Penzi unipalo wewe

Penzi unipalo wewe

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Joined
Mar 10, 2006
Posts
33,771
Reaction score
41,027
Penzi unalonipa
Hilo kwangu tamu sana
Penzi lisilokopa
Hilo ni penzi mwanana!
Penzi waaa!!


Penzi lanisisimua
Lapita hiyo asali
Penzi nimeligundua
Yamenitoka maswali
Penzi waaa!!

Penzi jingine sitaki
La kwako limenitosha
Penzi lingine si haki
Kwako weye nimekwisha
Penzi waaa!

Penzi na busu nipeye
Na mguso nisikie
Penzi la hamu na weye
Na raha nijipatie
Penzi waaa!

Penzi langu nipenziye
Ewe uliye mwandani
Penzi la aziza weye
Ulojichimba mtimani
Penzi waaa!!

Penzi nkuya na kuye
Nami na weye nikupe
Penzi nipeye nipaye
Kama pumzi nikupe
Penzi waaa!!

Penzi lako natamani
Maradhi unitibiye
Penzi nipate mwilini
Kama kidonge nigeye
Penzi waa

Penzi lako mafuriko
Nibebwe niende nayo
Penzi nipeleke huko
Uuteke wangu moyo
Penzi waaa!

Penzi kweli tamu sana
Hili unipalo miye
Masharti kweli halina
Wewe kwangu mimi ndiye
Penzi waaa!!

Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)
Julai 13, 2010
 
Hahahahahaah, naomba nocopy na kupate kwa mywife ila nitafanya editing kigogo tu ili iendane na kiswaili changu mamsapu alichokizoea.
 
Upendwapo maridhawa
Penzi pasipo mawaa
Penzi hilo lawalawa
Sio penzi la ngalawa
Penzi waaa!

Dunia taita pepo
Penzi hilo likiwepo
Hutochanganya mapendo
Penzi lake Hondo hondo
Penzi waaa!

Raha ya penzi upendwe
Upewe na vya mvungu
Usipewe ndembwe ndembwe
Ukajutia kilembwe
Penzi Waaa!:humble:
 
Anaza one from MMM... Tunga basi na za Injili Mzee... Pliiiiiiiiiiiiiiiiiiz
 
Asante sana Mwanakijiji Hili ni maalum kwa ajili ya nani??
Uko juu ...
 
Mwanakijiji tunga linaloelezea mpenzi aliyeumizwa na mapenzi, aliyesalitiwa..................

Asante kwa shairi tamu!
 
Msichoche mapenzi, kabla ya muda wake
Anaasa mwenye enzi, katika maandiko yake
usijitie kitanzi, wewe mtoto wa kike
Ungali mdogo wewe, kukimbilia mapenzi

Subiri muda mwafaka, ninakupa ushauri
Usije kufadhaika, nakuonya kwa shairi
majonzi yakikufika, itakuwa ni hatari
Ungali mdogo wewe, kukimbilia mapenzi

Hebu muone samia, yule binti wa mbagala
Ona anavyojutia, amezikosa fadhila
Mapenzi kakimbilia, amekuwa ka jalala
Subiri muda mwafaka, ungali mdogo bado

Haya mambo ya kikubwa, usiwe nayo haraka
wadanganywa kwa ubwabwa, utaishia dhihaka
ni spesho kwa wakubwa, subiri muda mwafaka
We kazana na masomo, mapenzi ni ya wakubwa
 
Anaza one from MMM... Tunga basi na za Injili Mzee... Pliiiiiiiiiiiiiiiiiiz

Hoja yako asikofu, mimi nimeisikia
naomba ondoa hofu, shairi ninakuletea
ngoja niipange safu, injili nakufikishia
Shairi la kiinjili, kaburunye nalileta

maandiko nimesoma, kitabu cha biblia
kimesheeni hekima, mi nakuhakikishia
Neno ukiliandama, shida lakuondolea
Injili uweza wa Mungu, uuletao wokovu

Neno la Mungu jamani, mambo yake ni hakika
shuhuda limesheheni, tena halina dhihaka
yaani laleta imani, maandiko ukishika
Injili uweza wa Mungu, uuletao wokovu

Siwezi kulikataa, limeosha dhambi zangu
Neno la Mungu ni taa, na mwanga wa njia yangu
Acheni kunishangaa, hebu mwaminini Mungu
Injili uweza wa Mungu, uuletao wokovu

Neno laleta amani, moyoni ukiliweka
wewe unangoja nini, ili upate pumzika
fanya uamuzi makini, na mbinguni utafika
Injili uweza wa Mungu, uuletao wokovu
 
Hoja yako asikofu, mimi nimeisikia
naomba ondoa hofu, shairi ninakuletea
ngoja niipange safu, injili nakufikishia
Shairi la kiinjili, kaburunye nalileta

maandiko nimesoma, kitabu cha biblia
kimesheeni hekima, mi nakuhakikishia
Neno ukiliandama, shida lakuondolea
Injili uweza wa Mungu, uuletao wokovu


Neno la Mungu jamani, mambo yake ni hakika
shuhuda limesheheni, tena halina dhihaka
yaani laleta imani, maandiko ukishika
Injili uweza wa Mungu, uuletao wokovu

Siwezi kulikataa, limeosha dhambi zangu
Neno la Mungu ni taa, na mwanga wa njia yangu
Acheni kunishangaa, hebu mwaminini Mungu
Injili uweza wa Mungu, uuletao wokovu

Neno laleta amani, moyoni ukiliweka
wewe unangoja nini, ili upate pumzika
fanya uamuzi makini, na mbinguni utafika
Injili uweza wa Mungu, uuletao wokovu

Asante Sana Mpendwa... Mungu Akubariki...
 
Back
Top Bottom