Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam.
Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itaendelea kuimarisha mazingira yanayowezesha maendeleo ya sekta ya lojistiki, usafirishaji na elimu ya ufundi ili kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, akisisitiza kuwa sekta hizo ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi.
View attachment 3641734
Dk. Nchemba aliyasema hayo Alhamisi, Julai 30, 2026, alipomwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Mwaka la Chama cha Wataalamu wa Lojistiki na Usafirishaji Tanzania (CILT), lililofanyika katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Mabibo, jijini Dar es Salaam.
Katika kongamano hilo, Dk. Nchemba alijibu ombi lililotolewa na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dk. Prosper Mgaya, kuhusu changamoto ya ukosefu wa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma kozi za muda mfupi za ufundi.
Alisema Serikali imelipokea ombi hilo kwa uzito mkubwa, akibainisha kuwa taaluma za ufundi na lojistiki ni miongoni mwa sekta muhimu katika kufanikisha maendeleo ya taifa.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kutafuta mbinu mbadala za kuweka mfumo rafiki utakaowawezesha wanafunzi wa kozi hizo kupata fursa ya masomo ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.
Aidha, Dk. Nchemba alitolea mfano wa mfumo wa Samia Scholarship, ambao umeendelea kuzingatia ufaulu na uwezo wa kitaaluma zaidi kuliko kigezo cha umaskini pekee, akisema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu ya ufundi nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), David Kafulila, alisema mfumo wa ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) si jambo la hiari wala la kinadharia, bali ni mkakati wa makusudi wa kimfumo unaolenga kuikomboa nchi kiuchumi na kuongeza ufanisi wa utendaji katika sekta mbalimbali.
Akifafanua umuhimu wa mfumo huo, Kafulila alisema mataifa mengi duniani yanaendelea kutumia mfumo wa PPP kwa sababu kuu tatu ambazo ni kuvutia mitaji kutoka sekta binafsi, kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya kisasa na kuongeza ufanisi wa usimamizi.
Alisisitiza kuwa uchumi wa dunia wa sasa unategemea zaidi maarifa, ujuzi na ubunifu kuliko rasilimali za asili pekee.
View attachment 3642061
Kafulila aliongeza kuwa Serikali haiwezi kubeba jukumu la kujenga kila aina ya miundombinu na wakati huo huo ikawa na rasilimali za kutosha kuwekeza katika maendeleo ya watu.
View attachment 3642124
Alieleza kuwa kupitia mfumo wa PPP, Serikali inapata fursa ya kushirikisha sekta binafsi katika uwekezaji wa miradi ya maendeleo na biashara, hatua inayowezesha kuelekeza rasilimali nyingi zaidi katika sekta za kijamii hususan elimu, afya na maendeleo ya rasilimali watu.
View attachment 3642125
Kongamano hilo limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wataalamu, wasomi, viongozi wa Serikali na wadau wa sekta ya usafirishaji na lojistiki kujadili namna bora ya kuimarisha sekta hiyo na mchango wake katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo na ukuaji wa uchumi wa Tanzania katika kipindi cha miaka 25 ijayo.
===