Operesheni ThunderBolt: Mkakati wa Kuokoa Mateka wa Israel Entebe - Uganda

Operesheni ThunderBolt: Mkakati wa Kuokoa Mateka wa Israel Entebe - Uganda

jerrytz

JF-Expert Member
Joined
Oct 10, 2012
Posts
5,975
Reaction score
4,266
Ni Juni 27, mwaka 1976 majira ya saa 12.30 jioni; ndege ya Airbus A300 inayomilikiwa na shirika la ndege la Ufaransa (Air France) ndege namba AF139 ilipaa kutoka uwanja ndege wa Athens. Ndege hii ilitua katika uwanja Athens ikiwa safarini kutoka Tel Aviv Israel kuelekea Paris Ufaransa.

Mpaka kufikia muda huo safari ilikuwa nzuri kwa abiria. Lakini baada ya muda hali hiyo ya safari ya utulivu ilibadilika kwa sababu miongoni mwa abiria 248 kwenye ndege hiyo kulikuwa na abiria 4 waliopanda ndege katika uwanja wa ndege wa Athens waliokuwa na mipango ya kuiteka ndege hiyo.

Hii ni simulizi ya kutekwa kwa ndege ya Ufaransa iliyokuwa na raia wengi wa Israel, na hatimaye ndege hiyo kupelekwa katika uwanja wa ndege wa Entebe nchini Uganda.

Ndege ikiwa inajiweka sawa mara baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege wa Paris, huku abiria wakiwa wameketi vitini, ghafla kijana wa kiume na kijana wa kike wakasimama kutoka katika viti vyao huku wameshika bunduki mikononi, majina yao ni Wilfred Bose na Brigita Koeman wote wakiwa ni raia wa Ujerumani Magharibi ambao walikuwa wanachama wa kundi la kigaidi lililokuwa likijulikana kama Red Army. Huku abiria wakiwa bado wanashangaa watekaji wengine wawili wakainuka eneo la nyuma ya ndege, nao pia wakiwa na silaha ila hawa walikuwa wanachama wa Chama cha Ukombozi cha Palestina (PLO)External Operation hawa walikuja kujulikana baadaye kama Jayel al-Arja na Fayez Abdul-Rahim al-Jaber. Abiria wakakosa utulivu, watekaji wakawamrisha wakae kimya na kutulia kwenye viti vyao.

Baada ya kusikia kelele, co-pilot akatoka kwenye chumba cha rubani (cockpit) na kuja upande wa abiria ili kujua kilichokuwa kinaendela. Kitendo hiki cha kufungua mlango kikampa nafasi Wilfred Bose kuingia chumba cha rubani na kumueleza rubani kuwa awe mtulivu na afuate maelekezo yake kwani, yeye mwenyewe Bose ni rubani hivyo, asijaribu kufanya chochote maana atahatarisha usalama wake. Mpaka kufikia hapo, Wilfred Bose akasema kwa muda huo ndege namba AF 139 imetekwa na ipo chini yake.

Akiwa amenyoshea bastola rubani, akamwamuru kuwa ndege hiyo sasa badala ya kuelekea Paris, inatakiwa kueleka Bengazi, nchini Libya, iliyokuwa chini ya Kanali Muamar Gaddaf.

Masaa mawili baadaye ndege namba AF 139 ikatua katika uwanja wa ndege wa Benghazi, Libya. Walipofika hapo abiria hawakushushwa kwenye ndege badala yake walibaki kwenye ndege, ndege iliwekwa mafuta na kulikuwa na mazingumzo ya upatanishi katika ya serikali ya Israel, Libya na Watekaji wa ndege.

Abiria mmoja, mwanamke wa makamo aliyekuwa mjamzito akashushwa hapo maana ilionekana kuwa ana dalili zote za kuzaa ama mimba kuharibika.

Baada ya saa saba, ndege ikapaa tena kutoka uwanja wa Bengazi, hii ikawa safari ndefu na yenye kuchosha kwa abiria, wachache wakagundua kuwa uelekeo wa ndege ni upande wa kusini. Kwahiyo ikawa wazi kwamba wanaelekea katikakati ya bara la Afrika.

Wakati wote wa safari, watekaji waliendelea kutoa vitisho kwa abiria kuwa inawapasa kuwa watulivu na wasijaribu kufanya chochote maana walikuwa wanamaanisha wanachokisema.

Wilfred Bose na Brigita Koeman walikuwa wakijitambusha kwa abiria kama Mr. Hijacker na Mrs Hijacker na kueleza kuwa utekeji huo wa ndege ni mpango mkubwa walioupa jina la Haifa One.

Baada ya zaidi ya masaa 20 tangu utekaji utokee hatimaye ndege ilitua katika uwanja wa ndege wa Entebe, nchini Uganda saa 9.15 mchana.

Kitu cha kwanza ambacho abiria waliona ni ziwa Victoria na baadaye kuona jengo la uwanja wa ndege wa lililokuwa limeandikwa Entebe Airport, ndipo wakajua kuwa wapo Uganda.

Wakiwa wanashuka kwenye ndege wakaona askari wamejipanga pembeni, hii iliwapa faraja kuwa inawezekana maafikiano yamefikiwa na watekaji sasa wapo tayari kuwaachia huru. Lakini hawakuwa sahihi, kwa maana wapo Uganda iliyokuwa chini ya Idd Amini. Na kiukweli shida yao ndio kwanza ilikuwa imeanza.

Wakiwa chini ya ulinzi wa wanajeshi wa Uganda abiria wakaongozwa kwenda kwenye jengo la zamani la abiria ambalo lilikuwa halitumiki kwa wakati huo.

Kiongozi wa watekaji, Wilfred Bose akapatiwa simu, na kwa mara ya kwanza tangu utekaji wa ndege namba AF 139 ufanyike dunia ikajua kile ambacho watekaji wanataka.

Mahitaji yaliyotajwa na Bose ili kuachia ndege na abiria wakiwa salama ni
Dola milioni 5 cash
Kuachiwa huru kwa Wafungwa Wa kipalestina wapatao 53 waliokuwa wakishikiliwa katika magereza nchini Israel na nchi nyingine za Magharibi.

Huku akisisitiza kuwa kama masharti yao hayatekelezwa ndani ya siku tatu basi wataanza kuua abiria mmoja baada ya mwingine tarehe 1 Julai, abiria mmoja kila baada ya saa moja.

Huko Jijini Tel Aviv, Israel Waziri Mkuu Yitzak Rabin aliitisha kikao cha dharura cha Baraza la Mawaziri na Baraza la Usalama.

Lakini pia aliwasiliana na Rais wa Marekani Gerald Ford, simu zilipigwa Ufaransa, Palestina na Misri kwa Rais Anwar Sadat na viongozi kadhaa wa nchi za Kiarabu.

Ikakubaliwa kwamba rais wa Misri atumie ushawishi wake kwa hawa Watekaji, lakini ikaoneka kuwa watekaji wa ndege hawakuonyesha kabisa kumkubali Saadat. Hivyo jukumu la upatanishi likaenda kwa kiongozi wa PLO Yasser Arafat.

Na sababu kubwa kumpa jukumu la upatanishi Yasser Arafat ni kuwa miongoni mwa watekaji kulikuwa na Wapalestina, lakini pia Yasser Arafat alikuwa na ukaribu na rais wa Uganda, Field Marshal Idd Amini Dada, kwasaba aliwahi kuwa msimamizi wa ndoa mojawapo ya Idd Amin.

Arafat akatuma kikosi maalumu kwenda Uganda kwa ajili ya kunusuru maisha ya abiria wa ndege namba AF 139.

Wajumbe walipofika watekaji wakashikilia msimamo wao kuwa ikifika tarehe 1 Julai, wataanza kuua abiria mmoja baada ya mwingine kila baada ya saa moja .

Jambo moja zuri ni kuwa walau Yaaser Arafat aliweza kushawishi watakaji kuongeza muda wa kutekeleza maazimio yao.
Israel ikaomba walau wapewe siku saba ili waone namna ya kutelekeza matakwa ya watekaji, watekaji wakatoa siku sita tu matakwa yao yote yawe yametelekezwa.
Siku sita zilikuwa zinaishia tarehe 4 Julai, hapa ndipo Idd Amini akaingia kama msuluhishi katika suala zima la utekajwi wa ndege namba AF 239.

Watu wengi wanajiuliza je Idd Amini alijua huu mpango wa ndege kutekwa? Kwa nini aliruhusu watekaji kutumia uwanja wa ndge wa Entebe? Inawezekana aliona ni nafasi tu ya kujipa umaarufu duniani.

Kwa miaka hiyo, Idd Amin alikuwa anatamba Afrika na hata siasa za dunia kwa misimamo yake na mambo kadhaa. Alikuwa amepindua serikali ya Milton Obote, alikuwa ameshafukuza Wafanyabiashara wenye asili ya Asia haswa Wahindi, alikuwa ameshafanya mauaji mengi hata kuua viongozi kadhaa wa kanisa Katoliki.

Katika siku nne za kwanza baada ya ndege kutua Entebe, Rais Idd amini alikuwa akienda uwajani kila siku na msafara wake, huku akizungumza na waandishi wa habariu wa mashirika ya kimataifa yaliyokuwa yakiripoti habari moja kwa moja kutokea uwanja wa ndege wa Entebe. Mara kadhaa alikuwa akisema kuwa ni yeye ambaye anaweza kutoa suluhisho kwa kinachoendelea hapo Entebe.
Lakini kiukweli hakuna ambacho angefanya katika kuleta ufumbuzi,alijiweka kama msuluhishi lakini hakuwa anafanya chochote kutafuta sululu.
Hakuna ajuaye kama hata alihusika kwa tukio lilitokea tarehe 30 Juni, ambapo watekaji waliruhusu kuachiwa huru kwa baadhi ya abiria wa ndege AF 139. Kundi la abiria waliochiwa walikuwa wazee, wagonjwa na watoto, jumla ya abiria 148 wakaachiwa katika makundi mawili.

Abiria waliochiwa walisafirishwa kwa ndege maalum kwenda Paris Ufaransa, lakini wote walioachiwa ni wale tu ambao hawakuwa raia wa Israel. Abiria wote waliokuwa na passport za Israel, hawakuachwa huru.

Katika hali isiyotarajiwa marubani na wahudumu wa ndege raia wa Kifaransa wapato 12 wakaamua kubaki na mateka wa Kiisrael.

Raia wa Israel ambaye alikuwa na asili ya Uingereza mwenye miaka 74 aliugua, huyu akapelekwa hospitali ya Mulago.

Huko nchini Israel, maafisa wa jeshi walikuwa kwenye vikao kupanga mipango mbalimbali katika kunusuru maisha ya raia wake ambao kwa sasa walikuwa chini ya watekaji katika uwanja wa ndege wa Entebe, Uganda.
Ikaamuliwa kwamba, operesheni maalum ifanyike maana serikali ya Israel haina sera ya kutii maagizo ya watekaji. Katika operesheni hii maalumu, maisha wa raia wa Israel ndio lengo la kwanza, hivyo operesheni yoyote itakayofanyika lazima kwanza iwe na lengo la kuokoa mateka na kuhakikisha kuwa wanabaki hai.
Miaka minne tu iliyopita wanajeshi na askari wa Kijerumani walijaribu kuokoa maisha wa wanamichezo wa Israel waliotekwa na watekaji katika michezo ya Olympic katika jiji la Munich lakini hawakufanikiwa, kwani magaidi waliwaua mateka wote.

Mpango wa awali ulikuwa kuleta kikosi maalum cha Makomandoo kisha washuke kwa parachute katika Ziwa Victoria, lakini kukawa na matatizo mawili, upande wa Entebe unapakana na Ziwa Victoria kulikuwa na mamba na pili baada kufanikiwa kuwaokoa hao mateka je hawa makomandoo watawapeleka wapi hao mateka( kumbuka wao wameshuka kwa miavuli).

Taifa la Israel lilikuwa halimuamini Rais Idd Amini maana alikataa kushughulika na watekaji ili wawaachie raia wa Israel.

Uwanja wa Uganda, na uwanjani kulikuwa na kikosi cha jeshi la Uganda hivyo kama kweli Idd Amini angekuwa mtu wa kutumainika basi angeweza kuwazidi nguvu watekaji na hatimaye raia wa israel wangekuwa huru.

Hivyo mpango wa kutuma makomandoo watakaoshushwa katika Ziwa Victoria ukaonekana kuwa haufai. Mpango sio tu kuwaweka huru mateka 106 lakini lazima pia watolewe nje ya Uganda.

Military Strategists. Wapangaji wa operesheni za kijeshi wakaja na mpango mwingine wa kutumia ndege kubwa nne za Kijeshi zinazojulikana Military Transport - Lockheed C-130 Hercules ambazo zina uwezo wa kubeba watu na vifaa vingine kama magari ya kivita.

Lengo likawa kushusha kikosi kidogo cha makomandoo katika uwanja wa ndege wa Entebe.

Lakini hapa napo kukawa na tatizo, kupeleka na kuingia ndege ya kivita nchini Uganda haitakuwa rahisi maana inawabidi kupita kwenye radar za nchi ya Saudi Arabia au Misri na hatimaye Sudani na kisha Ethiopia. Hivyo itawapasa kuruka chini kuruka kwa uangalifu, usiku katika spidi ya maili 400 kwa saa kwa umbali wa maili 2,189 sawa na Kilometre 3522 kutoka Israel mpaka Uganda. Swali likaja kwa safari ya umbali huu ndege haiwezi ikarudi bila kuongeza mafuta, hivyo ikabidi Israel itafute taifa rafiki katika nchi za Afrika Mashariki mahali ambapo ndege zake zitatua ili kuogeza mafuta katika safari ya kurudi. Baada ya majadiliano ya siri,Kenya ikaipa ruhusa nchi ya Israel kutumia uwanja wake wa ndege kwa ajili ya kuongeza mafuta.

Wakati huo wale abiria 148 walikuwa wakihojiwa na maafisa wa Israel nchi Ufaransa, mmoja kati ya mateka waliochwa huru aliwahi kuwa mwanajeshi hivyo alikuwa na kumbukumbu nzuri hivyo aliweza kuwa msaada mkubwa kwa maafisa wa shirika la Ujasus la Israeli (MOSAD) kuhusiana na watekaji, silaha zao na mambo yote muhimu.

Wakati huo pia taasisi ya Ujasusi ya Israel ikamtumia rubani mmoja kurusha ndege yake ndogo karibu na uwanja wa Entebe na kuchukua picha.

Lakini pia kulikuwa na Engineer wa Kiisrael ambaye alishiriki katika ujenzi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Entebe miaka 1960, huyu akawapatia michoro ya uwanja (blue print)

Tarehe 3 Julai, majira saa 12.30 jioni operesheni Thunderbolt ikapitishwa kwa utekelezaji. Baada Saa tano baadaye ndege nne za Israel zikawa zinawasili Ziwa Victoria, zikashuka katika uwanja wa Entebe.

Katika operesheni hii, Jeshi la Israel lilipanga kuwahadaa/kuwadanganya walinzi wa uwanja wa Entebe, katika ndege moja wapo ikashuka gari nyeusi (Black Cadillac Limosine) inayofanana na gari aliyokuwa akitumia Rais Idd AMINI, nyuma yake kukawa na Landlover mbili zikiwa na bendera ya Uganda kama msafara wa rais.

Na kwa wakati huo Idd Amini alikuwa amesafiri kwenda kuhudhuria mkutano huko Mauritius. Na kwakuwa hakuwa na kawaida ya kutoa taarifa anapokuwa anarudi, jeshi la israel likaona litumie hiyo nafasi.

Katika gari ya kwanza alikuwemo Luteni Kanari Yonatan Netanyahu, kiongozi wa operesheni Thunderbolt ambaye pia ni kaka wa Benjamini Netanyahu aliyekuja kuwa Waziri Mkuu wa Israel kwa vipindi kadhaa, magari mengine yalikuwa na makomandoo wengine wa Israel.
Walipokaribia check point, askari wawili wa Uganda wakawasimamisha, bila kuchelewa askari hawa wakapigwa risasi. Kufikia hapo wanajeshi na walinzi wengine wa Uganda wakashtuka kuwa kuna kitu hakipo sawa.

Mapambano yakaanza kati ya makomandoo wa Israel na wanajeshi wa Uganda.
Wakiwa katika uwiano wa Komandoo mmoja kwa wanajeshi 10 wa Uganda, mapambano yakaendelea huku makomandoo wakielekea kwenye jengo ambalo walipo mateka wa Kiisraeli na watumishi 12 wa ndege namba AF 239.
Baada ya mateka kusikia milio ya risasi , wakaingiwa na hofu lakini ghafla wakasikia sauti kwa lugha ya kiyahudi tulieni hii ni misheni ya kuwaokoa, kijana mmoja baada ya kusikia hiyo sauti akasimama kwa furaha; akapigwa risasi kutoka upande wa watekaji. Huyu mmoja kati ya watu watatu waliokufa katika opereshi Thunderbolt.

Mtekaji mmoja baada ya kuona mambo yameshaharibika akaamua kufyatua bomu la kurusha kwa mkono(hand grenade) likalipuka lakini halikuleta madhara kwa mateka.

Wakati huu ndipo kiongozi wa watekaji Wilfred Bose akatokea, huku akiwasisitiza mateka kukaa chini, huyu naye akapigwa risasi na komandoo wa Israel.

Mateka waliokombolewa wakapewa maagizo ya kushikana mkono huku wakitolewa katika eneo walilokuwemo huku wakiongozwa kuelekea kwenye ndege.
Wakati yote haya yanatokea, Kanari Netanyau akajeruhiwa vibaya kwa risasi na mwanajeshi wa Uganda.
Akabebwa na gari ya kijeshi huku makomandoo wengine wakiteketeza ndege 11 za kivita za Uganda zilizokuwa uwanjani hapo. Ilikuwa muhimu kuteketeza ndege hizi maana inaondoa kabisa uwezo wa jeshi la anga la uganda kuwakimbiza ama kuwafutilia baada ya operesheni kukamilika.

Muda mchache baadaye ndege za kivita za Israel, zipo hewani tena katika safari ya kurudi Israel. Opereshi nzima ya thunderbolt ilichukua dakika 23. Operesheni hii ilikamilika muda mchache kabla ya deadline ya watekaji ya Julai 4.
Ndege zilipoingia katika anga la Kenya, rubani mmoja akawasha radio ya masafa marefu na kuripoti kwa kamati maalumu ya Ulinzi na usalama ya Israel kuwa Opereshi Thunderbolt imekamilika kwa mafanikio makubwa.
Katika siku zilizofuata baadhi ya mataifa yakiongozwa na Libya yakailaumu Israel kuwa operesheni ya kijeshi ndani ya Uganda imevunja sheria za kimataifa. Hata umoja wa afrika uliilaumu israel pia kwa operesheni yake,lakini mataifa ya magharibi yakaipongeza israel kwa operesheni Thunderbolt.


Idd Amin alichukizwa sana na tukio hili; maana alipoteza wanajeshi 40 na ndege za kivita 11 katika jeshi lake la anga.
Aliporejea Uganda na baada ya uchunguzi mdogo ikagundulika kwamba kiongozi wa kijeshi wa kikosi alikuwa hoteli ya Victoria akinywa bia wakati makomandoo wa Israel walipovamia uwanja wa entebe.
Wamajeshi 14 wa Uganda waliokuwa zamu Entebe pamoja na mkuu wa kikosi wakapewa shutuma za kushirikiana na Jeshi la Israel.
Wakapelekwa kambini na hatimaye wakapigwa risasi na kuuwawa.

Na katika hospital ya Mulago, kule alipopelekwa mateka mgonjwa; katika hali isiyo ya kawaida mgonjwa alipigwa mpaka akafariki. Daktari aliyekuwa akimhudumia pia naye aliuwawa, mwili wa daktari na mateka ikakutwa pembezoni mwa shamba la miwa maili 21 nje ya jiji la Kampala.

Iddi Amini hakuishia hapo, akafukuza wakenya waliokuwa wanaishi Uganda. Kenya nayo ikafunga mpaka wake na kuzuia Uganda kutumia bandari ya Mombasa.


Simulizi ijayo; itakuwa Historia ya Mapinduzi ya Uganda mpaka Vita ya Kagera​
 
Haya jihadists waje wapinge kwamba hilo zoezi halikufanyika.
 
Back
Top Bottom