Wakuu, tukio hili ni la kweli?
- Tunachokijua
- Agosti 7, 1974 katika hali isiyotarajiwa mwanasanaa wa sanaa ya kutembea juu ya kamba alifanya tukio la kustaajabisha lenye hatari ya kifo na kuitwa “uhalifu wa kisanaa’. Mwanasanaa huyo alifahamika kwa jina la Philippe Petit kutoka nchini Ufaransa.
Phillipe aliandika historia alipofanikiwa kutembea juu ya waya uliounganisha Minara Pacha ya World Trade Center jijini New York, futi 1.350 kutoka ardhini. Alitumia takribani dakika 45 kuonesha ustadi wake wa kutembea juu ya kamba.
Alienda na kurudi kutoka mnara mmoja hadi mwingine mara nane, akiruka, kucheza, kupiga magoti na hata kulala juu ya waya huo jambo liliwashangaza maelfu ya watu kumshangilia kutokea chini.
Mpango ulipoanzia
Phillipe alitekeleza tukio hilo akiwa na umri wa miaka 24, lakini mpango aliuanza miaka sita nyuma alipokuwa na umri wa miaka 18 tu akiwa nchini kwao Ufaransa. Anaeleza kuwa alianza kutembea juu ya kamba akiwa na umri wa miaka 16, lakini familia yake haikumuunga mkono wala kumuelewa anachokifanya.
Siku moja alipoenda kumuona daktari wa meno ndipo alipoona kijarida kilichokuwa kikieleza kuhusu ujenzi wa minara hiyo ambayo ingekuwa mirefu zaidi duniani kwa wakati huo na ndipo wazo la kwenda kufanya sanaa katika eneo hilo lilipomjia.
Hakukamilisha mpango huo peke yake bali kwa kushirikiana na wenzake alioshirikiana nayo kwenye kufunga waya huo kutoka mnara mmoja hadi mwingine usiku wa tarehe 6, Agosti 1974.
Kukamatwa na polisi
Siku ya tukio polisi walifika na kumtaka ashuke kwenye waya huo lasivyo wataukata lakini mwenyewe aliendelea hadi alipoona imetosha akashuka na kukamatwa na polisi hao kwa kosa la kuvunja sheria za jiji hilo na kuhatarisha maisha.
"Nilipopiga hatua yangu ya mwisho na kujisalimisha kwa polisi, mvua ilianza kunyesha. Walikuwa na hasira sana. Iliwachukua mchana mzima kunifanyia taratibu za kipolisi na kuniachia. Walikuwa wakali, lakini baadhi yao waliniomba saini yangu,"
Hukumu
Jambo la kufurahisha ni kuwa, mashtaka yake yalifutwa baada ya kukubali kufanya onesho la bure kwa watoto katika Central Park.
Picha za Petit akitembea juu ya waya kati ya Minara Pacha zilisambaa duniani kote na kutawala kurasa za mbele za magazeti mengi. Onesho hilo la kipekee lilimfanya aingie kwenye historia kama mmoja wa wasanii jasiri na wabunifu zaidi kuwahi kushuhudiwa.
Filamu
Mwaka 2015, iliachiwa filamu yenye jina la The Walk kuonesha kisa hicho na namna kilivyotokea.