Josh Michael
JF-Expert Member
- Jun 12, 2009
- 2,523
- 87
- Asema Indonesia wanavaa batiki
SIKU moja tu baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutaka viongozi waandamizi waache kununua magari ya kifahari, jana alikuja na lingine jipya kwa kuwataka Watanzania kuachana na vazi la suti akisema kuwa lina gharama kubwa na halifai kwa wananchi maskini.
Pinda ambaye juzi alikaririwa akisema kuwa ni lazima nchi ibane matumizi kwa magari ya bei ndogo, jana alisema suti wanazovaa Watanzania ni za gharama kubwa ukilinganisha na kipato cha Mtanzania wa kawaida.
Aliyasema hayo wakati akifunga mkutano wa siku tatu uliofanyika katika ukumbi wa St Gasper nje kidogo ya mji wa Dodoma, ambako alikuwa mwenyekiti kwa siku zote walipojadili masuala ya mifugo nchini.
Tazameni hata nchi ya Indonesia, juzi juzi nilikuwa huko ilinibidi hata mimi na msafara wangu tuache suti zetu na tuvae mashati ya batiki ya yaliyoshonwa kwa kutumia kitambaa cha nchi hiyo, ili tuweze kuonana na rais wao ambaye pia tulimkuta akiwa katika vazi la shati la kawaida kabisa hivi sisi Watanzania kwa nini tunapenda vitu vya kuiga?" aliuliza Pinda.
Waziri Mkuu alisema kama Watanzania wataamka na kufikiria kuwa wapo Watanzania wenzao ambao wanaishi bila ya kupata hata dola moja, hawatakumbuka kuvaa hizo suti ambazo alisema sio vazi la lazima sana kwa watu maskini kama Tanzania.
Pamoja na magari ya kifahari, lakini pia kuna hili suala la kuvaa suti, hivi kwa nini tusiige hata mfano wa Hayati baba wa Taifa kuwa alikuwa akivaa mavazi ya kawaida kabisa, lakini hakuweza kupoteza heshima yake ya Urais, alisema Pinda.
Juzi baada ya kutamka kuwa magari ya kifahari hayafai na iko siku atatangaza kupigwa marufuku na kusisitiza kwamba magari ya serikali yatakuwa aina ya Land Cruiser (Hard Top), baadhi ya wadau walianza kutoa maoni yao wakisema kuwa kiongozi huyo alitakiwa kutamka rasmi ni lini serikali itaachana na mashangingi.
Hata hivyo baada ya kusikia maoni hayo, Waziri Mkuu ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa Serikali jana alisema katika bunge la bajeti lijalo kutakuwa na kazi moja tu ya kupitisha bajeti ya kununua magari ya bei nafuu bila ya kutaja ni aina gani ya magari yatakayonunuliwa.
Kama alivyofanya juzi kwa kutolea mfano wa nchi ya India ambayo alisema kuwa imebana matumizi ya magari ya kifahari, jana alitoa mfano wa nchi ya Indonesia ambako alisema hata vazi la Taifa ni nguo iliyoshonwa na batiki ya nchi hiyo.
Wakati huo aliwatahadharisha wakurugenzi na viongozi wa wilaya ambao wanapenda kukaa maofisini muda wote bila ya kwenda vijijini kukagua shughuli za maendeleo ambapo alisema jicho lake litawamulika watu hao na hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika na makosa.
Alisema umezuka mtindo wa baadhi ya viongozi katika halmashauri ambao wanatumia muda mwingi kukaa ofisini na kupulizwa na viyoyozi ili hali maisha ya Watanzania huko vijijini yanakuwa ni ya hatari na wanategemea msaada wao.
Katika mkutano huo kulikuwa na maazimio 11 ambayo aliagiza utekelezaji wake uanze kabla ya kumalizika kwa mwezi Oktoba na akamtaka Waziri wa Mifugo na Uvuvi, John Magufuli kuendelea na kasi aliyonayo na kwamba yeye Pinda atakuwa nyuma yake akimuunga mkono.
Huku akiyasema hayo, ziara iliyofanywa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa Septemba, 2007 katika mataifa hayo ya mashariki ya mbali ilizaa wazo lililoisukuma serikali kutaka kuleta wataalamu kutoka Thailand kwa ajili ya kutengeneza mvua, maarufu kama 'Mvua ya Lowassa'.
Hata hivyo, mpango huo ulivurugika wiki chache baada ya Lowassa kurejea nchini, kufutia mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Serikali ya Waziri Mkuu, Thaksin Shinawatra, yaliyotokea Septemba, mwaka jana.
Kupinduliwa kwa Shinawatra na Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo, Sonthi Boonyaratglin, kulivuruga mpango huo ambao uliombwa na Lowassa wakati Tanzania ikikabiliwa na ukame, uliosababisha kukauka kwa mabwawa ya kuzalisha umeme.