Hii tamu zaidi
Ole Sendeka ambwaga mshirika wa Lowassa
Na Charles Ngereza
Ashinda kesi aliyopakaziwa ya kushambulia
Pia alidaiwa kutishia kuua kwa bastola
Iliibuliwa wakati wa mkutano alioandaa Lowassa
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, akipongezwa na baadhi ya wananchi wa jimbo lake baada ya kushinda kesi iliyokuwa ikimkabili ya kumshambulia Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Arusha, James Millya mwaka jana wilayani Monduli.
Ile kesi ya jinai dhidi ya Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, ambayo chimbuko lake ni mkutano wa wazee wa Kimasai ulioitishwa na Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, imetupwa na mahakama.
Kesi hiyo ilitupiliwa mbali jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Devota Minja, baada ya kuthibitika kwamba ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi wa upande wa mashitaka ulikuwa dhaifu na wa kujichanganya hivyo kukosa nguvu ya kisheria kumfanya Sendeka awe na kesi ya kujibu katika kesi hiyo, Sendeka alikuwa akishitakiwa kwa tuhuma za kutishia kwa bastola na shambulio la kudhuru mwili dhidi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana CCM (UVCCM) Mkoa wa Arusha, James Millya.
Millya kada kijana wa CCM, wakati kesi hiyo ikiendeshwa alidaiwa kuwa anaishi kwenye moja ya nyumba za Lowassa iliyoko mkoani Arusha.
Wakati usikilizaji wa kesi hiyo ukiendelea, jopo la mawakili watano wa upande wa utetezi wakiongozwa na wakili Mpaya Kamala, uliwasilisha hoja za kutupwa kwa kesi dhidi ya mteja wao kwa hoja kuwa mashahidi wa upande wa mashitaka walijichanganya na kupingana katika ushahidi wao mahakamani.
Aidha, Mahakama hiyo ilieleza kuwa ushahidi uliotolewa na mtu aliyemjazia fomu mlalamikaji haukuwa na hoja ya msingi kwa kuwa hakuwa na sifa za kuwa daktari.
Baada ya Hakimu Minja kusoma uamuzi huo, umati mkubwa wa wafuasi wa Sendeka kutoka maeneo ya Simanjiro, Longido na Arusha walianza kupiga mayowe mahakamani wakiashiria kufurahia maamuzi hayo.
Wananchi hao walikuwa wamevaa mavazi ya Kimasai huku baadhi yao wakiwa wameshika mabango mbalimbali moja likisomeka Hata Yusufu alisingiziwa kubaka na baadaye kuonekana hana hatia.
Wananchi hao walijazana katika eneo la mahakama wakipongezana kufuatia uamuzi huo wa mahakama.
Shamrashamra za wafuasi wa Sendeka zilisababisha shughuli za mahakama kusimama kwa muda huku watumishi wakitoka nje kushuhudia umati wa watu waliokuwa mahakamani kujua hatma ya mbunge huyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wananchi wa jamii ya Kimasai waliokuwepo mahakamani wanaokadiriwa kufikia 500 walikuwa wakiruka na wengine kupandwa na mori wakati wakimpa mkono wa hongera Sendeka, ambaye ni mbunge wao.
Mara baada ya kuondoka katika eneo la mahakama, Wamasai hao waliendelea na maandamano yao ya amani wakimzunguka mbunge wao huku wakiwa na silaha zao za jadi hadi eneo la Makao Mapya ambapo walianza maandalizi ya tafrija kubwa ya kupongezana iliyotarajiwa kufanyika jana jioni. Akizungumza mara baada ya kufika katika eneo la Makao Mapya, Sendeka aliishukuru mahakama kwa kumtendea haki katika kesi hiyo aliyodai ilipikwa na kutungiwa uongo na maadui zake katika ulingo wa kisiasa mkoani Arusha na Manyara. Hata hivyo, hakuwataja kwa majina. Binafsi nilikuwa radhi kupokea uamuzi wowote, kama nilivyowaahidi wenzangu wakati kesi hiyo ikianza Januari mwaka jana, niliwaambia waende kuendelea na kazi za kujenga Taifa kwa kuwa niliamini kuwa mahakama zetu zina hadhi ya kuaminiwa na zinatenda haki, alisema Sendeka.
Alidai kuwa hata kama angeambiwa ajitetee angeweza kusaidia umma kupata ukweli wa upande wa pili wa shilingi katika sakata hilo.
Ninachoweza kusema nikiwa Mkristo nawasamehe wote walionitendea haya kwa dhamira ovu wakiwa na nia mbaya, lakini kwa kuwa wananchi wa Simanjiro na Watanzania wenzangu wamekuwa wakifika katika mahakama hii toka siku ya kwanza kwa gharama zao kunisindikiza kwa nia ya kuweka kumbukumbu sawa na kulinda hadhi yetu dhidi ya wale waliokusudia kuharibu hadhi na heshima yetu, nitazungumza nao kama watanikubalia niwasamehe, wakikataa tutawataka watuombe radhi na kusafisha majina yetu, alisema Sendeka.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Minja alisema kuwa anakubaliana na hoja za upande wa utetezi kuwa mtuhumiwa hana kesi ya kujibu na mahakama imetupilia mbali kesi hiyo.
Alieleza kuwa mahakama imeziangalia kwa makini hoja za pande zote na misingi ya kisheria ya makosa ya jinai na kubaini kuwa Mbunge huyo hana kesi ya kujibu.
Nipashe ilijaribu kuwasiliana na upande wa Jamhuri kupata maoni yake kama unakusudia kukata rufani na wakili wa serikali, Hashim Ngole, alisema kuwa unajipanga kujua la kufanya baada ya uamuzi huo wa mahakama.
Awali mawakili wa utetezi wakiongozwa na Kamala waliiambia mahakama kuwa madai ya upande wa mashitaka hayakuwa na msingi wowote na hayana nguvu ya kisheria wa kuifanya mahakama kutamka kuwa mteja wao ana kesi ya kujibu.
Alisema kuwa mashahidi wote waliotoa ushahidi walipingana wao kwa wao huku wengine wakitoa ushahidi wa kusikia ukiwa na mapungufu makubwa ya kisheria ya kuweza kuisadia mahakama kumtendea Sendeka haki.
Aidha, mawakili katika hoja zao walisema kuwa mahakama kuendelea na kesi hiyo ingekuwa ni kupoteza muda wa mahakama na mawakili wa pande zote kutokana na kila jambo kuwa wazi kisheria kuwa mashahidi waliotoa utetezi hawana sifa ya kuisaidia mahakama kutenda haki.
Walidai kuwa katika ushahidi wa shitaka la pili, mashahidi wa upande wa mashitaka namba 6 na 7 waliiambia mahakama kuwa shahidi namba mbili, Parseko Kone, hakuwa katika eneo la tukio na kwamba shahidi huyo aliiambia mahakama kuwa alimwona mshitakiwa akishika bastola na kumwelekezea Millya.
Aliendelea kuiambia mahakama kuwa katika shitaka la kwanza la shambulio la kudhuru mwili, shahidi namba 2, 6 na 7 waliiambia mahakama kuwa shahidi namba 5 hakuwa katika eneo la tukio na alitoa ushahidi wa kumwona Sendeka akimpiga Millya.
Kuhusu ushahidi wa tabibu kutoka hospitali ya Wilaya ya Monduli kujaza fomu namba tatu, wakili mwingine wa utetezi, Michael Ngalo, alidai kuwa upande wa mashitaka ulisisitiza kuwa ushahidi huo ulikuwa na upungufu kutokana na kujazwa na mtu asiyeruhusiwa kufanya kazi hiyo kwa mujibu wa sheria.
Mbunge huyo alikuwa akituhumiwa kutenda makosa hayo yaliyotupiliwa mbali Januari 9, mwaka jana majira ya saa 10 jioni katika Chuo cha Ualimu Monduli wakati wa mkutano huo.
Ilidaiwa katika maelezo ya awali mahakamani hapo kuwa siku ya tukio
mtuhumiwa alikuwa anahudhuria mkutano ulioandaliwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, uliokuwa na lengo la kuzungumzia suala la elimu kwa watoto wa kike wa jamii za wafugaji wa Kimasai ambapo baadhi ya wajumbe walitofautiana wakati wa uchangiaji wa mada zilizowasilishwa. Ilidaiwa kuwa baada ya kutoka mapumziko ya chakula cha mchana ndipo Sendeka alimshambulia Millya na kumsababishia maumivu na kumtishia kwa bastola yake.
Yaliyojiri kesi ya Sendeka Jan.2009 - Machi 2010
Nipashe Januari 10, 2009: Mkutano wa Lowassa wazua balaa Monduli
Mkutano wa viongozi wa jadi wa kabila la Kimasai ulioitishwa na kiongozi wake aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, umezua balaa baada ya Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM) na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, James Ole Millya, kurushiana makonde mazito hadharani.
Nipashe Januari 13, 2009: Polisi bado kuamua kumshtaki Sendeka.
Jeshi la Polisi mkoani Arusha, limesema halina mamlaka juu ya hatma ya Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, kufikishwa mahakamani au la, kufuatia tuhuma za kumpiga ngumi na kutishia kumuua Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Arusha, James Ole Millya.
Nipashe Januari 17, 2009: Kesi ya Sendeka yatikisa Arusha
Wamasai wengi wajitokeza kumuunga mkono
Wataka kuandamana jimboni Simanjiro
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, kujibu shtaka la kumshambulia na kumdhuru mwili Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Arusha, James Ole Millya.
Nipashe Machi 13, 2009: Kesi ya Sendeka kunguruma Aprili 20
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha itaanza kusikiliza kesi inayomkabili Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, ya kumshambulia Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Arusha, James Ole Millya, Aprili 20, mwaka huu.
Nipashe Aprili 21, 2009: Kesi ya Sendeka yaanza kunguruma
Hatimaye kesi inayomkabili Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, imeanza kunguruma.
Nipashe Mei 28, 2009: Mbunge Sendeka augua, kesi yapigwa kalenda
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, imeahirisha kesi ya shambulio la kudhuru mwili na kutishia kuua kwa silaha inayomkabili Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, hadi Julai 29, mwaka huu, baada ya mshtakiwa huyo kudaiwa kuwa mgonjwa.
Nipashe Agosti 20, 2009: Mshtaki wa Sendeka aishi nyumba ya Lowassa
Kesi inayomkabili Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, ya kumshambulia James Ole Millya, jana ilianza kusikilizwa huku mlalamikaji akielezwa kwamba anaishi nyumba ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Nipashe Agosti 21, 2009: Lowassa atajwa tena kesi ya Sendeka
Uhalali wa cheo cha mwenyekiti wa viongozi wa kimila wa kabila la Wamasai (Ilaigwanani) ambacho kinadaiwa ni cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kimehojiwa mahakamani katika kesi inayomkabili Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, ya kumshambulia James Ole Millya.
Nipashe Agosti 22, 2009: Wakili wa serikali kesi ya Sendeka akwama
Wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha ikikubali kupokea waraka uliozua utata wa maelezo ya shahidi wa pili, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Parseko Ole Kone, katika kesi ya kumshambulia James Ole Millya, inayomkabili Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, shahidi wa tatu katika kesi hiyo, Ngisayo Majuka, amesema hakuona mshtakiwa akimnyooshea bastola mshtakiwa.
Nipashe Novemba 24, 2009: Shahidi upande wa mashtaka ampa ahueni Sendeka
Mpelelezi katika kesi ya kutishia kuua inayomkabili Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, ambaye ni shahidi wa nane wa upande wa mashtaka, amekana mahakamani kuwapo kwa maelezo ya awali ya kutishia kuua kwa bastola katika jalada la kesi hiyo na kwamba hayo yalikuja baadaye.
Nipashe Machi 5, 2010: Hatma ya kesi ya Sendeka leo
Uamuzi wa kesi inayomkabili Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, ikiwa ana kesi ya kujibu au la, utatolewa leo.