Padre Charles Kitima ni katibu wa baraza la maaskofu katoliki Tanzania
(TEC) ambaye alipata daraja takatifu ya upadre takribani miaka 27 iliyopita ambapo mwaka 2022 aliadhimisha Jubilei ya miaka 25 ya Upadre katika Parokia ya Kristu Mfalme Siuyu Jimbo Katoliki Singida mahali alipozaliwa.
Padre Kitima amekuwa ni moja kati ya viongozi wa dini ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu ya kiraia ili kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu kwenye michakato ya kidemokrasia.
Mnamo usiku wa tarehe 30, Aprili 2025 iliripotiwa kuwa watu Wasiojulikana walimvamia Padre Dkt. Charles Kitima majira ya usiku na kuanza kumshambulia wakati akiwa kwenye makazi yaliyopo Ofisi za Baraza la Maaskofu (TEC) Kurasini, Dar Es salaam.
Aidha tarehe 04 mwezi Mei 2025 makamu wa rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC Askofu Eusebius Nzigilwa alieleza hali ya padre huyo,
akisema anaendelea na matibabu na hali yake inaimarika huku akiwataka watanzania kuendelea kuombea ili mwenyezi Mungu amuwezeshe kupona haraka.
Madai
Kumekuwapo na taarifa inayodaiwa kuchapishwa na The Chanzo pamoja na Mwanahalisi kuwa 'Father Kitima azuia watumishi wa serikali kumtembelea hospitali'
Uhalisia wa machapisho hayo
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck kwa kutumia maneno muhimu (Key Word Search) ulibaini kuwa machapisho hayo si ya kweli ni ya kutengenezwa kwani hayakuchapishwa katika kurasa rasmi za mitandao ya kijamii, za
Mwanahalisi na
The Chanzo.
Aidha yamebainika mapungufu kadhaa katika machapisho hayo ambayo yanayatofautisha na machapisho rasmi ya vyombo hivyo. Matumizi ya mwandiko (fonts) ambao unatofautiana na ule unaotumiwa katika machapisho rasmi ya vyombo hivyo ni sehemu ya mapungufu hayo.