyama vya siasa, anawasihi CHADEMA msitishe mkutano huo a viongozi wen waku kufika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa tarehe 24 Julai 2023 saa nne asubuhi kuonana naye, ili kuongea kuhusu suala hilo a masuala mengine ya utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa.”
Ukweli wa taarifa hii
JamiiForums imebaini kuwa taarifa hizi ni sahihi, zimetolewa na mamlaka husika.
Ukweli wa taarifa hii umethibitishwa pia na Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, jioni ya Julai 23, 2023 wakati mkutano huo unaendelea. Amesema:
“Jana jioni nilipokea barua ya msajili wa vyama vya siasa, kama mtendaji mkuu wa chama akinieleza kwamba tuahirishe, tuufute huu mkutano wa leo. Sasa kwa sababu nilipokea nje ya muda wa ofisi, na chama chetu kinafanya kazi kitaasisi, kwa vikao, nikabaki nayo. Na busara zikanielekeza kwamba tuendelee na mkutano huu.”
Awali, Julai 22, 2023, Jeshi la Polisi lilikiri kupata taarifa ya uwepo wa Mkutano huo na kusisitiza ufanyike kwa kuzingatia sheria zilizowekwa.
Mkutano huu unaungwa mkono na CHADEMA pamoja na Sauti ya Watanzania, klabu maarufu iliyoanzia kwenye mtandao wa Clubhouse ikiwa na mkusanyiko wa watu wengi ikiwemo watanzania waishio nchi za nje (Diaspora).
Baadhi ya sababu zilizopelekea Ofisi ya msajili kutoa wito wa kusitisha Mkutano huo ni CHADEMA kualika watu wasio wanachama wake kuhuduhuria mkutano huo.
Miongoni mwa watu hao ni viongozi wa dini na taasisi nyingine ikiwemo Rais wa Chama cha Wanasheria cha Tanzania Bara (TLS) pamoja na kutoa matangazo ya mkutano yenye picha za viongozi wa dini wakiwa na nguo rasmi za taasisi zao za dini.
Kwa mujibu wa msajili, jambo hili sio sawa, ni ukiukaji wa sheria za nchi zinazokataza vyama vya siasa kuwa na udini na kutumia dini kufikia malengo yake ya kisiasa.
Pia ni ukiukaji wa sheria zinazokataza taasisi za dini kufanya shughuli za kisiasa hivyo amewataka CHADEMA kufika ofisini kwake, Julai 24, 2023 kwa ajili ya mazungumzo yanayohusu utekelezaji wa Sheria ya vyama vya siasa.
Akijibu wito wa kufika Ofisi ya Msajili wa vyama, Mnyika amebainisha kuwa CHADEMA hakitakwenda kwa sababu ni chama kinachosikiliza maoni ya umma.