Ndahani,
Sehemu katika Waraka wa Shura ya Maimamu Uchaguzi Mkuu 2020:
WAISLAMU TUNATAKA HAKI NA USAWA
Hapo nyuma tumezungumza kama Watanzania. Maelezo yetu yamejadili na kupigania maslahi ya Taifa na Watanzania kwa ujumla. Lakini pia sisi ni Waislamu na kama yalivyo makundi mengine ya kijamii tunao wajibu wa kutafakari, kujitazama na kutazamwa kwa maslahi yetu. Waislamu wanatambua kuwa siasa ni sehemu muhimu ya maisha yao na hawawezi kujitenga na siasa. Kwasababu hiyo wanaelewa mfumo wa siasa usio wa haki na usawa unaweza kuathiri ustawi wa maisha yao ya kila siku kidini, kijamii, kiuchumi, kiusalama, kiutamaduni na kadhalika.
Tunaweza kusema siasa inanafasi kubwa katika mustakbali wa ustawi wao. Waislamu tumeshiriki ipasavyo chaguzi za nyuma ukiwemo uliounda serikali iliopo madarakani. Lengo likiwa ni kushiriki katika ujenzi wa Taifa bora, huru na lenye maendeleo. Taifa la wote linalotenda Haki, Usawa na Uadilifu kwa wote. Tukitaraji tuwe na Uongozi wa nchi unaowatendea haki wananchi wote bila ubaguzi wa Kidini, Kikabila, Jinsia, Rangi au eneo analotoka mtu.
Mpaka sasa Waislamu wameshindwa kuona nafuu yao katika matokeo ya siasa hizo. Hawaoni nafuu katika Uhuru wa kuabudu, Uhuru wa Kujiamulia mambo yao wenyewe (hata yale ya kidini), Usalama wa Viongozi wao, Madrasa zao, Misikiti na Watu wao. Hawaoni usawa wowote katika madaraka na ajira za serikali. Mfumo wa Elimu wa Taifa hautoi fursa sawa wala kutenda haki kwa wote. Orodha ya viashiria vya tatizo hilo ni kubwa mno lakini tunaweza kupitia hivi vichache:
Uadilifu I
Januari 11, 2019, serikali ilifanya uhamisho mkubwa wa kushitukiza kwa wahadhiri na watumishi wandamizi katika Chuo Kikuu cha Serikali cha Dodoma-UDOM. Waliohamishwa walikuwa 11, lakini wote walikuwa Waislamu: Dk. Maryam Khamis (Director of Graduate Studies), Dk. Ibun Kombo (Political Science), Dk. Mwinyikombo Amir (Mwalimu wa Udaktari wa Binadamu), Dk. Yusuf Kambuga (College of Education), Dk. Masoud Masoud (Informatics) , Bw. Subira Sawasawa (Mkurugenzi Mkuu Rasilimali Watu), Bw. Mohamed Mwandege (Bursar/Mhasibu Mkuu), Bi. Aziza Gendo (Seniour Estate Oficer), Bw. Simba Omary (Senior Supplies Oficer), Bw. Wema Mbegu (Legal Oficer), Bw. Khamis Mkanachi (Mwalimu wa Idara ya Historia).
Barua zao za uhamisho hazikuonesha makosa katika utendaji wao wa kazi au uongozi. Pamoja na kutokuwa wakosaji, uhamisho wao uliambatana na udhalilishaji mkubwa, kunyimwa haki stahiki za uhamisho, kuhamishiwa katika nafasi za chini kinyume na hadhi zao.
Baada ya uhamisho huo, Serikali ilifanya uteuzi mwingine katika chuo hicho hicho cha Serikali. Katika uteuzi huo walioteuliwa walikuwa 11, wote Wakristo: Prof. Leonard James Mselle, Prof. Adam B. Swebe Mwakalobo, Prof. Julius William Nyahongo, Prof. Justin Ntalikwa, Prof. Frowing Paul Nyoni, Prof. Odass Bilame, Prof. Ainory Piter Gasese, Dkt. Victor George Mareale, Dkt. Alex Shayo, Dkt. Calvin Swai, Dkt. Augustine Mwakipesile.
Kuhamisha wahadhiri 11, katika Chuo Kikuu si jambo dogo. Vilevile kuhamisha Wahadhiri 11, wa dini moja (Waislamu) katika Chuo Kikuu ukaingiza wahadhiri 11 wa dini moja (Wakristo), na hao Waislamu 11, baadhi yao ukawatoa kabisa katika mfumo wa elimu kwa kuwapeleka sekta nyingine na zisizo lingana na hadhi zao si jambo dogo. Wala si hatua ya kitaalamu ya kuboresha mfumo wa Elimu wa Taifa. Na wala si hatua ya kijinga bali ya werevu uliofurutu ada dhidi ya maslahi ya Taifa. Hatuwa hiyo ni salamu nzito kwa jamii yao na Taifa kwa ujumla. (Ndio maana katika maoni yetu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tulipendekeza Katiba Mpya imtambuwa Mwenyezi Mungu na Dini liwe suala rasmi na la wazi katika uendeshaji wa nchi).
Uadilifu II
Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani Mwaka (2015), Rais alifanya uteuzi wa Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Wilaya na Wakurugenzi mbalimbali. Uteuzi wake ulikuwa kama ifuatavyo:
Mawaziri na Manaibu: 30.
Waislamu 10, sawa na asilimia 33%.
Wakristo 20, sawa na asilimia 67%.
Makatibu Wakuu na Manaibu: 50.
Waislamu 10, sawa na asilimia 20%.
Wakristo 40, sawa na asilimia 80%.
Wakuu wa Mikoa na Wilaya: 166.
Waislamu 41, sawa na asilimia 25%.
Wakristo 125, sawa na asilimia 75%.
Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya: 163.
Waislamu 24, sawa na asilimia 15%.
Wakristo 139, sawa na asilimia 85%.
Wakurugenzi mbalimbali: 249.
Waislamu 45, sawa na asilimia 18%.
Wakristo 204, sawa na asilimia 82%.
Manaibu Kamishna wa Polisi: 25.
Waislamu 5, sawa na asilimia 20%.
Wakristo 20, sawa na asilimia 80%.
Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi: 33
Waislamu 7, sawa na asilimia 21%.
Wakristo 26, sawa na asilimia 79%.
Jumla Kuu ya Uteuzi:
Waislamu asilimia 20%.
Wakristo asilimia 80%.