Na Waandishi WETU
SIKU saba zinaisha leo tangu kuwasilishwa kwa ripoti ya kuchunguza matukio mabaya yaliyoharibu taswira ya Tanzania yaliyosababisha watu zaidi ya 500 kuuawa, lakini hakuna aliyewajibika.
"Katika dunia ya kuthamini utu, kujali maslahi ya taifa na utulivu wa nchi, kunapotokea majanga makubwa yanayosababishwa na siasa, wahusika waliokuwa na dhamana wakati wa matukio mabaya; iwe kwa lazima au utashi wao, huchukua hatua za kuwajibika – kujiuzulu, anasema Julius Kamanzi, aliyejitambulisha kuwa mwanaharakati na mtetezi wa haki za binadamu.
Lakini licha ya tukio la Oktoba 2025 kuweka historia ya kupoteza maisha ya watu wengi, hili halijafanyika kwa baadhi ya viongozi wa Tanzania ambao – kwa njia moja ama nyingine, bado wapo ndani ya ofisi za umma hadi leo.
Pambazuko limefikiwa na watu 29; wanawake saba na wanaume 22, waliofika ofisini, Mtaa wa Mpakani A, Sayansi – Kijitonyama, Dar es Salaam wakielezea masikitiko kwa baadhi ya watendaji wa serikali ambao wanapaswa kuwa wamejiuzulu nyadhifa zao kwa kuwajibika na kutekeleza matakwa ya utawala bora.
Pia, baadhi ya watu wametuma ujumbe kwa njia mbalimbali, kupiga simu wakishangaa; "Aisee! Yaani bado kuna watendaji wako ofisini kwa mauaji yale?" Ripoti ya Chande inasemaje? Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani Oktoba 29, 2025 iliyokabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan wiki moja iliyopita inaonyesha kuwa idadi ya Watanzania waliouawa katika vurugu hizo walikuwa 518.
Akisoma ripoti hiyo Aprili 23,2026 mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu (mstaafu) Mohamed Chande alisema jumla ya watu 518 waliuawa, ambapo, wanaume ni 490, sawa na asilimia 94.6 na wanawake ni 28, sawa na asilimia 5.4.
Alisema vingi kati ya vifo hivyo vilikuwa siyo vya kawaida (unnatural), ambapo Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na vifo vingi zaidi, ukiwa na vifo 182, ikifuatiwa na Mkoa wa Mwanza vifo 90; Mbeya vifo 80 na Mkoa wa Arusha vifo 53.
“Kati ya vifo hivyo 518, ishirini na moja (21) vilikuwa vya watoto. Katika kundi hilo, 15 walikuwa watoto wenye umri kati ya miaka 15 – 17, wanne (4) walikuwa na umri kati ya miaka 7 - 10, na wawili (2) umri chini ya miaka mitano,” anasema Jaji Chande na kuongeza:
“Vifo 502 sawa na asilimia 96.9 vilikuwa vya raia (civilians), na 16 sawa na asilimia 3.1 vilikuwa vya maofisa na askari wa vyombo vya ulinzi na usalama. Kati ya watu 518 waliofariki, 373 walifikishwa hospitali wakiwa wamefariki, majeruhi 121 walifariki wakati wakiwa wanapatiwa matibabu, na maiti 24 hakuna taarifa kutoka vituo vya kutolea huduma za afya. Kati ya maiti 518, maiti 480 sawa na asilimia 92.7 zilitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu na familia.”
Wanaonyooshewa kidole Viongozi wanaonyooshewa kidole kiuwajibikaji ni pamoja na waliokuwa mawaziri wakati wa machafuko hayo; Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa, ambaye taasisi aliyokuwa akiiongoza ndiyo yenye dhima ya kuhakikisha ulinzi wa watu na mali zao.
Pia panga la uwajibishaji, wananchi hao wanapendekeza, litue kwa viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama akiwamo Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jenerali Jacob Mkunda, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camilius Wambura na Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), Seleiman Mombo.
Walivyohusika
Kuhusika kwa viongozi kunatokana na maelekezo waliyokuwa wakiyatoa pamoja na kusimamia vyombo vya ulinzi na usalama vinavyotuhumiwa kusababisha mauaji. Mapema Januari 22, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan alilitaka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kujiandaa kikamilifu na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Akihutubia katika mkutano wa saba wa Mkuu wa Majeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Makamanda kwa mwaka 2023, Rais Samia alisema; “Ombi langu kwenu Rais Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye hafla ya kupokea Ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025, Ikulu jijini Dar es Salaam. ni kwamba, mwaka huu na mwakani tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa nchi yetu…” “… na hapa ndipo usalama mkubwa ndani ya nchi yetu unapotakiwa kuangaliwa kwa ukaribu zaidi.
Kwa hiyo niwaombe Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwenye kamandi zenu kujipanga zaidi.” Kauli hiyo ilizua mijadala mitandaoni, ambapo baadhi ya watu walihoji sababu ya kulitaka Jeshi lijiandae kwenye mchakato wa demokrasia unaowapa haki wananchi kuchagua viongozi wao.
Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 Rais Samia alisikika mara kadhaa akionya watu wanaopanga kuandamana wakati wa uchaguzi na salamu hizi zikiaminika kuwalenga wakuu wa vyombo vya usalama.
Wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2025, Rais Samia alisikika mara kwa mara akijitambulisha kuwa yeye ni Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania, akiwaonya watu waliopanga kufanya maandamano katika uchaguzi huo.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Gombani ya Kale, Pemba Septemba 20, 2025, Rais Samia alisema; “Niwatoe hofu kwamba, tarehe zile za kupiga kura hakutakuwa na vurugu yoyote, tokeni kwa wingi kapigeni kura…”
"… Vyombo vya ulinzi vimejipanga vyema kuilinda nchi hii na mimi ndiye Amiri Jeshi Mkuu. Tumejipanga vyema kuilinda nchi hii. Kwa hiyo hakutakuwa na nywinywinywi wala nywinywinywi. Naomba watu tokeni, amshaneni kapigeni kura.”
Kauli kama hiyo alitoa pia Oktoba 22, 2025 alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Leaders Club, Dar es Salaam, alipowahakikishia wanachama wa CCM na wananchi wengine kuwa hakutakuwa na vurugu hivyo wakapige kura bila hofu.
“Nataka niwaambie, maandamano yatakayokuwepo ni ya watu kwenda vituoni kupiga kura. Hakuna maandamano mengine yatakuwepo, hakuna tishio la usalama litakalokuwepo,” alisema.
Kauli za mawaziri
Moja ya kauli zinazotajwa kuwa zinaweza kumuweka pabaya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa ni ile aliyoitoa Oktoba 15, 2025 wilayani Karagwe, Kagera, akiwaonya waliopanga kuandamana.
“Hakutakuwa na mtu yeyote atakayethubutu kuandamana Oktoba 29, atakutana na kisiki. Niwaombe vijana wa Tanzania msikubali kuungana na mkumbo huo,” alisema.
Licha ya aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax kutotoa kauli yoyote dhidi ya waliokuwa wakipanga kuandamana, hata hivyo, dhamana yake inahusishwa na tuhuma hizo kutumika kwa nguvu kubwa wakati wa kile kinachotajwa kuwa “kudhibiti vurugu wakati na baada ya uchaguzi.”
Wakuu wa usalama Viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama wanatajwa kuhusika moja kwa moja kutoka na dhima yao ya kutakiwa kutafuta taarifa za kiintelijensia kuhusiana na mipango ya maandamano na vurugu ili kuchukua hatua ya kudhibiti.
Kwamba vifo vingi vilivyobainika na Tume ya Rais kuwa vilikuwa si vya kawaida, huku miili mingi ikionekana kuchomwa na vitu vyenye ncha kali, inaaminika kuwa watu hao waliuawa kwa kupigwa risasi.
Jambo hilo nalo linaviweka vyombo vya ulinzi na usalama kwenye tuhuma za ushiriki katika udhibiti wa vurugu hizo na kusababisha mauaji na majeruhi ya wananchi walioandamana na hata wale ambao hawakuandamana.
Waliowahi kuwajibika
Kutokana na kuwepo kwa baadhi ya matukio ya vifo vilivyosababishwa na vyombo vya ulinzi na usalama, Januari 22, 1977, aliyekuwa Rais wa Tanzania - Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, aliwahi kuachia ngazi ya uwaziri wa Mambo ya Ndani. Mwinyi, wakati huo akiwa waziri alimuandikia Rais Julius Kambarage Nyerere barua ya kujiuzulu wadhifa huo.
Ali Hassan Mwinyi alijiuzulu kutokana na ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanyika wakati wa operesheni maalum ya kuzuia mauaji ya vikongwe katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga.
Alieleza kwamba alijitolea mwenyewe kujiuzulu bila shinikizo kutoka kwa Mwalimu Nyerere au mtu mwingine yeyote. Katika sentensi ya mwisho ya barua hiyo, aliongezea, “Kwa fedheha hii, naomba unikubalie nijiuzulu."
Mawaziri nao wajiuzulu
Kufuatia ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji, mateso, na uporaji, wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili mawaziri wanne walijiuzulu Desemba 2013.
Mawaziri waliwajibika ni pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dkt. Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Mathayo David.
Operesheni hiyo iliyoanzishwa kupambana na majangili ilibadilika na kuwa ya mateso dhidi ya wananchi, ikijumuisha mauaji, utesaji, na hata kulazimisha wanaume kufanya mapenzi na wanyama au miti.
Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilifichua ukiukwaji huo mkubwa wa haki za binadamu, na kusababisha wabunge kushinikiza mawaziri kuwajibika. Rais Jakaya Kikwete alitengua uteuzi wao baada ya ripoti kuonyesha kuwa wizara zilizokuwa zikiongozwa na wanasiasa hao zilihusika katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Hata katika matukio hayo, idadi ya watu waliouawa hawakufikia 518, idadi inayotajwa na Tume ya Jaji Chande kwenye kadhia ya Oktoba 29 mwaka jana.
Mauaji ya Kenya
Kufuatia vurugu za uchaguzi mkuu wa Kenya wa mwaka 2007, ambapo zaidi ya watu 1,000 waliuawa na mamia kupata ulemavu huku wengine wakilazimika kuhama makazi na hata nchi yao, nazo zilileta hatua za uwajibikaji.
Uchaguzi huo uliotawaliwa na ‘rafu,’ ulimpa ushindi Mwai Kibaki wa PNU dhidi ya aliyekuwa mgombea wa ODM, Raila Odinga. Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wasira (wa kwanza kulia) akiwa na viongozi wastaafu wakati wa hafla ya ripoti ya tume Ikulu jijini Dar es Salaam.
Viongozi wa dini wakiwa katika hafla ya ripoti ya tume. Hata hivyo, Odinga alipinga ushindi huo na ndipo vurugu zilipozuka. Kutokana na hali hiyo, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kibinadamu (ICC), ilianza uchunguzi kuhusu waliodaiwa kuwajibika.
Baada ya uchunguzi huo, Rais mstaafu wa Kenya wakati huo akiwa waziri, Uhuru Kenyatta alishtakiwa na ICC kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya ubinadamu, ikiwemo kuhusika katika kupanga au kusaidia mashambulizi dhidi ya jamii zilizodaiwa kumuunga mkono mpinzani wa kisiasa. Mashtaka yalihusisha madai ya kufadhili au kuratibu makundi yaliyotekeleza mashambulizi katika maeneo kama Naivasha na Nakuru.
Hata hivyo, mwaka 2014, ICC ilifuta kesi dhidi yake kutokana na kile ilichosema ni ukosefu wa ushahidi wa kutosha, huku kukiwa na madai ya kuingiliwa kwa mashahidi na ukosefu wa ushirikiano wa serikali ya Kenya.
Mwingine aliyeshtakiwa ni William Ruto, aliyekabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa madai ya kuandaa na kuhamasisha mashambulizi dhidi ya wafuasi wa chama pinzani katika Bonde la Ufa (Rift Valley).
ICC ilidai kuwa Ruto alihusika katika kupanga mashambulizi dhidi ya jamii fulani baada ya uchaguzi. Mwaka 2016, kesi yake ilifutwa pia kutokana na uhaba wa ushahidi, huku majaji wakitaja matatizo kama mashahidi kubadili kauli au kutowasiliana tena.
Licha ya kesi hizo, Uhuru Kenyatta na William Ruto waliungana kisiasa na kushinda uchaguzi wa 2013 nchini Kenya. Mwingine aliyeshtakiwa ICC alikuwa mtangazaji wa Kass Radio FM, Joshua arap Sang, ambaye alishtakiwa pamoja na William Ruto kwa makosa ya mauaji, uhamishaji wa kulazimishwa watu, na mateso. Sang alituhumiwa kutumia kipindi chake kuratibu na kuchochea vurugu.
Hata hivyo, kesi hiyo pamoja na ya Ruto ilifutwa kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha.
Waziri Mkuu Nepal
Machi 26, 2026 aliyekuwa Waziri Mkuu wa Nepal, Sharma Oli alikamatwa kufuatia mauaji ya mwaka jana Septemba, 2025 wakati wa maandamano ya Gen Z ambapo watu 70 waliaga dunia.
Oli alijiuzulu kufuatia hasira kali ya umma baada ya vifo vya watu waliouawa kwenye makabiliano kati ya polisi na waandamanaji waliokuwa wakipinga ufisadi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi yake, kujiuzulu kwake kulilenga kufungua njia ya kupatikana kwa suluhisho la kikatiba kufuatia maandamano makubwa yanayoongozwa na vijana, yaliyosababishwa na tuhuma za ufisadi uliokithiri na marufuku ya mitandao ya kijamii ambayo sasa imeondolewa.
Maandamano hayo yaligeuka kuwa ya vurugu baada ya maelfu ya waandamanaji, wengi wao wakiwa wamebeba mabango yaliyokuwa na maandishi kuwa ni vijana wa kizazi cha Gen Z, kuingia barabarani jijini Kathmandu.
Inakadiriwa kuwa watu takriban 200 walijeruhiwa katika makabiliano hayo, ambapo polisi walitumia gesi ya kutoa machozi, magari ya maji kuwatawanya waandamanaji, na hata risasi za moto. Waandamanaji walivamia jengo la bunge na majengo mengine ya serikali, huku wakichoma moto jengo la bunge, makao makuu ya Chama cha Congress cha Nepal, na nyumba ya aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Sher Bahadur Deuba.
Nyumba za viongozi wengine wa kisiasa pia zilivamiwa na kuharibiwa.
Viongozi wengine
Rais wa zamani wa Serbia na Yugoslavia, Slobodan Milošević alikamatwa mwaka 2001 na kupelekwa ICC, alikoshtakiwa kwa mauaji ya halaiki (genocide) na uhalifu dhidi ya ubinadamu wakati wa vita vya Bosnia na Kosovo. Alifariki akiwa gerezani mwaka 2006 kabla ya hukumu kutolewa.
Mwingine ni Rais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor aliyekamatwa mwaka 2006 na kuhukumiwa mwaka 2012. Alipatikana na hatia ya kusaidia waasi waliotekeleza mauaji na ukatili mkubwa nchini Sierra Leone na alifungwa kifungo cha miaka 50 jela.
Ingawa kesi yake ilisikilizwa katika kituo cha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) huko T he Hague, ilisimamiwa na Mahakama Maalum ya Sierra Leone (SCSL) inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa. Mwingine ni Rais wa zamani wa Sudan, Omar al-Bashir aliyeondolewa madarakani mwaka 2019 na baadaye kukamatwa na mamlaka za Sudan.
Alishtakiwa na ICC kwa mauaji ya halaiki katika eneo la Darfur, lakini mpaka leo bado kuna mjadala kuhusu kupelekwa kwake ICC.