Utaratibu upo hivi Mkuu, endapo polisi wilaya na hasa OCD mwenyewe amekataa kesi yako isiende mahakamani, unaweza kuchagua, ama kwenda kumuona/kupeleka malalamiko yako kwa kamanda wa polisi wa mkoa husika(RPC) au Mkuu wa Upelelezi wa jinai wa mkoa husika(RCO) ambao watasikiliza lalamiko lako na kuitisha faili la kesi yako ili waone uhalali wa lalamiko lako, kama ni halali basi shauri lako litafikishwa mahakamani, na kama kuna hatua zilizokwama kiupelelezi msukumo utawekwa na kutendewa haki. Endapo hata ngazi ya mkoa wamekukatalia peleka lalamiko lako kwa ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi au Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi(DCI). Au peleka lalamiko lako kwenye ofisi ya wakili wa serikali mfawidhi wa mkoa uliopo au kwa Mkurugenzi wa mashitaka(DPP) ambaye naye ataliitisha jalada na kulisoma ajiridhishe ukweli wa lalamiko lako pindi atakaporidhika atalipeleka shauri lako mahakamani.
Ni vema ukaelewa kuwa siyo kila kesi inayoripotiwa polisi ni lazima ifikishwe mahakamani, sheria ya Jeshi la Polisi iliyotungwa na Bunge imewapa mamlaka Polisi ya kupeleleza na endapo hawatapata ushahidi wa kutosha wa kosa la jinai wanayo mamlaka ya kukataa kulipeleka shauri mahakamani na kulifunga jalada. Hatua hii ni ya makusudi ili kuzuia kesi za kukomoana kwenda mahakamani na matumizi mabaya ya mahakama, kuifanya mahakama isielemewe na mashauri mengi na kuchelewesha haki za watu wengine wenye kesi halali.