Tarehe 29 Mei, 2025 Chama Cha Mapinduzi
CCM kilifanya
mkutano mkuu jijini Dodoma, ukiongozwa na mwenyekiti wake Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mkutano huo ulihudhuriwa na wanachama wa CCM kutoka maeneo mbalimbali nchini ambapo chama kilipitisha marekebisho matatu kwenye Katiba ya chama chao ikiwemo vikao vya chama kufanyika kwa njia ya mtandao.
Kabla ya mkutano huo Tarehe 24 Mei, 2025 Askofu Josephat Gwajima Mbunge wa Kawe kupitia CCM alifanya
mkutano na waandishi wa habari ambapo alisema kumekuwa na mlolongo wa matukio ya watu kutekwa pamoja na kupotea hivyo kutokana na hayo, aliamua kuitisha mkutano na waandishi wa habari kuongelea kuhusu suala hilo na kisha kutoa ushauri wake wa namna ya kutatua changamoto hiyo.
Kupitia mtandao wa X ipo Picha ya Gwajima inayosambazwa ikidaiwa kuwa ni kutoka mkutano mkuu wa CCM Dodoma, Mei, 29 2025 na kwamba chama chake kimesusia kuchapisha picha hiyo mtandaoni kutokana na ukosoaji wa Gwajima dhidi ya matukio ya utekeji.
Je, ni upi uhalisia wa picha hiyo?
Kwa kutumia Google reverse image search, JamiiCheck imejiridhisha kuwa picha hiyo si ya mwaka 2025.
Aidha picha hiyo ilitumika kuelekea uchaguzi mkuu 2020, ambapo
Millard Ayo aliichapisha katika mtandao wa X Julai 21, 2020 katika tukio la kuhesabu kura za maoni watia nia wa ubunge CCM jimbo la Kawe Dar es salaam.
Aidha
Mwanahalisi ilitumia picha hiyo mnamo Agosti 20, 2020 ikieleza kuteuliwa kwa Askofu Gwajima na CCM, kugombea Ubunge jimbo la Kawe, Dar es Salaam.
Hivyo kuitumia na kueleza kuwa picha hiyo ni ya mwaka 2025 ni kupotosha uhalisia.