SEASON 2
SEHEMU YA 22
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
“ Flaviana do something my love.Fanya kila unavyoweza ili niweze kuipata ripoti hiyo” akasema Elibariki.Flaviana akakaa tena kimya kidogo halfu akauliza
“ Unaitaka lini hiyo ripot?
“ Haraka iwezekanavyo na kama ukiweza kuipata usiku huu itakuwa vizuri zaidi” akasema Elibariki
“ Ok ngoja niangalie namna ya kufanya kama nikifanikiwa kuipata nitakutaarifu.”
“ Nashukuru sana Flaviana , nitaarifu mara moja endapo ukifanikiwa na nitakufahamisha ni wapi tukutane ili unipatie.”akasema Elibariki na kukata simu.Mathew akatabasamu na kusema
“ You did great.Your wife loves you so much” akasema Mathew.Elibariki akatabasamu
“ I don’t know” akajibu Elibariki
“ Anyway tuachane na hayo.Wakati tunamsubiri Flaviana apige simu ,mpatie Anitha laini yako ya simu na tuanze kuifanyia kazi ile namba ya yule mwanamke aliyekupigia na kukupa onyo kuhusiana na kuwepo kwa shambulio.” Akasema Mathew na jaji Elibariki akamkabidhi Anitha simu yake na wote wakaelekea katika chumba ambacho wenyewe wanakiita chumba cha kazi.
ENDELEA………………..
Flaviana hakuwa na habari kwamba maongezi yote aliyoongea na mume wake Elibariki yalikuwa yakisika katika kifaa Fulani kilichokuwa ndani ya gari moja jeusi lililokuwa maeneo ya ikulu ambalo hutumiwa na watu wa usalama.Flaviana hakuwahi kugundua kama simu yake imeunganishwa na kifaa hicho na kwamba kila atakachoongea simuni basi kitasikika kwa watu wale kupitia kile kifaa cha elektroniki kilichounganishwa na simu yake kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu.Mara tu Flaviana alipokata simu bila kupoteza hata sekunde moja jamaa moja aliyekuwa amekaa katika kiti cha kushoto ndani ya lile gari akawageukia wenzake.
“ Jamani nadhani mmesikia kilichoongelewa hapa.Nini ushauri wenu,tumufahamishe Dr Kigomba?
“ Mimi nadhani tufuate maelekezo tuliyopewa.Tumtaarifu Dr Kigomba kuhusiana na taarifa hii.Alitukabidhi kazi hii kwa hiyo lazima tuifanye kama alivyotuelekeza.Mnaijua hatari yake endapo akigundua kwamba tumemficha kuhusu jambo hili” akasema jamaa aliyekuwa katika usukani
“ Hata mimini nashauri tumtaarifu tu Kigomba.” Akasema jamaa mwingne aliyekuwa amekaa katika kiti cha nyuma.Yule kiongozi wao akakaa kimya akafikiri kwa muda halafu akasema
“ Ok sawa ngoja tumtaarifu “ akachukua simu yake akampigia Dr Kigomba akamtaarifu kuhusu kunaswa kwa maongezi kati ya Elibariki na Flaviana.Kigomba akastuka sana na kuomba atumiwe maongezi yale akayasikia na kisha akamtumia Dr Joshua ambaye naye aliyasikia halafu akampigia simu
“ Dr Kigomba tumuache Flaviana afanye hivyo alivyoagizwa na mume wake.Nitampatia ile taarifa ili ampelekee mume wake.Andaa vijana mahiri wa kuweza kumfuatilia na baada ya kumkabidhi Elibariki taarifa hiyo vijana waanze kumfuatilia Elibariki na kupafhamu mahala alikojificha halafu ndipo achukuliwe na kumzimisha kimya kimya na maiti yake itupwe mbali sana ikiwezekana iharibiwe kiasi cha kutoweza kutambulika.Sitaki Elibariki aonekane tena. Kigomba hii ni fursa nyingine nzuri tumeipata na tunatakiwa tuitumie kikamilifu.Tukishindwa na hapa basi tutakuwa hatarini sana kwa sababu huyu jamaa anaonekana kutokukata tama kupambana na sisi.Anaonekana bado anaendelea kutufuatilia na ndiyo maana anataka kuipata taarifa ile.Sijui anaitaka kwa madhumuni gani lakini mwisho wake umewadia.Tafadhali Kigomba naomba kwa kila namna itakavyowezekana zoezi hili lisishindikane na tuiondoe hatari hii mbele yetu” Akasisitiza Dr Joshua
“ Nakuahidi Dr Joshau safari hii Elibariki hawezi kuponyoka.Hawezi kusalimika.Dakika alizobaki nazo ni chache sana.Nitashughulikia jambo hili mimi mwenyewe na nitakuwepo eneo la tukio ili kuhakikisha kwamba hakuna kosa lolote linalofanyika” akasema Dr Kigomba.
“ Moyo wangu utatulia na kuwa na amani pale tu nitakaposikia kwamba huyu jamaa ameondoka duniani.Ananinyima amani sana huyu jamaa ana sumu kali kuzidi ya nyoka na ni hatari mno kwetu.Sijui kwa nini Flaviana alikubali kuolewa na mtu mjinga kama Elibariki. Lakini pamoja na hayo ninaamini mwisho wake umefika .Huyu ni kijana mdogo sana na hawezi kushindana na mimi ambaye nchi yote iko chini yangu.Hawezi mtummoja akazuia mipango yangu.Lazima nimuonyeshe kwamba mimi ni rais na nina nguvu” akawaza DrJoshua na kuinuka kitandani akaenda kabatini akaichukua ile bahahsa iliyokuwa na ripoti ile ya uongo kuhusiana na kifo cha mke wake halafu akazitoa karatasi zile akaziangalia na kuzirudisha tena katika bahasha.
“ Sifahamu kwa nini anaitaka ripoti hii.Kuna kitu gani anataka kufanya ? Ama kweli sijawahi kukutanana mtu ambaye ameniumiza kichwa kama Elibariki lakini safari hii hataweza kuponyoka tena.”akawaza Dr Joshua halafu akachukua baadhi ya vito vya Dr Flora kama vile herein ,bangili na mikufu akavoweka katika boksi dogo akamuita mmoja wa walinzi wake na kumpa maelekezo avipeleke vitu vile kwa Flaviana pamoja na ile bahasha yenye taarifa ya kutunga.Baada ya mlinzi yule kuondoka Dr Joshua akachukua simu na kumpigia Flaviana
“ hallow baba.Imekuwa vizuri umenipigia kwani nilikuwa na mpango wa kukupigia sasa hivi.” Akasema Flaviana baada ya kupokea simu
“ Nimeona nisilale bila kujua maendeleo yako.Una tatizo lolote Flaviana?akauliza Dr Joshua
“ Ndiyo baba.Unaweza kunipatia ile ripoti ya kifo cha mama ? Ninataka kuipitia unajua Captain Amos alitusomea kwa ujumle wake.”Akasema Flaviana
“ Ina maana bado haijakufikia? Akashangaa Dr Joshua
“ Haijanifikia? Kwani umenitumia? FLaviana naye akashangaa
“ Ndiyo nimekutumia kitambo kidogo.Kuna vito kadhaa vya mama yako kama mikufu,heleni na vingine vidogo vidogo nimemtuma mlinzi wangu akuletee uvitunze kama kumbu kumbu ya mama yako nikiviona vinanipa uchungu sana.Nimempa pamoja na ile ripoti akuletee ili uihifadhi” akasema Dr Joshua
“ Ouh ahsante sana baba.” Akasema Flaviana kwa furaha
“ Usijali Flaviana .Kuna jambo lingine ninataka kukuomba pia,naomba umsaidie sana mdogo wako Anna ili aweze kuizoea hii hali.Kifo cha mama yake kimempa huzuni kubwa sana.Tafadhali naomba uwe naye karibu kwa sababu najua wewe ni mwanamke jasiri na umekutana na mambo mengi sana.Kitu kingine ambacho kimenifanya nikupigie simu usiku huu ni kukutaarifu kwamba bado juhudi za kumtafuta Elibariki zinaendelea kwa kasi na kwa mujibu wa taarifa niliyoipata toka kwa jeshi la polisi ni kwamba kuna matumaini ya kumpata Elibariki .Usijali Flaviana ninafanya kila juhudi ili Elibariki aweze kupatikana na ninakuahidi atapatikana tu” akasema Dr Joshua.
“ Nitashukuru sana baba .Nitafurahi sana Elibariki akipatikana akiwa mzima.Naomba uwe ukinitaarifu pindi upatapo taarifa zozote za kuhusiana na Elibariki” Akasema Flaviana na kukata simu
“ Dah ! baba ni kama alikuwa katika mawazo yangu kuhusiana na ripoti hii.Nilikuwa najiuliza sana namna ya kuweza kuipata lakini imekuwa ni kama vile kayasoma mawazo yangu.Lakini Elibariki anaitakia nini taarifa hii,anataka kufanya jambo gani ? Akajiuliza Flaviana
“ Lakini ni akina nani wanaotaka kumuua na kwa nini ? Kwa sasa nimeanza kuamini maneno yake kwamba kuna jambo linaloendelea hapa.Nimeanza kuingiwa na hofu kwamba huenda ni kweli kifo cha mama kina mkono wa mtu.Elibariki alikuwa anasisitiza sana kuhusiana na jambo hili lakini nilimpuuza lakini sasa kuna kitu nimeanza kukiona kwamba huenda alikuwa sahihi.Elibariki aliniahidikwamba lazima siku moja ukweli utafahamika na ninadhani ndiyo sababu ameitaka taarifa hii. Ngoja nitakapoonana naye usiku wa leoo nitamuomba aniweke wazi.Ninamfahamu Elibariki huwa akilikazania jambo Fulani ni lazima ahakikishe limefika mwisho.Ninamuonea huruma sana mume wangu na ninatamani sana kusikia kwamba watu waliotaka kumuua wote wamekamatwa.Huko aliko sijui yuko wapi,sijui nani anamuhudumia.Nataka awe huru na arejee nyumbani ili maisha yetu yaendelee” akawaza Flaviana huku akilengwa na machozi
******
Anitha alikuwa kimya akiendelea kucheza na komyuta yake akijaribu kutafuta namba ile ya simu iliyotumika kumpigia Elibariki na kumpatia tahadhari kuhusianana mpango wa kumuua iikuwa ni ya nani.Mathew na Elibariki wote walikuwa kimya kabisa wakisubiri amalize kazi yake.Baada ya muda wa zaidi ya dakika thelathini, Anitha akawageukia
“ Pamoja na ujuzi wangu wa kompyuta nimeshindwa kuitambua namba hii ni ya nani.Namba hii ya simu imewekwa katika mfumo ambao ni vigumu kuweza kuifuatilia na kujua mmiliki wake .Ni utaalamu wa hali ya juu sana ambao umetumika hapa.” Akasema Anitha
“ Hii inatuonyesha kwamba mtu huyu anayetumia namba hii ya simu ni mtu mwenye uzoefu mkubwa na makini katika kazi hizi na ndiyo maana hataki kuacha nyuma kitucchochote kinachoweza kumfanya akatambulika.Mtu anayefanya mambo yake katika hali ya usiri namna hii siku zote huwa ni mtu hatari sana.Tutegemee safari hii kukutana na mtu hatari sana lakini muhimu kwetu.Hakuna njia nyingine yoyote tunayoweza kufanya ili kumpata mtu huyu? Akauliza Mathew
“ kwa hapa sina tena namna ninayoweza kufanya ili kumfahamu mtu huyu ni nani labda niombe msaada kwa wenzangu wenye ujuzi zaidi yangu.” Akasema Anitha
“ kama wewe umeshindwa nadhani itachukua muda mrefu kwa mtu mwingine kuweza kulitatua jambo hili.Anyway tutatafuta namna nyingine ya kufanya ili kuweza kumfah…………” Kabla hajamaliza sentensi yake simu iliyokuwa mezani ambayo Elibariki aliitumia kumpigia mke wake ikaita. Ni namba za simu za Flaviana mke wa Elibariki
“ Mke wako anapiga” akasema Anitha na kumpatia Elibariki ile simu
“ Bonyeza kitufe cha sauti kubwa ili wote tusikie atakachokiongea” akasema Mathew
“ Hallow Flaviana” akasema Elibariki
“ Eli,tayari nimepata ile taarifa”
“ Ouh ahsante sana Flaviana.Umeipataje mapema hivi? Akauliza jaji Elibariki
“ Imekuwa ni kama bahati,mara tu uliponipigia simu nilikuwa nafikiria namna nitakavyoweza kuipata taarifa ile lakini kumbe baba naye tayari alikwisha mtuma mlinzi wake aniletee pamoja na vitu vingine vya mama.Kwa hiyo taarifa ninayo hapa na ninaomba sasa nielekeze mahala tutakapokutana ili nikupatie” akasema Flaviana
“Sawa Flaviana naomba unipe dakika mbili halafu nitakupigia na kukuelekeza ni wapi tukutane” akasema Elibariki na kukata simu akamgeukia Mathew
“ Imekuwa bahati sana kwa Flaviana kuipata taarifa ile mapema zaidi ya nilivyotegemea.Sasa ni sehemu ya kukutana.Tunakutana wapi? Akauliza jaji Elibariki
“ Kabla ya hapo kuna jambo ambalo nimelisikia na limenipa shaka kidogo” akasema Mathew
“ Jambo gani Mathew? Akauliza Elibariki
“Ni kuhusu rais kumpatia Flaviana taarifa hiyo ghafla namna hii.Ukumbuke kwamba rais alikuwa na taarifa hii toka majuzi na katika kipindi chote hicho hakumkabidhi Flavina taarifa hiyo na hakutaka mtu yeyote yule awe nayo .Najiuliza imetokea nini hadi usiku huu ampatie Flaviana taarifa hiyo tena muda mfupi tu baada ya Elibariki kumpigia simu na kumuomba afanye juu chini kuipata taarifa hiyo? Hebu jaribuni kuliona jambo hili kwa jicho la tatu ,hakuna kitu hapa? Akauliza Mathew.
“ Mhh ! hata mimi nimeanza kuhisi kitu”akasema Anitha
“ Ukijiuliza ni kwa nini rais ampatie Flaviana taarifa ile tena usiku huu unagundua kwamba hapa kuna kitu na si bure.”
“ Ahsante Anitha kwa kunielewa nilichokuwa nakimaanisha.Ukichunguza kwa undani hapa lazima utagundua kuna kitu Fulani na si bure.Rais hakuwa tayari kumpa Flaviana wala mtu yeyote yule taarifa ile na ndiyo maana akaifungia chumbani kwake.Kitendo chake cha kupatia Flaviana taarifa ile tena usiku huu na muda mfupi tu baada ya Elibariki kumpigia simu kinatia shaka na kwa kuwa mimi ni mzoefu sana katika mambo haya kuna kitu nimekihisi” akasema Mathew
“ Kuna kitu gani umekihisi Mathew? Akauliza jaji Elibariki.
“ Elibariki this is a trap.Hapa kuna mtego.Najua huwezi kuniamini lakini mimi ni mzoefu katika haya mambo na ninafahamu namna yanavyokwenda.Ninaamini kabisa kwamba huu ni mtego .Baada ya kunusurika katika ajali ile watu wale ambao hawalali wakikutafuta waliamini kabisa kwamba uko hai na waliamini kwamba mtu wa kwanza ambaye utawasiliana naye na kumjulisha kwamba uko mzima ni mke wako kwa hiyo ninahisi kuna kitu wamekiweka katika simu ya mke wako ili kuweza kunasa maongezi yote ambayo atayaongea kupitia simu yake.Ninajua Elibariki utashangaa kwa hiki ninachokuambia lakini mimi ni mzoefu katika mambo haya na niyafahamu vizuri sana .Ninachokueleza hapa nina uhakika nacho.Mpigie simu mkeo na mwambie kwamba atafute simu nyingine ndipo uweze kumpa maelekezo ya wapi pa kukutana.Usimpe maelekezo kwa kutumia simu yake’ akasema Mathew
“ Mathew ninakuamini sana.Una akili ya ajabu.Sikuwahi kuwaza kama kitu kama hiki kinaweza kufanyika” akasema Elibariki na kumpigia simu Flaviana
“ Hallow Flaviana uko karibu na Anna ? akauliza Elibariki
“ Hapana yuko chumbani kwake”
“ Naomba ukachukue simu yake na unipigie kwa kutumia simu yake” akasema jaji Elibariki
“ kwani kuna nini kinaendelea Elibariki ? Simu yangu ina tatizo gani? Hunisikii vizuri? Akauliza Flaviana
“ Naomba ufanye hivyo Flaviana.Naomba uchukue simu ya Anna ndipo nikupe maelekezo” akasema jaji Elibariki
“ Elibariki mbona unaniogopesha? Akasema Flaviana
“ Usiogope Flaviana naomba ufanye hivyo “ akasema Elibariki na kukata simu.Mathew akampa maelekezo namna ya kufanya.
Baada ya dakika mbili Flaviana akapiga simu kwa kutumia simu ya mdogo wake
“ Hallow Elibariki sasa ninatumia simu ya Anna ” akasema Flaviana
“Sawa Flaviana,naomba tukutane pale Simbona hoteli.Mbele kidogo ya hoteli ile kuna kituo cha mabasi na pale utakuta kuna gari moja aina ya Toyota carina lenye rangi ya bluu .Utafungua mlango wa nyuma na kuingia” akasema jaji Elibariki
“ Sawa Eli,nitaanza safari muda si mrefu” akasema Flaviana na kukata simu.
“ Elibariki,pamoja na mkeo kubadilisha simu yake lakini bado hatari haijaisha.Macho ya wale wanaokutafuta bado yataelekezwa kwako kwa hiyo basi nina hakika kabisa kwamba lazima atafuatiliwa hivyo lazima tuchukue tahadhari kubwa.Ili tuamini maneno niliyoyasema basi lazima tuweke mtego.Kuna mtu mmoja ambaye tunamshikilia hapa ndani tutamtumia kubaini endapo kuna mtego na kama mkeo anafuatiliwa ama vipi.Yeye atakuwa pale hotelini akiwa na ile gari aina ya Toyota carina na mkeo atakapoingia ndani ya ile gari ataiondoa na kuelekea moja kwa moja katika viwanja vya ukombozi na kama kuna mtu yeyote ambaye atakuwa akimfuatilia mkeo basi tutafahamu na kumdhibiti.Kama hakuna mtu yeyote ambaye atakuwa akimfuatilia basi atatukabidhi hiyo ripoti na tutamrejesha pale Simbona hoteli alikoacha gari lake na ataondoka zake.Lakini endapo tutagundua kwamba kuna watu wanaomfuatilia basi itatulazimu kuingia katika mapambano nao kuwafahamu ni akina nani na wametumwa na nani” Akasema Mathew.jaji Elibariki akaonekana kuwa na wasiwasi mwingi
“ Mathew are you sure my wife will be safe? Akauliza
“ Elobariki naomba nikuweke wazi kwamba hili si suala jepesi na ni jambo la hatari kubwa ,na chochote lazima kitokee lakini ninakuhakikishia kwamba tutafanya kila lililo ndani ya uwezo wetu kuhakikisha kwamba mkeo anakuwa salama. “ Akasema mathew
“ Ahsante sana Mathew.Ninakuamini kwa kila utakachokisema.” Akasema Elibariki na Mathew akatoka mle chumbani akaelekea katika kile chumba alichokuwamo yule jamaa wanayemshikilia akamuamsha
“ hallow amka !! akasema Mathew kwa ukali
“ Brother una mpango gani na mimi? Utaniweka hapa hadi lini?Ulichokuwa unakitaka nimekwisha kueleza lakini mbona huniachii? Akauliza yule jamaa
“ Kuna kazi moja ambayo nataka unifanyie na endapo ukifanya vizuri basi nitakuacha uende zako”akasema Mathew
“ Ni kazi gani hiyo brother? Niambie niko tayari”
“ Unaweza kuendesha gari? Akauliza Mathew
“Ndiyo ninaweza kuendesha.”akajibu yule jamaa
“ Good” akasema Mathew na kisha akamuelekeza yule jamaa namna mpango mzima utakavyokuwa.
“ Tutakuwa nyuma yako na endapo ukijaribu kwenda kinyume na nilivyokwambia basi sahau kabisa suala la kuachiwa huru na nitakufanyia kitu kibaya sana .Tena naomba nikuweke wazi kwamba sijakufanyia vile nilivyokuwa nimepanga kukufanyia kwa sababu ulinieleza ukweli na nikaamua kukusamehe.Vinginevyo ningekufanyia kitu kibaya sana kutokana na mambo mliyomfanyia Sabina na kwa taarifa yako Sabina amekwisha fariki dunia.Kwahiyo basi nakusisitiza kwamba unatakiwa ufanye kile tu nilichokuelekeza.Kinyume na hapo basi utakuwa unajiweka wewe mwenyewe hatarini” akasema Mathew
“ Usihofu kitu kaka.Nitafanya kama unavyotaka.Ninataka niwe huru ,ninahitaji kuendelea kuishi kwa hiyo siwezi kufanya jambo lolote la kipuuzi.Kitu kingine kaka nakuomba usinikabidhi kwa vyombo vya dola.Nikifikishwa kule nitafungwa kifungo kirefu gerezani kwani tayari rekodi zangu ziko kule .” akasema yule jamaa
“ Diwezi kukuahidi chochote kwa sasa hadi hapo nitakapohakikisha kwamba umefanya kile ambacho nimekuagiza ukifanye” .akasema Mathew halafu akatoka katika kile chumba akaenda katika gereji yake ya magari na kulitoa gari moja aina ya Toyota carina.Ni gari ambalo bado hajalisajili toka alinunue na huliweka ndani kwa ajili ya kulitumia kwa nyakati kama hizi.Alifunga namba bandia katika gari lile na kulijaribu akahakisha liko sawa akarejea ndani
“ jamani kila kitu kinakwenda vizuri.Sasa ni muda wa kujiandaa kwa ajili ya kuelekea huko.Akasema Mathew na kuwachukua Elibariki na Anitha hadi katika chumba ambacho huhifadhi silaha .Akafungua kabati na kutoa fulana nne zisizopenya risasi akawapatia Elibariki na Anitha na moja ikawa kwa ajili ya yule jamaa mwingine watakayemtumia
“ Eli,unaweza kutumia silaha ? Akauliza Mathew
“ Ndiyo ninaweza Mathew , nimewahi kupitia mafunzo katika jeshi la kujenga taifa kwa hiyo ninafahamu kutumia silaha ingawa sijawahi kuingia katika mapambano.” Akasema jaji Elibariki.Mathew akampatia bastora.
“ Ihifadhi hiyo silaha pengine tunaweza kuihitaji” akasema Mathew halafu akaelekea katika chumba alimo Yule jamaa na kumpatia fula moja isiyopenya risasi .
Walipokuwa tayari wakaingia katika gari na kuanza safari wakitanguliwa na Yule jamaa akiwa katika Toyota Carina
NINI KITATOKEA USIKU HUO? ELIBARIKI ATASALIMIKA USIKU HUO? TUKUTANE TENA SIKU YA JUMATATU ...WEEKEND NJEMA WOTE