Rostam: Siwajui Richmond
na Mwandishi Wetu
1. MFANYABIASHARA na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM), amesema hana uhusiano wowote, na wala haijui Kampuni ya Richmond Development Company LLC ambayo ilishinda zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura baada ya kuingia mkataba wenye utata na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
2. Rostam aliyepata kuwa Mweka Hazina wa CCM Taifa hadi mwaka ujana, alitoa kauli ya kuikana Richmond jana, wakati alipofanya mahojiano ya simu na Tanzania Daima, alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa kinachosababisha jina lake lihusishwe na kampuni hiyo ya kitapeli na ile ya Dowans ambayo ilirithi mkataba wa Richmond.
3. Siijui hata kidogo, siwatambui na siwafahamu. Mimi ni mfanyabiashara, sina sababu ya kuficha, kama ingekuwa ni kampuni yangu, nisingeshindwa kutekeleza mradi huo. Leo hii kutokana na kuwepo kwa mawasiliano ya kutosha, si rahisi mmiliki wa kampuni hiyo asijulikane. Mimi sidhani kama imekuwa ni ngumu kiasi hicho, alisema Rostam.
4. Wakati akikana kuifahamu Richmond na wamiliki wake, Rostam, alikiri kuwahi kutaka kufanya kazi na Kampuni ya Dowans Holdings S.A ambako Kampuni ya Richmond ililazimika kuhamishia mkataba wake huko, baada ya kushindwa kuutekeleza kwa muda uliowekwa. Mimi ni mkandarasi. Nina kampuni inaitwa Caspian. Sina uhusiano na Dowans ingawa niliomba kupatiwa kazi ya ukandarasi, alisema Rostam.
5. Matamshi haya ya Rostam yanatokana na shaka iliyojitokeza baada ya Kamati Teule ya Bunge kueleza katika ripoti yake kwamba, iligundua kuwa Dowans iliwahi kutumia anwani ya barua pepe ya Kampuni ya Caspian Construction Ltd inayomilikiwa na mfanyabiashara na mwanasiasa huyo.
6. Akifafanua kuhusu hilo, Rostam alisema alilazimika kuacha anuani yake kwa Dowans baada ya kuomba kazi kwa kampuni hiyo.Nilipoomba kazi kama mkandarasi, nilitakiwa kuacha anuani, unapoomba kazi lazima uache anuani, alisema kwa ufupi.
7. Akizungumza kuhusu kauli ya Kamati Teule ya Bunge kuwa alikwepa wito wa kwenda kuhojiwa juu ya anwani ya kampuni yake kutumiwa na Dowans, na pia baadhi ya wafanyakazi wa kampuni yake kusemekana kuwa wafanyakazi wa Dowans pia, alisema barua hiyo ya wito ilichelewa kumfikia.
8. Alipoulizwa kuhusu ushahidi uliotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salvatory Rweyemamu kuwa yeye ndiye aliyemuunganisha na Mkurugenzi wa Richmond, Mohammed Gire kufanya kazi ya ushauri wa habari katika kampuni hiyo, Rostam alikana kwa kusema kuwa, alichowahi kufanya ni kumuunganisha kufanya kazi kama hiyo kwa kampuni ya uwakala wa kupakua mizigo bandarini.