Yoda,
PICHA ZA BI. TITI MOHAMED KUTOKA BUKOBA 1962
Nimepokea picha mbili kutoka Bukoba kwa kaka na rafiki yangu Ramadhani Kingi.
Kingi kaeleza hapa jamvini masikitiko yake kuhusu yale yaliyowafika Ali Migeyo na Bi. Titi.
Nitamweleza Ali Migeyo kwa muhtasari tu na sitatia neno langu nitamleta hapa barzani Dr. Michael Lugazia mumsikilize.
Hii ni miaka ya mwanzoni 1950 wakati wa TAA bado haijaundwa TANU:
''Ukitazama mwelekeo wa siasa na mazingira ya wakati ule, uongozi wa wazee katika TAA, kwa hali yao na kutokana na mambo yaliyokuwa yakiwakabili, walikuwa hawana uwezo wa kukabiliana na changamoto ya ukoloni.
Lakini pamoja na yote hayo, wazee hawakutaka kuachilia madaraka. Jambo hili lilizusha mvutano baina ya wazee na wanasiasa vijana waliosomeshwa na himaya ya Waingereza.
Vijana hawa walikuwa akina Abdulwahid na Ally Sykes, Tewa Said Tewa, Stephen Mhando, Dossa Aziz, James Mkande, na wale madaktari watano - Joseph Mutahangarwa, Luciano Tsere, Michael Lugazia, Vedasto Kyaruzi na wengineo. Haya yalikuwa ni mapambano baina ya kizazi kipya na kile cha kale.''
Hii ni bashraf kutoka kitabu cha Abdul Sykes.
Sasa msome Dr. Lugazia akiandika kutoka Makao Makuu ya TAA New Street:
''Dr Lugazia alikuwa anatoka Bukoba, alitaka kuhakikisha kuwa viongozi wa TAA kutoka nyumbani kwao hawapitwi na mkutano ule muhimu wa kuunda TANU.
Dr Lugazia alichukua juhudi za makusudi kupeleka rasimu ya katiba ya TANU kwa tawi la Bukoba.
Lakini baada ya kukamatwa kwa Migeyo, TAA ilikuwa imepoteza uhai wake. Hakuna mtu aliyeweza kuwasha tena moto aliouwasha Migeyo.
Barua muhimu ya mwaliko iliyoandikiwa TAA Bukoba na Dr Lugazia ikiambatanisha katiba ya TANU ambayo ilitakiwa kujadiliwa katika mkutano uliokuwa uitishwe Dar es Salaam haikushughulikiwa.
Hii ndiyo sababu katika mkutano wa kuasisi TANU mwaka 1954 Bukoba haikuwakilishwa.''
Bukoba haikuwakilishwa kwa kuwa Ali Migeyo alipigwa mabomu na wakoloni, akakamatwa akashitakiwa na kufungwa jela Butimba.
Uhuru ukapatikana mwaka wa 1961.
Mwaka wa 1965 Migeyo akakamatwa na kufungwa Jela ya Ukonga na serikali aliyopiginia yeye mwenyewe kwa damu na jasho lake kuiweka madarakani.
PICHA 1:
Viongozi wa akina Mama wa TANU kutoka kulia walioketi Mama Boi, Bibi Titi Mohammed na Bint Farahani. Waliosimama kutoka kulia Bint Kaijage, Bint Sheikh na Madanganyo Bint Saliboko Bukoba Mjini 1962.
PICHA 2:
Baraza la wazee wa TANU Bukoba na Bibi Titi walioketi kutoka kulia Maalim Idd Kombo kampakata mwanawe, Bibi Titi Mohammed, Mzee Ali Migeyo Waliosimama kutoka kulia Shaaban Mserengeto, Mzee Ali Kagire, Juma Mwanandege, jina ninesahau, koti jeusi RAJABU Kasheijege, jina nimesahau, Bint Mwanandege, Maalim Majuto Lubangula, Jaafary Rwabyo mbele ya Jaafary ni Amri Babakas, mwisho jina nimesahau.
(Maelezo na picha kutoka kwa Ramadhani Kingi).