Pinda kufa na mkataba kampuni ya familia ya Kingunge Ubungo
2009-03-16 10:29:35
Na Mashaka Mgeta
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ameagiza Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), kukagua hesabu za makusanyo ya fedha katika kituo kikuu cha mabasi kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam.
Makusanyo ya fedha hizo, yanafanywa na kampuni ya Smart Holdings inayomilikiwa na familia ya Mbunge wa kuteuliwa na Rais, Kingunge Ngombale-Mwiru.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana, alipokuwa akizungumza katika kikao cha majumuisho, baada ya ziara yake ya siku tatu jijini Dar es Salaam.
Alisema bila kujali mmiliki halali wa kampuni hiyo, ukaguzi wa hesabu hizo unapaswa kufanyika kwa maslahi ya umma, kabla ya kuchukua hatua kwa mujibu wa mapendekezo yatakayotolewa na CAG.
``Mimi sijui ni nani anayemiliki ile kampuni, lakini hapa ninachokizungumzia kinahusu maslahi ya umma. Tuone hicho kinachofanyika huko ni kwa maslahi ya nani,`` alisema Pinda katika mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee.
Pinda, alisema inashangaza kuona licha ya kuwepo mazingira yanayothibitisha kupatikana kwa kiasi kikubwa cha fedha, serikali inaambulia Sh. milioni 1.5 pekee kwa siku.
Katika hali iliyoonyesha kuchukizwa na hali hiyo, Pinda alisema ukaguzi huo unapaswa kufanyika haraka, ili kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kisizidi kupotea.
``Tusijidanganye kwamba mkataba bado una muda wake kabla ya kuisha, (mkataba) utaendeleaje kuwepo wakati tunazidi kupoteza... CAG afanye kazi yake na ushauri atakaotupatia ndio tutakaoufanyia kazi,`` alisema.
Pinda alisema ukaguzi huo unapaswa kufanyika hadi katika vibanda vilivyomo ndani ya kituo hicho, ili kubaini ikiwa kuna baadhi visivyolipa mapato serikalini.
Alisema kituo cha Ubungo ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya mapato ikiwa usimamizi wake ungefanyika kwa ufanisi zaidi.
Aidha, Waziri Mkuu, alisema licha ya kituo hicho, CAG atafanya ukaguzi kama huo katika Soko la Kariakoo, ambalo uongozi wake unadhihirisha kutokuwa na uwezo wa kusimamia uendeshaji wake.
Siku moja baada ya ziara ya Waziri Mkuu kituoni hapo, kampuni ya Smart Holdings ilisema madai yaliyotolewa dhidi yake hayana ukweli wowote.
Mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo, Hassan Khan alisema kilichodhihirika ni kwamba, viongozi wa Jiji waliokuwapo kwenye ziara hiyo, hawajui lolote kuhusu mkataba huo na ndio maana wakashindwa kumueleza Waziri Mkuu ukweli kuhusu suala hilo.
Khan alisema katika mkataba huo, walikubaliana na Halmashauri ya Jiji kwamba, watakuwa wakiilipa asilimia 75, lakini akashangaza kusema kwamba asilimia hiyo ni Sh. milioni 1.5 na kwamba watakuwa wanalipa kiasi hicho kwa kila siku bila kujali hali ya mapato itakayokuwa kituoni hapo.
Khan alisema siku za wikiendi na wakati madaraja yanapokatika, kampuni yao hupata hasara.
Katika hatua nyingine, Pinda, alizitaka halmashauri za manispaa za Ilala, Temeke na Kinondoni, kuweka utaratibu wa kuboresha mazingira ya masoko na kuondoa uchafu uliokithiri kwenye maeneo kadhaa jijini.
Waziri Mkuu aliwaambia watendaji na viongozi kuwa masoko mengi ya jijini hayapo katika hali nzuri, hivyo kutowapa wafanyabiashara fursa nzuri za kunufaika kiuchumi.
Pia alisema uchafu umekithiri kwenye maeneo mengi, hivyo kutaka ongezeko la kasi ya kuondokana na hali hiyo.
Kuhusu kero ya usafiri wa wanafunzi katika Jiji la Dar es Salaam, Waziri Mkuu aliutaka uongozi wa manispaa hizo kubuni mbinu mbadala, ikiwemo matumizi ya mabasi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).
Alisema kwa kuwa tatizo hilo ni kubwa linalotegemea utekelezaji wa mradi wa mabasi yanayokwenda kwa kasi kuwa sehemu ya suluhu yake, mabasi ya UDA yanaweza kutumika kwa kipindi cha kabla ya kuanza kwa mradi huo.
Waziri Mkuu Pinda alisema kuna dalili za kuwepo vitendo vya rushwa kwa watendaji wa halmashauri ya Jiji na Manispaa ya Ilala katika ugawaji wa mabanda ya biashara katika soko la Mchikichini.
Alisema baadhi ya wafanyabiashara walielezea kuwepo mabanda yasiyokuwa na watu kutokana na watendaji wasiokuwa waaminifu na wanaosimamia soko hilo, kutaka hongo kutoka kwao (wafanyabiashara).
``Hatuwezi kwenda hivyo, hebu gavana (Mkuu wa Mkoa) ingilieni kati suala hili, mtangaze ili vibanda vile vipate watu,`` aliagiza.
SOURCE: Nipashe