Hii sio hadithi wala chitchat. Ni habari ya kweli. Ni ufunuo aliouona Yohana mnamo mwaka 95 BK, alipokuwa katika kisiwa cha Patmo. Mungu alimfunulia mambo mengi mazito, ya kutisha, yatakayotokea nyakati za kuelekea mwisho wa dunia.
Katika sura ya 12:12 ya kitabu alichoandika, Yohana alionyeshwa jinsi shetani alivyoishukia dunia na wanadamu wote akiwa amejaa ghadhabu.
Leo hii tunaona waziwazi matendo mabaya yanayoendelea katika dunia hii. Haya ni matokeo ya ghadhabu ya shetani. Ana ghadhabu kubwa kwa sababu anajua wazi kwamba muda wake umebaki mchache. Yeye aliishahukumiwa kutupwa katika moto wa milele.
Na anajua kuwa muda uliobaki kabla ya hukumu hiyo kutekelezwa umebaki mchache sana, na hana tumaini la kuokoka. Anachotaka ni ili asitupwe motoni peke yake, bali aingie humo na kundi kubwa la watu. Ndio maana anapambana kwa nguvu zote kuwavuta wengi katika upotevu.
Ghadhabu yake ameamua kuwaangushia wanadamu kwa kufanya yafuatayo: Anachochea uasi dhidi ya Mungu kwa njia mbalimbali. Anawachochea watu kuanzisha vita vinavyoangamiza kinababa, kinamama na watoto wasio na hatia.
Anawashawishi watu kujiingiza katika upotovu wa maadili kama vile ushoga. Amezitia giza akili za watu wengi na kuwafanya waone kuwa uzinzi ni mahusiano tu ya kawaida. Ndoa za watu anazivuruga na kuzisambaratisha, kisha anawashawishi walioachana waoe au kuolewa mara ya pili kinyume na Maandiko.
Vijana kwa wazee amewaingizia roho ya ulevi. Na wenye pesa amewajaza kiburi na majivuno. Uongo na hila anavifanya vionekane katikati ya watu kana kwamba ni vitu vya kawaida. Na pia anawachochea wasomi waione Injili kama kitu kisicho na maana.
Nimekufunulia siri hii leo. Chomoka kwa shetani. Njoo kwa Yesu sasa kabla mwisho haujafika. Mimi niliishachomoka kwake kitambo. Niko salama ndani ya Yesu. Nakuhurumia wewe ndugu yangu, ndio sababu kila mara nakutahadharisha kwamba kuna moto wa milele, hivyo usipuuze. Tubu sasa na umwamini Yesu kabla hujachelewa.