Kambiko,
Unasema maneno hayo kwa kuwa wewe huijui historia ya uhuru wa Tanganyika.
Mimi nitakueleza kwa ufupi.
Baada ya Abdul Sykes na Dr. Vedasto Kyaruzi kuchukua uongozi wa TAA mwaka wa 1950 juhudi za kuunda chama cha siasa zikaanza kwa nguvu sana.
Serikali iliomba mapendekezo ya katiba kutoka kwa wananchi na vyama vyao.
Mapendekezo ya TAA HQ ilikuwa katika moja ya vipingele vyake kutaka wajumbe wa LEGCO wapigiwe kura badala ya kuteuliwa na Gavana na baada ya miaka 13 Waingereza waondoke Tanganyika.
Kipengele hiki kilighadhibisha sana serikali.
Mapendekezo haya yalitengenezwa na TAA Political Subcommitee ambayo wajumbe wake walikuwa: Dr. Vedasto Kyaruzi, Abdul Sykes, Mufti Sheikh Hassan bin Ameir, Hamza Mwapachu, Steven Mhando, Sheikh Said Chaurembo na John Rupia.
Mshauri wa TAA Political Subcommitte alikuwa Earle Seaton.
Dr. Kyaruzi kama adhabu akapewa uhamisho kwenda Kingolwira kisha Nzega kwa nia ya kuidhoofisha TAA na sababu ni hayo mapendekezo ya katiba ambayo TAA HQ waliwasilisha kwa Gavana Edward Twining.
Hamza Mwapachu akahamishiwa Nansio, kisiwani.
TAA HQ akabaki Abdul Sykes akiwa Secretary na Act. President.
Abdul Sykes na Hamza Mwapachu wakaamua katika kikao kilichofanyika Nansio nyumbani kwa Hamza Mwapachu kuwa TAA isisubiri waunde TANU haraka.
Hii ilikuwa 1950/51.
Abdul alikuwa anamtaka Chief David Kidaha Makwaia awe Rais wa TAA kisha waunde TANU mwaka unaofuatia.
Hili halikuwezekana.
Mwaka wa 1952 Nyerere akaja Dar es Salaam na akajuana na Abdul Sykes.
1953 Abdul Sykes na Ali Mwinyi Tambwe wakaenda Nansio kutaka ushauri wa Mwapachu kuhusu nafasi ya Rais wa TAA katika uchaguzi uliokuwa mbele yao.
Mwapachu alikuwa akimtaka Nyerere atiwe katika uongozi wa TAA.
Mwapachu yeye alikuwa anamtaka Nyerere ashike nafasi ya President.
Abdul Sykes alikwenda kwa Mwapachu kupata kauli yake ya mwisho kuwa yeye (Abdul) ampishe Nyerere nafasi ile na amsaidie ashinde uchaguzi awe Rais na mwaka unaofuatia 1954 waunde TANU na Nyerere aongoze harakati za kudai uhuru.
Nyerere bila ya msaada wa Abdul Sykes na viongozi wa TAA HQ asingeweza kiumshinda Abdul Sykes katika uchaguzi katika Dar es Salaam ile ya 1950s.
Mwapachu alisisitiza kuwa nafasi ya Rais wa TAA kwenda TANU na kudai uhuru inahitaji Mkristo ile kuvunja ile dhana kuwa harakati za TAA na TANU itakapoundwa zisichukuliwe kuwa ni harakati za Waislam peke yao.
Waasisi wa harakati hizi walijua kuwa endapo harakati hizi zitapewa sura ya Uislam hii itawaweka Wakristo nje ya ulingo na Waingereza wangepata mwanya ya kuwagawa Watanganyika.
Hili halikutakiwa kabisa.
Nyakati hizo Waislam ndiyo waliokuwa mstari wa mbele katika kupambana na ukoloni wa Waingereza.
Hawa waasisi wa harakati hizi hawakuwa watu wajinga walijua fitna za wakoloni na walijua faida ya umoja wa wananchi.
Hata siku moja hawakuwaza kuleta ubaguzi.
Historia hii ukiitaka kwa ukamilifu wake nimeandika kitabu hicho hapo chini.
Chukua muda ukisome ndiyo utawajua Waislam na ukweli wa historia yao.
Laiti wangelikuwa wabaguzi Nyerere asingefika hapo alipofika.
Lakini kubwa utajua kwa nini wewe hukusomeshwaa historia hii mahali popote.