Pinda asafisha nyumbani kwa JK
Thursday, 21 January 2010 07:21
*Amtimua mkurugenzi, mweka hazina Bagamoyo
*Ni kwa tuhuma za ubadhirifu, kutowajibika
Na Edgar Nazar, Bagamoyo
WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda amegeuka mbogo na kuwavua madaraka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mweka Hazina na maofisa wengine wa halmashauri hiyo kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za maendeleo ya umma na kushindwa kuwajibika ipasavyo.
Mbali ya hatua hiyo, Bw. Pinda alitoa onyo kuwa atakuwa mkali na asingependa kuona yaliyojitokeza katika halmshauri hiyo, ambayo ndio nyumbani kwa Rais Jakaya Kikwete, yakitokea kwingineko na kuwataka wakuu wa wilaya na mikoa kuzitizama halmashauri zao kwa jicho la karibu na kuwabana watendaji ambao wanaonekana kuwa walaji wa fedha za serikali.
Kama hiyo haitoshi, Bw. Pinda pia aliwaonya madiwani kuacha kupenda kuchukua posho kutoka kwa wakurugenzi wa halmashauri zao, hali ambayo inawafanya kuwa sehemu ya wakurugenzi na kushindwa kuwabana wanapoona kuwa wanakwenda kinyume, hivyo aliwataka kuwa wakali kama wabunge wanavyokua katika ukumbi wa bunge.
Hatua hizo za Bw. Pinda zilizoonekana jana alipokutana na viongozi na watendaji wa wilaya hiyo, zimetokana na mapendekezo ya ripoti ya uchunguzi uliofanywa Septemba na Oktoba mwaka jana na Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Serikali (CAG) uliobaini ukiukwaji mkubwa wa kanuni za fedha, uzembe na kushindwa kuwajibika na matokeo yake kuzorota kwa miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Watendaji walioshukiwa na Bw. Pinda ni pamoja na Bi. Rhoda Nsemwa (Mkurugenzi Mtendaji), Mweka hazina Bw, Carlo Wage, Mkaguzi wa Mahesabu wa Ndani, Bw, Abdul Mwinyi, Afisa Kilimo, Mifugo na Ushirika, Bw. Anaftal Remtulah pamoja na Ofisa Mipango, Bw. Aloyce Gabriel.
Akizungumza kwa ukali, Bw. Pinda alisema kuwa amechukizwa sana baada ya kupitia ripoti ya CAG na kugundua kuwa kuna matatizo katika kila kona, hali ambayo inaonesha wazi kuwa watendaji wakuu wa halmashauri wanahusika kwa kiasi kikubwa.
"Hawa watendaji ambao nimewavua madaraka kuanzia leo na saa hii, watachunguzwa na kama itathibitika kuwa na makosa ya jinai wanaweza kufukuzwa kazi au hata kupelekwa mahakamani na kushtakiwa au hata kushushwa vyeo walivyokuwa navyo kwa uzembe wa kutofuatilia shughuli za maendeo au kula fedha za serikali," alisema Bw. Pinda.
Watendaji wengine waliopitiwa na panga la Bw. Pinda ni pamoja na Mhandisi wa Ujenzi, Bw. Felix Ngomano, Mhandisi wa Maji, Bw. Galson Rafael ambaye ameondolewa katika nafasi hiyo na kubaki mtendaji wa kawaida baada ya kubainika kuwa hana sifa kushika nafasi hiyo.
Alisema kuwa baada ya kutokea kutokuelewana kati ya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Mugesa Mulongo na aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya, Bi. Rhoda Nsemwa juu ya kuwepo miradi hewa, serikali iliamua kuwaleta wakaguzi ili kujua ukweli ambao sasa umebainika wazi.
Alisema kuwa katika ripoti hiyo kumebainika mapungufu makubwa yanayotokana na uzembe wa ufuatiliaji wa masuala ya maendeleo ya watu wa Bagamoyo, Baraza la Madiwani kutokuwa na nguvu ya kuhoji masuala yanayohusu maendeleo ya wananchi wao, hali ambayo imesababisha kuwepo kwa ubadhirifu katika miradi mingi ya maendeleo.
Kwa upande wa Ofisa Elimu wa Wilaya ya Bagamoyo, Bi. Cheka Omar, yeye amewekwa chini ya usimamizi mkali na kama atabainika ameshindwa kazi kutokana na sekta ya elimu katika Wilaya ya Bagamoyo kuwa na matatizo makubwa naye atavuliwa madaraka aliyonayo.
Bw. Pinda alisema kuwa amewavua madaraka viongozi hao kuanzia jana kwa mujibu wa kanuni ya 37 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003 na watakuwa watendaji wa kawaida, huku wakiwa katika ukaguzi mkuu wa kuangalia kila sekta kama wataonekana kuwa wamefanya ubadhirifu wa makosa ya jinai sheria itafuata mkondo wake.
Bw. Pinda aliwataja watakaouchukua nafasi za watendaji walioondolewa kuwa ni Bw. Samuel Saiyanga kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya akitokea Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Vijijini, Bw. Fidelis Nenetwa atakuwa Mweka Hazina, akitokea Shinyanga.
Wengine walioteuliwa ni Fidelica Gabriel Myovelo, kutoka Wilaya ya Iringa ambaye atakuwa Ofisa Kilimo, Mifugo na Ushirika, Felista Chuki Masamba kuwa Mkaguzi wa Ndani kutoka Wilaya ya Lindi na Prudence Mtiganzi kuwa Mhandisi wa Maji kutoka Wilaya ya Kilombero, Ofisa Mipango mpya atakuwa Bw. Lucas Mweri kutoka Moshi.
Amesema kuwa watendaji hao wanatakiwa kufika mjini Bagamoyo haraka iwezekanavyo na kufanya shughuli za maendeleo kwa ufanisi kwani ana imani na watendaji hao hivyo, watafanya kazi zao kwa uadilifu mkubwa ili kuiendeleza Bagamoyo.
Gazeti hili lilipomfuata aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bi. Nsemwa alisema kuwa ameridhika na uamuzi huo na kushukuru, huku akisema kuwa angeweza hata kutolewa roho yake kwa kuwa alikuwa anasakamwa sana.
Kauli hiyo ilienda sambamba na ile ya aliyekuwa Mweka Hazina, Bw. Wage ambaye alidai ameridhishwa na maamuzi hayo, ambayo yanamfanya kuwa na amani sasa, bila kufafanua alikuwa akimaanisha nini.