Ongezeko la mshahara kwa watumishi wa umma kwa hapa Zanzibar

Ongezeko la mshahara kwa watumishi wa umma kwa hapa Zanzibar

Abuhafsa

Member
Joined
Aug 11, 2022
Posts
5
Reaction score
3
TIRIGIVYOGO YA MSHAHARA

Napenda kuchukua fursa hii kueleza maoni na hisia zangu juu ya ongezeko la mshahara kwa watumishi wa umma kwa hapa Zanzibar.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia raisi wake mpendwa kwa nia njema ilitangaza kuongeza mishahara ya watumishi wa umma kuanzia mshahara wa mwezi wa Julai 2022. Ili ongezeko hilo la mshahara liweze kukidhi mahitaji muhimu ya maisha ya wananchi na kupunguza ukali wa maisha unaotokana na mfumko wa bei hapa Zanzibar na duniani kote.

Agizo la Mheshimiwa Raisi wa Zanzibar la kuongeza mshahara lililenga katika nyanja kuu mbili. Nazo ni;
1. Uzoefu wa kazi (experience).
2. Kiwango cha elimu.

Idara maalumu ya Utumishi wa Umma ilipewa mamlaka ya kusimamia jukumu hilo. Idara ilianza na uhakiki wa wafanyakazi wote kwa kuangalia uzoefu na elimu ya kila mtumishi wa umma na kumpangia mshahara wake kulingana na fomula walioiandaa.

Matokeo yake katika mwezi huo wa Julai 2022, mishahara ikatoka ikiwa kinyume kabisa na mategemeo ya watumishi. Walio wengi wamepewa mshahara si kwa kigezo kilichotajwa. Wako walioongezewa mshahara mkubwa wa kupindukia matarajio ya mshahara huo. Wako waliopunjika. Na wengine kupunguziwa hata haukufika katika mshahara wao wa miezi ya nyuma.

Hata hivyo idara ya Utumishi wa Umma ikawataka wafanyakazi watulie na wewe na subira kwani marekebisho ya mshahara huo yalikuwa na makosa mengi na kuahidi kurekebishwa katika mshahara wa August 2022. Na kila mfanyakazi akatakiwa ajaze fomu maalumu ya kuonesha uzoefu wake wa kazi na kiwango chake cha elimu.

Kufikia mwezi wa August mshahara ukatoka pamoja na kubainishwa fomula iliyotumika kugawa mshahara kwa kila mtumishi. Matokeo yake ndio ikazidisha zaidi sokomoko kwa wafanyakazi. Kwani suala la uzoefu wa kazi lilionekana ni mwiba mkali utakaopandisha watumishi madaraja na kupelekea kuwa na mshahara mkubwa. Hivyo suala hilo likaekewa kikomo (limit). Na kwa upande wa elimu, nalo liliangaliwa mpaka digirii ya kwanza tu.

Mvurugano wa mshahara huo umepelekea baadhi ya watumishi walio na umri mrefu kazini (uzoefu wa kazi mkubwa) kuwa na mshahara mdogo kulingana na wale walioajiriwa miaka ya karibuni (wenye uzoefu wa kazi mdogo). Kwa sababu kigezo cha uzoefu wa kazi kimezingatiwa kutokea mwaka wa cheti cha mwisho cha mfanyakazi bila ya kuangalia tarehe/mwaka alioanza kuajiriwa. Na hii sio haki hata kidogo. Na inasababisha watumishi kutoengeza elimu kwa kuhofia kupunguziwa mshahara wao.

Tirigivyogo hii imetokea kwa makusudi. Kwani ukweli usiopingika kama mshahara utazingatia kigezo cha elimu basi watakaonufaika kupitia kigezo hicho ni wachache katika sekta zote kwa ujumla. Ama kwa upande wa sekta ya elimu kitawanufaisha walio wengi hasa walimu. Kwani walimu walio wengi wameanza ajira kwa ngazi ya cheti/FIV (certificate) na kujiendeleza kielimu hadi kufikia sasa walimu wengi wamemaliza shahada ya kwanza (degree) na wengine shahada ya pili (master).

Tunawaomba idara ya Utumishi wa Umma ifanyie marekebisho fomula ya kugawa madaraja ya mshahara kwa kuzingatia kauli ya Raisi juu ya kigezo cha uzoefu wa kazi na elimu.
Tunaposema uzoefu wa kazi tunamaaisha ni tokea tarehe ya kuanza kuajiriwa hadi hivi sasa.
Aidha, tukisema elimu basi iangaliwe tokea alipoajiriwa akiwa na elimu gani hadi sasa ana elimu ya kiwango gani. Iwe degree, Master, Au PhD.
 
Hiyo formula ilotumika kupandisha mishahara ni ipi naona wenzenu wa vikosi vya smz wanalalamika hata hiyo elimu haijaangaliwa kwa ufupi bado changamoto ni nyingi
 
Hiyo formula ilotumika kupandisha mishahara ni ipi naona wenzenu wa vikosi vya smz wanalalamika hata hiyo elimu haijaangaliwa kwa ufupi bado changamoto ni nyingi
Fomula inayotumika ni nyang'anti kwani uzoefu wa kazi mwisho miaka 12. Elimu yako ya mwisho ndio wanaanza kukuhesabia miaka hapo na kupelekea walomaliza masomo miaka ya karibuni hata kama wana uzoefu wa miaka mingi haizingatiwi. Na hao vikosi wanalalamika kwa sababu fomula inaazia elimu ya FIV na wao wengi wameajiriwa bila ya FIV
 
Fomula inayotumika ni nyang'anti kwani uzoefu wa kazi mwisho miaka 12. Elimu yako ya mwisho ndio wanaanza kukuhesabia miaka hapo na kupelekea walomaliza masomo miaka ya karibuni hata kama wana uzoefu wa miaka mingi haizingatiwi. Na hao vikosi wanalalamika kwa sababu fomula inaazia elimu ya FIV na wao wengi wameajiriwa bila ya FIV
Mh. kuna watu mi nawafahamu wana digrii lakini mishahara yao haijarekebishwa labda hao vikosi walitumia formula nyingine
 
Back
Top Bottom