Hivi karibuni, kwa kuwa Benki Kuu ya Marekani imepandisha kiwango cha riba kwa mfululizo, kiwango cha ubadilishanaji wa dola za Kimarekani kimeongezeka kwa kiasi kikubwa. Hali hii imesababisha ongezeko la bei ya chakula na nishati duniani, ambavyo vinauzwa kwa dola za Kimarekani, na kuleta shinikizo kubwa la mfumuko wa bei katika nchi za Afrika. Idara ya Takwimu ya Kenya hivi majuzi ilitangaza kuwa mfumuko wa bei nchini Kenya ulifikia asilimia 8.5 mwezi Agosti, ambacho ni kiwango cha juu zaidi katika miaka mitano iliyopita.
Hali ya nchi nyingine za Afrika ni mbaya zaidi. Kiwango cha mfumuko wa bei nchini Nigeria, ambayo ni nchi ya kwanza kwa ukubwa a uchumi barani Afrika, kilifikia asilimia 19.64 mwezi Julai. Ripoti iliyotolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika inatabiri kuwa, wastani wa kiwango cha mfumuko wa bei cha nchi zote za Afrika kitafikia asilimia 13.5 mwaka huu.
Ili kukabiliana na shinikizo la juu la mfumuko wa bei, Benki Kuu za nchi nyingi za Afrika zimelazimika kuongeza kiwango cha riba. Matokeo ya moja kwa moja ya hatua hii ni kwamba, kasi ya ukuaji wa uchumi itapungua. Ripoti ya Benki ya Maendeleo ya Afrika inatabiri kwamba kasi ya ukuaji wa uchumi wa Afrika itapungua hadi asilimia 4.1 mwaka huu, na itakuwa chini sana ikilinganishwa na asilimia 6.9 ya mwaka jana.
Aidha, kiwango cha juu cha riba nchini Marekani pia kimeongeza kiwango cha ubadilishaji wa dola za Marekani, na kusababisha kushuka kwa thamani ya sarafu za nchi za Afrika, na hata baadi yao zinakabiliwa na hatari ya kushindwa kulipa madeni ya nje. Takwimu za Shirika la Fedha Duniani (IMF) zinaonyesha kuwa hivi sasa nchi 22 za Afrika zinakumbwa na msukosuko wa kulipa madeni.
Vitendo hivi vya kutowajibika vya Marekani vimepingwa vikali na nchi za Afrika. Mwanauchumi wa Kenya Ken Gichinga anaona kuwa nchi nyingi za Afrika zinaagiza chakula na mafuta ghafi kutoka nje, na kupanda kwa kiwango cha riba cha Marekani kumeongeza kiwango cha dola, ambayo imeongeza moja kwa moja gharama ya uagizaji wa bidhaa hizo.
Wakati huo huo, wawekezaji wengi wa kimataifa wameondoka barani Afrika kutokana na mvuto wa kiwango cha juu cha riba nchini Marekani, hali ambayo imeathiri maendeleo ya uchumi wa Afrika. Mtaalamu wa masuala ya uhusiano wa kimataifa wa Nigeria Charles Onunajju amesema shughuli za uchumi na biashara ya nje za Nigeria na nchi nyingine za Afrika zina uhusiano wa karibu na akiba ya dola za kimarekani, jambo ambalo linamaanisha kwamba Marekani inaweza kuhamisha shinikizo la mfumuko wa bei kwa nchi za Afrika kupitia sera ya kifedha.
Marekani inasema ni kiongozi wa uchumi wa dunia. Hata hivyo, inarekebisha sera yake ya kifedha kama inavyopenda bila kujali kwamba italeta changamoto kwa nchi nyingine haswa nchi za Afrika, kitendo ambacho si cha kuwajibika.