Pinda alisema hayo jana bungeni mjini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo hapo kwa Waziri Mkuu, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ziwani Ali Said Salim (CUF), aliyetaka kujua mambo ambayo si ya Muungano yanaongozwa kupitia serikali gani, wakati kwa Zanzibar yanasimamiwa na Serikali ya Mapinduzi (SMZ).
Akijibu swali hilo, Pinda alisema serikali ya Tanganyika haipo na kwamba mambo yote yanayohusu shughuli zisizo za Muungano yanaongozwa na serikali ya Muungano.
Alisema mambo ambayo si ya Muungano kwa upande wa Zanzibar huongozwa na serikali ya Zanzibar, isipokuwa kwa upande wa Tanganyika mambo hayo huongozwa na serikali ya Muungano kwa kuwa Tanganyika haipo na hakuna serikali.
Kusema kweli mimi ningekuwa kama nabii na mtume Issa ningesema kuwa naam,hapo umenena kuwa serikali ya Tanganyika ilimezwa na serikali ya Muungano na ndivyo ilivyo kweli, alisema Pinda.
Waziri Mkuu alisema kuwa ndoto yake kubwa ni kuona kuwa siku moja kunakuwa na mfumo wa serikali moja na nchi moja kuliko ilivyo sasa ambapo kuna serikali mbili ndani ya nchi moja.
"Suluhu ya Muungano ni nchi moja na serikali moja, ndipo kelele zote zitakwisha,"alisema Pinda.