Miss Zomboko
JF-Expert Member
- May 18, 2014
- 4,599
- 9,532
IKIWA leo ni mwisho wa kusajili laini za simu, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema kuwa fedha za Watanzania ambao laini zao za simu zitafungwa, zitakuwa salama kwa muda wa miezi mitatu.
Baada ya hapo iwapo watashindwa kufungua laini zao za simu, wateja hao watalazimika kwenda kwa kampuni za simu kuomba kurejeshewa fedha zao.
Wakati TCRA ikieleza hayo, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeshasajili asilimia 85 ya Watanzania walioomba kupewa kitambulisho cha taifa tangu kazi hiyo ianze mwaka 2011.
Ofisa Mwandamizi Mkuu wa TCRA, Semu Mwakyanjala, anapeleka ujumbe kwa Watanzania ambao wanamiliki laini za simu zinazofikia jumla ya milioni 21.4 ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole na zitazimwa leo, wawe na uhakika kuwa fedha zao zitakazokuwa kwenye laini hizo, zitakuwa salama kwa muda wa miezi mitatu.
Kwa mujibu wa Mwakyanjala, baada ya miezi mitatu, mmiliki wa laini ambaye atakuwa amehifadhi fedha kwenye laini iliyofungwa na hakufanikiwa kuirejesha laini yake ndani ya kipindi hicho, atatakiwa kuwasiliana na watoa huduma yaani kampuni ya simu husika.
TCRA imewataka wananchi ambao wamekamilisha usajili wa laini zao kwa alama za vidole na wale ambao hawajakamilisha, kuhakikisha wanazingatia matumizi bora ya mitandao au simu, kutumia mitandao kujenga umoja, mshikamano na utengamano wa nchi, kutumia fursa za kiuchumi zilizopo ili kuboresha maisha pamoja na kuepuka wizi, uchochezi, upotoshaji na utapeli mtandaoni.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2012, Tanzania ina jumla ya watu milioni 44.9 ambapo kwa sasa idadi hiyo inaweza kuwa zaidi ya milioni 50.
Wakati NIDA ikisema kuwa imeshasajili asilimia 85 ya Watanzania, TCRA imesema idadi ya laini zilizosajiliwa ni milioni 48.7, huku laini zilizosajiliwa kwa alama za vidole mpaka sasa ni milioni 27.3 sawa na asilimia 56 na zile ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole ni milioni 21.4 sawa na asilimia 44.
Kwa upande wake Meneja Usajili na Utambuzi wa NIDA, Julien Mafuru alisema kazi ya usajili kwa ajili ya vitambulisho vya taifa pia inawahusu rai wa kigeni wanaofanya kazi hapa nchini.
Alisema usajili kwa Watanzania ni bure lakini raia wa kigeni wanalipia huduma hiyo kati ya Dola za Marekani 20, 50 na 100 kutegemea na shughuli ambayo mhusika anaifanya hapa nchini.
Mafuru alisema wageni wanasajiliwa kwenye ofisi za NIDA wakiwa na nyaraka muhimu na mwitikio kwa upande wao pia ni mzuri.
“Changamoto tunayokutana nayo mara nyingi ni wananchi kubadilisha majina, utakuta mtu alijisajili mwaka 2012 kwa jina la Asha, leo anakuja anasema anaitwa Amina, lakini wengine wanakuja wakiwa hawana nyaraka na wakielekezwa wanakuwa wabishi, kwa hiyo ni vizuri wananchi wakatunza nyaraka zao zote bila kujali umri kama ni kijana au mzee,”alisema Mafuru.
Meneja Biashara wa Kanda wa Kampuni ya Simu ya Airtel, Mussa Sultan, alisema fedha zitakazokuwa kwenye laini zitakazofungwa za wateja wao hazipotei kwa kuwa laini ni mali ya mteja.
Sultan alisema laini ambazo zitafungwa zilikuwa zimeshasajiliwa mwanzoni kabla ya usajili wa alama za vidole haujaja, hivyo wateja ambao watakuwa hawajakamilisha usajili huo na endapo kuna fedha kwenye laini zao, wasiwe na hofu kwa kuwa zitakuwa salama na watakapokuwa wamesajili kwa alama za vidole watazikuta fedha zao ziko salama.
Katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kufanikisha usajili kwa alama za vidole, Kituo cha Utangazaji cha EFM kiliandaa tamasha kubwa la muziki kwenye Viwanja vya Zakhem Mbagala jijini Dar es Salaam.
Mratibu Miradi wa EFM Radio, Mack Mwinshaha, alisema tamasha hilo ni sehemu ya kampeni yao waliyoipa jina la ‘Maisha Kidole’ ili kuwahamasisha wananchi kujitokeza kujisajili ili kupata kitambulisho cha taifa, kusajili laini kwa alama za vidole na kupata cheti cha kuzaliwa.
“Maisha ni kidole maana yake ni kwamba maisha ya mtanzania kwa sasa yameunganishwa kwa karibu na matumizi ya simu za mkononi ikiwemo kununua umeme, kulipia bili za maji, ardhi, malipo ya chuo na huduma nyingine nyingi,”alisema Mwinshaha.
Kutoka Mkoani Dodoma, Wakazi wa jiji hilo na viunga vyake wamejitokeza kwawingi kuwahi siku hiyo iliyobaki ili kusajili laini zao.
HabariLEO ilitembelea Viwanja wa Nyerere na kushuhudia mamia ya watu wakiwa kwenye misururu mirefu wakiwa na fomu mikononi tayari kutambuliwa kama raia na Uhamiaji na kuingia banda la Nida kupata namba za vitambulisho.
Wananchi hao wameitikia mwito wa Rais John Magufuli aliyeongeza muda hadi Januari 20, mwaka huu ambao aliahidi kwamba baada ya hapo TCRA inatakiwa kuzima simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole.
Katika mahojiano na HabariLEO wengi waliomba serikali iwafikie kuongeza muda walau hadi mwishoni mwa mwezi huu ili kuwapa nafasi wananchi wengi hasa wa vijijini ambao wanatakiwa kufuata huduma ya kusajili laini mijini hasa wilayani.
Akiwa kwenye foleni, Jumanne John (66) aliomba serikali ifikirie kuongeza hadi Januari 31, mwaka huu, kutokana watu wengi hasa vijijini kutosajili laini za simu na hivyo watapoteza mawasiliano na fedha ambazo wanaziweka kwenye simu.
Mariam Hamisi (68) aliwaomba Nida kutoa namba za vitambulisho kwa haraka, ili kuepusha usumbufu wa wananchi kutoka katika maeneo ambayo wametoa vitambulisho lakini wengi wao bado.
Mariam aliomba serikali kuongeza muda hadi Januari 31 mwaka huu, ili kuwapa muda wa kutosha wananchi waliosubiri siku za mwisho na bado wapo kwenye misururu mirefu wakitaka kujisajili liini.
Mwinyijuma Omari (56) alisema kwa siku moja iliyobaki Nida wanatakiwa kuongeza nguvu kazi na vitendea kazi ili kukamilisha usajili.
Akizungumza Ofisa Usajili kutoka Nida, Grace Msaki amesema wamejipanga na kuhakikisha siku moja iliyopo wanaitumia vizuri kuhakikisha wananchi waliopo kwenye misururu wanapata huduma ya kupata namba za vitambulisho.