Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,809
- 15,421
Josie alinusurika.................
Josie alivyo sasa...
Josie akiwa na baba yake
Familia ikiwa pamoja, Lin, Megan, Russell na Josie....Megan aliuawa na mama yao Lin naye aliuawa
Josie akiwa na baba yake
Josie akiwa na baba yake
Ilikuwa ni majira ya saa kumi za jioni mnamo July 1996, katika mji wa Kent kusini mwa Uingereza mama mmoja aliyejulikana kwa jina la Lin Russell alikuwa ametoka shuleni kuwachukua mabinti zake wawili, Megan aliyekuwa na umri wa miaka 6, na Josie aliyekuwa na miaka 9. Wakiwa wameongozana na mbwa wao aitwae Lucy, walitembea kwa mguu kutoka katika shule hiyo ya Goodneston kuelekea nyumbani kwao. Walikuwa wanaishi katika eneo la Nonington, umbali wa kama kilomita moja kutoka hapo shuleni. Lakini kwa bahati mbaya hawakutokea nyumbani.
Majira ya saa 1:15 usiku Dk. Shaun Russell 47, mwalimu wa baioloji katika chuo kikuu cha Kent, alirudi nyumbani lakini jambo la kushangaza, hakuikuta familia yake hapo nyumbani. Hali hiyo haikumstua sana, hivyo aliamua kujipumzisha sebuleni kwake akijua kwamba muda wowote mkewe na watoto watarejea kutoka katika matembezi ya jioni. Baada ya saa moja Dk. Russell alishangazwa na familia yake kutotokea na hivyo kuanza kujenga wasiwasi.
Aliwapigia marafiki zao kadhaa, lakini hakuna hata mmoja aliyedai kuiona familia yake. Ilibidi awajulishe majirani zake na haraka sana kwa kushirikiana na majirani hao walianza kuitafuta familia yake katika maeneo ya hapo karibu na nyumbani kwao wakianzia shuleni, lakini hawakuweza kuwapata. Hatimaye ilipofika majira ya saa 4:45, Dk. Russell aliamua kuwajulisha Polisi kwamba familia yake imetoweka katika mazingira ya kutatanisha. Majira ya saa 7:45 usiku, Polisi hao walifanikiwa kupata miili ya familia ya Dk. Russell ikiwa imelala njiani umbali wa nusu kilomita kutoka hapo nyumbani kwake. Lin na Megan Russell walikuwa wamekufa, akiwemo mbwa wao aitwae Lucy, Josia alikuwa bado hajakufa, lakini alikuwa amepoteza fahamu. Wote walikuwa wamepigwa na nyundo kichwani.
Mtoto Josie Russell alikimbizwa hospitalini ambapo alifanyiwa upasuaji wa dharura. Ilibidi sehemu ya ubongo wake iondolewe ili kuokoa maisha yake. Hata hivyo hali yake iliendelea kuwa mbaya na kulikuwa na matumaini finyu sana ya mtoto Josie kupona. Dr. Russell alifika pale hospitalini akiwa amechanganyikiwa. Kwa kuwa hali ya mwanaye ilionekana kuwa mbaya na isiyo na chembe ya matumaini ya kupona, madaktari bingwa waliokuwa wakimtibu binti yake walimuomba awaruhusu wazime mashine iliyokuwa ikisaidia mapigo ya moyo na kuridhia binti yake kufa.
Ditective Chief inspector David Stevens aliyekuwepo pale hospitalini muda wote akifuatilia hali ya binti huyo pia alikuwa na matumaini finyu ya binti huyo kupona na kurudi katika hali yake a kawaida.
"Itakuwa ni vigumu Josie kukumbuka jambo lolote kuhusu tukio zima la kushambuliwa na muuaji hata kama akipona." Alisema askari huyo wa upelelezi akiongea na waandishi wa habari. "Mpaka sasa inabidi tutafute mashahidi wengine watakaoweza kutusaidia kumpata muuaji. Ni lazima kuna mtu anajua ni nani alihusika na mauaji haya ya kutisha, kwani tusipofanya juhudi za kumkamata mapema anaweza kushambulia tena mahali pengine na kuuwa… hivyo ni lazima ufanyike msako mkali ili mtuhumiwa atiwe mbaroni kabla ya kutekeleza mauaji mengine. Nisingependa wananchi waendelee kuwa na hofu juu ya maisha yao." Aliendelea kusema.
"Hii ni jamii adilifu iliyokuwa ikiishi kwa amani kabla ya mauaji haya, ni pale muuaji atakapopatikana ingawa sijui ni kwa namna gani, ndipo nitakaposema watu sasa wako salama. Kutokana na tukio hili, kuanzia sasa watoto wasiruhusiwe kuwa nje peke yao na si vyema wanawake kutoka nje ya nyumba zao wakiwa peke yao. Ukweli ni kwamba hili ni tukio la kutisha ambalo sijawahi kulishuhudia katika maisha yangu. Ni mwendawazimu pekee anayeweza kufanya hivyo."
Mchoro wa picha ya muuaji
Ili kumpata muuaji, ilibidi Detective Chief Inspector Stevens aunde timu ya wapelelezi 30 ambayo aliipa kazi maalum ya kufanya upelelezi makini juu ya mauaji hayo. Kwa kuanzia askari hao wa upelelezi walifankiwa kupata silaha iliyotumika katika mauaji hayo ambayo ilikuwa ni nyundo.
Askari hao walianza upelelezi wao kwa kuhoji nyumba kwa nyumba, walitengeneza mchoro unaionyesha familia hiyo ikitembea kutoka shuleni kurudi nyumbani, pia walichora picha ya mtu aliyetajwa na mashahidi mbalimbali waliomuona katika eneo hilo muda mfupi kabla ya mauaji kutokana na muonekano wake kuwa ni wa kutiliwa mashaka. Michoro yote hiyo ilionyeshwa katika televisheni ikiwa ni juhudi za askari hao wa upelelezi kumpata muuaji.
Mpaka kufikia hapo, walichokuwa wakihitaji askari hao wa upelelezi ni maelezo kutoka kwa mtu aliyeshuhudia tukio hilo la mauaji. Na shahidi muhimu na ambaye angeweza kuwategulia kitendawili hicho alikuwa bado amelazwa hospitalini hali yake ikiwa mbaya sana. Binti huyo alionekana dhahiri kupigania maisha yake, kwani baada ya wiki tatu, aliwashangaza madakatari ambao walishakata tamaa, kutokana na afya yake kuonekana kuimarika kwa kasi ya ajabu. Haraka sana alimudu kunyanyuka kitandani na kuanza kutembea pale wodini. Alimudu pia kuongea, ingawa matamshi yake yalikuwa kama ya mtoto wa miaka miwili anayejifunza kuongea. Hata hivyo baba yake hakupoteza matumaini. "Ingawa ni vigumu kwangu kujua itachukua muda gani Josie kumudu kuongea na kuwasiliana kama zamani, lakini anaonyesha dalili zote za kukusanya kumbukumbu ambapo siku moja ataweza kuwasaidia askari wa upelelezi kumkamata muaji aliyewaua mama yake na dada yake." Alisema Dr. Russell.
Detective Chief Inspector Stevens akizungumzia kuimarika kwa afya ya Mtoto Josie alisema kwamba, amefurahishwa na kuimarika kwa afya ya binti huyo, lakini alieleza wasiwasi wake kuhusiana na uwezekano mdogo wa binti huyo kukumbuka tukio zima. "Kwa akili ya kawaida huwezi kutegemea binti aliyejeruhiwa kwa kiwango kile kupona na kumudu kukumbuka tukio zima kwa usahihi. Tukio hilo litamtesa kwa maisha yake yote."
Mara baada ya Josie kuruhusiwa, baba yake Dr. Shaun Russell alihama kutoka katika eneo hilo na kuhamia Kaskazini mwa Wales katika eneo ambalo halikutajwa kwa usalama wake na wa mtoto Josie. Kwa muda wa mwaka mmoja Josie alikuwa anahudhuria katika hospitali kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kuongea (Speech Therapy) na taratibu alianza kumudu kuongea na pia kurudisha kumbukumbu. Pamoja na kuwahoji watu zaidi ya 9,000, na kuchukua maelezo kutoka kwa watu mbalimbali wapatao 1,000 nchini humo na nje ya nchi hiyo, kama Ufaransa, Ubelgiji na Marekani, lakini Detective Chief Inspector na timu yake walionekana kukwama kumpata muuaji.
Hata hivyo Ditective Stevens alionekana kuwa mtulivu na aliendelea kuvuta subira huku akifuatilia maendeleo ya binti Josie. Hali ya mtoto Josie iliendelea kuimarika na Detective Stevens aliona kwamba huo ni wakati muafaka kwa Josie kusaidia kumpata muuaji wa mama yake na dada yake. Josie alikubali kuongea na askari huyo wa upelelezi na mnamo July 9, 1997 ikiwa umeshapita mwaka mmoja tangu tukio hilo litokee, Polisi walitangaza rasmi kwamba Josie amekubali kutoa maelezo ya kina kuhusiana na tukio hilo.
Katika mkutano wake na vyombo vya habari Ditective Chief Inspector Stevens alisema kwamba, maeleza waliyoyapata kutoka kwa Josie yatasaidia sana kumpata muuaji pasi na shaka yoyote. Katika kipindi chote cha mahojiani yaliyofanywa na Polisi maalum wa upelelezi waliofunzwa kufanya mahojiano na watu wenye hali kama ya Josie waliotajwa kwa majina ya Pauline Smith na Ed Tingley. Josie alionekana kuwa na kumbukumbu sahihi juu ya tukio hilo.
Detective Stevens alitoa maelezo hayo kutoka kwa Josie kama ifuatavyo:
"Josie na familia yake walikuwa wanarudi nyumbani kutoka shuleni, ambapo waliona gari likija nyuma yao na kuwapita. Waliendelea kutembea, lakini walipokuwa wanakaribia kukata kona, waliliona lile gari likiwa limesimama mbele yao. Josie alikumbuka rangi ya gari kuwa lilikuwa ni jekundu. Wakati walipolikaribia hilo gari, walimuona mtu aliyekuwa kwenye gari hilo akichukua nyundo kutoka kwenye kishubaka cha kuhifadhia vifurushi ndani ya gari. Aliwafuata na kumuamuru mama yao: "Nipe pesa haraka" mama yao alimjibu: "Nitakwenda nyumbani kukuchukulia, kwani siishi mbali kutoka hapa." Mtu huyo alianza kuwashambulia, na mama yao alianza kupika kelele: "Tafadhali usitudhuru….." Mama yake alimamuru Jose akimbie na Josie alikimbilia katika nyumba moja ambayo kwa bahati mbaya ilikuwa haikaliwi na mtu kwa wakati ule. Yule muuaji alimkimbiza na kumkamata kisha kumrudisha pale alipo mama yake na dada yake. Yule muuaji aliwafunga kwa kipande cha kamba alichokipasua kutoka kwenye taulo. Muuaji huyo alidiriki hata kumuuliza Josie kama ile kamba aliyowafunga imekaza sawasawa. Alianza kupekua mkoba waliobebea vyakula vyao vya shule ambapo kiukweli haukuwa na kitu chochote. Muuaji yule alianza kumshambulia mama yao. Yule muuaji hakuongea tena bali alianza kuwashambulia lakini hakumbuki kuona dada yake akishambuliwa wala mbwa wao, anachokumbuka ni kuona mama yao akishambuliwa kikatili na muuaji huyo. Alimuelezea muuaji kuwa anafanana na picha iliyowahi kuchorwa na Polisi ambayo ilichorwa baada ya mauaji hayo kwa msaada wa mashahidi waliojitokeza na kudai kumuona mtu katika eneo hilo yalipotokea mauaji mwenye muonekanao wa kutia shaka muda mfupi kabla ya mauaji hayo." Alisema Detective Stevens.
"Alichotueleza Josie, kinatisha na kusikitisha, na maelezo yake ni msaada mkubwa sana kwetu utakaotuwezesha kumpata muuaji.." Alimalizia kusema Detective Stevens.
Jioni hiyo kituo cha televisheni cha BBC, katika kipindi chake cha matukio ya uhalifu maarufu kama Crimewatch walirudia matangazo yanayoonyesha mchoro wa Lin, Josie na Megan wakitembea kurudi nyumbani, na picha ya mchoro ya mtuhumiwa wa mauaji hayo. Kuonyeshwa kwa tukio hilo katika kipindi hicho kuliamsha hisia za watu wengi na haraka sana simu zilianza kumiminika katika kituo hicho cha televisheni. Mpaka usiku wa manane kulipokelewa simu zaidi ya 1,000 za watu waliodai kuwa na taarifa zitakazowasaidia Polisi kumkamata muuaji.
Wiki moja baada ya kipindi kile kurushwa, Polisi walifanikiwa kumkamata mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la Michael Stone aliyekuwa na umri wa miaka 37 wakati huo. Walimkamata katika nyumba aliyokuwa akiishi iliyoko katika eneo la Gilligham Kent. Michael Stone alielezewa kama mtu asiye na mke na mpweke asiye hata na rafiki. Alihojiwa na askari wa upelelezi kwa muda wa masaa 96, kabla ya kufikishwa mahakamani na kushitakiwa kwa makosa ya mauaji ya watu wawili na jaribio la kutaka kuua.
Siku mbili baadae Michael Stone alitakiwa kusimama katika gwaride la utambulisho lilioitishwa na askari wa upelelezi na wale watu wote waliotoa maelezo kwa askari wa upelelzi kwamba siku hiyo ya mauaji walimuona mtu mwenye sura ya kutiliwa mashaka katika eneo hilo, waliitwa ili kumtambua muuaji huyo. Ingawa shahidi muhimu katika kesi hiyo alikuwa ni Josie, lakini askari wa upelelezi walisita kumuita kwa sababu hawakuwa na uhakika kama angeweza kukabiliana uso kwa uso na muuaji huyo.
Hata hivyo Detective Chief Inspector Stevens aliandaa gwaride la utambulisho katika kituo cha polisi cha Rainham ambacho kina eneo maalum kwa kazi hiyo ya utambulisho. Josie aliweza kumuona muuaji wa mama yake na dada yake kwa njia ya video. Baada ya gwaride hilo, la utambulisho Detective Stevens alikataa kusema iwapo Josie au mashahidi walioletwa waliweza kumtambua muuaji Michael Stone, lakini alizungumzia jinsi upelelezi ulivyofanyika kwa ujumla. Akiongea na waandishi wa habari alionyesha kuwa na imani zaidi na ushahidi wa vipimo vya DNA ambayo vimeonekana kuleta mafanikio makubwa katika miaka ya karibuni.
Wataalamu walichukua mabaki ya nywele yaliyokutwa kwenye vipande vya taulo iliyotumika kuwafunga wahanga hao kabla ya kuuwawa ambavyo vilikutwa katika eneo la tukio. "Tunaamini yeye ndiye muhusika wa tukio hilo." Alisema Ditective Stevens. "Tunazo sampuli za nywele tulizozitoa katika vipande hivyo vya taulo ambapo tutachukua vipimo kutoka kwa mtuhumiwa, kwani zaidi ya watuhumiwa 100 wameshatoa sampuli zao za DNA kwa ajili ya vipimo na walishaondolewa tuhumua hizo. Sasa ni muda muafaka kuchukua sampuli za Michael Stone kwa vipimo hivyo vya DNA, na majibu yatapatikana baada ya wiki tatu.
Kuanzia siku hiyo Ditective Stevens alikuwa kama anacheza karata zake huku akiwa amezificha mkabala na kifua chake. Alikataa kuzungumzia maendeleo ya vipimo hivyo na jinsi upelelezi unavyoendelea. Lakini ilitosha tu kuamini kwamba vipimo havikumtoa Michael Stone katika tuhuma hizo, kwani aliendelea kusota rumande huku akisubiri kufikishwa mahakamani. Baada ya Michael Stone kukamatwa, Josie na baba yake walirudi katika nyumba yao iliyoko Wales na kuanza maisha mapya. Josie alimudu kurudi shuleni na kuendelea na masomo, na taratibu maisha yake na baba yake yalainza kurudi na kuwa ya kawaida.
Mnamo April, 1998, Mamlaka inayohusika na kulipa fidia kwa watu waliaoathiriwa na uhalifu (Criminal Injuries Compensation Authority) ilimtunukia Josie kiasi cha dola 30,000 kwa kumpoteza mama yake, dola 8,000 kwa majonzi aliyoyapata na dola 3,500 kwa mwaka kwa kukosa malezi ya mzazi wake. Hata hivyo kulikuwa na kelele nyingi kutoka kwa wananchi, bunge la nchi hiyo pamoja na vyombo vya habari kuhusiana na fidia hiyo. Waziri mmoja wa wakati huo Jack Straw alikiri kuhusu udhaifu huo wa sheria, na alisikitika kwamba hana mamlaka ya kuingilia juu ya maamuzi hayo. Lakini alimtaka baba wa mtoto Josie, Dr. Shaun Russell kukata rufaa kwa niaba ya binti yake.
Wakili wa Josie, Sarah Harman alisema watakata rufaa.
Damien Daley
Mnamo mwaka 1998 Michael Stone alikutwa na hatia kutokana na ushahidi uliotolewa na mfungwa mwenzie aliyekuwa naye gerezani aitwae Damien Daley wakati akiwa anasubiri kufikishwa mahakani ambapo mfungwa huyo alidai kwamba Michael Stone aliwahi kukiri mbale yake kwamba ni yeye aliyehusika ka mauaji hayo. Alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani.
Baada ya majaribio kadhaa ya kukata rufaa, mnamo Decemba 21, 2006 mahakama ya rufaa ilitoa uamuzi kwamba Michael Stone atumikie angalau kifungo cha miaka 25 jela ndipo anaweza kufikiriwa kutolewa kwa msamaha wa Parole. Hiyo inaonyesha kwamba ibabidi akae gerezani hadi mwaka 2023 ambapo kama atatolewa, basi atakuwa amefikisha umri wa miaka 63.
Josie anafanya nini kwa sasa...?
Josie alifanikiwa kumaliza elimu ya juu katika chuo cha Coleg Menai kilichopo Bangor na kufanikiwa kupata shahada yake ya graphic design hapo mnamo mwaka 2009. Alianzisha mradi wake mwenyewe wa kutengeneza na kuuza kadi za salaam alizokuwa akizitengeneza kiusanii kabla na kupanua wigo wa biashara zake kwa kuanzisha mradi mwingine wa sanaa ya uchoraji ambapo kazi zake zimefikia thamani ya paundi 500 kwa kila kazi moja.
Amefanikiwa kuanzisha website yake inayoonyesha kazi zake, unaweza kubofya hapa kuona kazi zake: www.josierussell.com.
Josie na mpenzi wake Iwan Griffith
Kwa sasa anaishi na mpenzi wake aitwae Iwan Griffith na wana matarajio ya kufunga ndoa.
Hii hapa chini ni Documentary inayosimulia tukio zima lililoikumba familia hiyo:
Last edited by a moderator: