View attachment 3585080
Chama cha Mapinduzi (CCM), kinatarajia kufanya uamuzi mgumu wa kuridhia kung’atuka kwa Katibu Mkuu wake, Dk Asha-Rose Migiro na kupitisha jina la kada mwingine kushika nafasi hiyo, taarifa zinaeleza.
Mbali ya Dk Asha-Rose, taarifa zinaeleza kuwa Makamu Mwenyekiti, Stephen Wasira huenda akapumzika na nafasi yake kuchukuliwa na Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa huku Sekretarieti ikipitiwa na panga pangua.
Uamuzi huo mgumu unatarajiwa kufanyika Dodoma kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan. Wakati wajumbe wa NEC wakiwa njiani kwenda Dodoma, swali linalogonga vichwa vya wengi ni kuhusu atakayekuwa mrithi wa Balozi Asha-Rose.
Ingawa Rais Samia anaweza kuja na jambo la kushangaza, kwa jina lisilotarajiwa na wengi, lakini duru za siasa zinataja majina ya baadhi ya wanasiasa maarufu mmoja wao kukalia kiti hicho. Wanaotajwa ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, Mbunge wa zamani wa Bumbuli, Januari Makamba, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.
Duru za siasa ndani ya CCM, zinaeleza kuwa Dk Asha-Rose aliomba kujiuzulu muda mrefu ili kupumzika, kutokana na majukumu makubwa ya nafasi tofauti alizotumikia kitaifa na kimataifa. Sababu nyingine inayotajwa ya kujiuzulu kwa Dk Asha-Rose ni kutokana na umri wake kuwa mkubwa (miaka 69) kiasi kwamba imekuwa vigumu kwake kukimbizana na majukumu ya kila siku ya utendaji mkuu wa chama.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa aliombwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia kushika nafasi hiyo kwa muda, ili kukivusha chama kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu uliopita. Inaelezwa, kwamba hatua ya Rais Samia kumteua Dk Asha-Rose kuwa mwanamke wa kwanza kushika kiti hicho, ilitokana na hofu ya makundi ya urais, yeye akiwa chaguo sahihi kwani hana chembe ya makundi yanayotafuna chama hicho kwa muda mrefu.
Hatima ya Dk Asha-Rose kung’atuka, ilitarajiwa kujulikana Mei nne mwaka huu kwenye kikao cha NEC, lakini kiliahirishwa hadi Mei saba kutokana na ugeni wa marais wa Kenya, William Ruto na Paul Kagame wa Rwanda.
Awali, NEC ilitarajiwa kukutana Februari mwaka huu, lakini wajumbe wakiwa tayari wamejulishwa, mkutano huo ukaahirishwa. Mbali na kung’atuka, taarifa zaidi zinaeleza kuwa huenda Mwenyekiti Samia akatumia nafasi hiyo kufanya mabadiliko makubwa kwenye Sekretarieti ya chama iliyokuwa chini ya Dk Asha-Rose.
Wajumbe wengine mbali ya Dk Asha-Rose ni Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mongela; Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Mohamed Said Mohamed ‘Dimwa’ na Katibu wa NEC Oganaizesheni, Issa Haji Gavu. Pia Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Kenani Kihongosi, Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Himid na Katibu wa Sektretarieti.
Yumo pia Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake (UWT), Suzane Kunambi, Katibu Mkuu Jumuiya ya Wazazi, Ally Happi na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM), Khalid Mwinyi.
“Kama Katibu Mkuu anaondoka, sioni Sekretarieti ikibaki salama, kuna uwezekano mkubwa wa kupitisha panga la nguvu hasa ukizingatia kuwa tangu uchaguzi ulipomalizika, hajafanya mabadiliko kwenye chama,” alisema mtoa taarifa wetu.
Moja ya sababu zinazotajwa kuhusu mabadiliko hayo ni mwenendo wa Sekretarieti inavyofanya kazi, kwani tangu wakati na baada ya uchaguzi mkuu na yaliyotokea Oktoba 29 mwaka jana, hakuna aliyepambana kusafisha hali ya hewa na kuacha mzigo wote kwa Rais Samia.
Baadhi ya makada wa CCM, walisema mbali na Sekretarieti ya chama hicho kushindwa kwenda na kasi ya Rais Samia, wameshusha lawama kwa jumuiya za CCM. Jumuiya hizo ni pamoja na Umoja wa Vijana (UVCCM), Umoja wa Wanawake (UWT) na Jumuiya ya Wazazi.
Hata hivyo, hakuna kiongozi wa CCM aliyethibitisha taarifa hizi kwani Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo Taifa, Kenani Kihongosi alisema hana taarifa za Dk Asha-Rose kuomba kujiuzulu na hajui kama kuna mkutano wa NEC.
Baadhi ya makada wa CCM, walileza kuwa Dk Asha-Rose aliyedumu muda mfupi kwenye nafasi hiyo kuliko waliomtangulia. Aliingia kwenye nafasi hiyo Agosti 23 mwaka jana, huku akithibitishwa na CCM kuwa Katibu Mkuu mpya, akichukua nafasi ya mtangulizi wake Balozi Emmanuel Nchimbi.
Tangu aliposhika nafasi hiyo, Balozi Asha-Rose alionekana zaidi kwenye majukwaa ya kampeni, akimnadi mgombea urais Samia kupitia CCM, Dk Asha-Rose aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) alichukua nafasi hiyo baada ya Balozi Nchimbi kuchaguliwa na CCM kuwa mgombea mwenza wa Samia kwenye uchaguzi mkuu mwaka jana.
Makatibu wakuu wa CCM waliotangulia ni Pius Msekwa (1977-1982), Rashid Kawawa (19821990), Horace Kolimba (1990-1995), Lawrence Gama (1995-1997) na Philip Mangula (1997-2007).
Wengine ni Yusuf Makamba (2007-2011), Wilson Mukama (2011-2012), Abdulrahman Kinana (2012-2018), Dk Bashiru Ally (2018-2021), Daniel Chongolo (2021-2023), Dk Nchimbi (20242025) na Dk Asha-Rose (2025 hadi leo).
Chanzo: Raia Mwema.