Ulishawahi kuona wapi jeshini kunamaridhiano? Watu wengine wajinga sana hili ni jeshi la polisi siyo polisi jamii maridhiano yanatoka wapi
Tatizo la Jeshi la Polisi ni kwamba halikupata nafasi ya kuundwa upya kama ilivyotokea kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania - JW. Jeshi lilipoasi, hapo 1964, lilivunjwa na kuundwa upya kwa malengo tofauti kabisa na yale ya enzi ya mkoloni. misingi ya taifa letu imejengwa na mkoloni, kwa hiyo ilihitajika iundwe upya baada ya uhuru. JW ilipoundwa upya, imeendelea vizuri kutekeleza majukumu yake, kuna vitu vichache sana ambavyo vinahitaji marekebisho.
Kwa Polisi haikuwa hivyo. hata hizo sheria zinazowapa Polisi mamlaka ya kuingilia nafasi ya raia kukutana, kubadilishana mawazo, naam, hata kuandamana, ni sheria za mwaka 1954. Inaelekea ziliundwa ili kukabiliana na tishio la kudai uhuru wa nchi, maana kipindi hicho TAA ilianza kuja juu na mwaka huo ndio TANU ilipoundwa. Kwa hiyo Jeshi la Polisi kimuundo ni la kutetea na kuulinda utawala uliopo. Bahati nzuri kwetu, utawala wa awamu ya kwanza ulijishughulisha hasa na kujenga taifa jipya lililo huru. Sheria hizo zilikuja kuhojiwa na Tume ya Jaji Nyalali, kuonekana kwamba hazifai tena kwa mfumo wa Kidemokrasia ya Vyama Vingi. katika mfumo huu, tunahitaji watu wawe huru kutoa maoni yao, na Jeshi la Polisi litoe ulinzi kwa watu na vyama vyao watoe maoni yao kwa uhuru bila bugudha. kazi ya serikali iliyoko madarakani ni kutekeleza sera na ahadi ilizoahidi. kama watu wanaongea, waache waongee, lakini serikali inachapa kazi ili mwisho wa siku, waweze kuwaonesha watanzania ni kwa kiasi gani walitekeleza ahadi zao.
Mimi sioni tatizo lolote hapo, hata kama watu wanaongea, wanafanya mikutano na maandamano, mwisho wa siku anayejijenga zaidi ni yule anayefanya vitu halisi na watu wanaviona. mashaka yanakuja pale huyo ambaye ndio ana fursa ya kufanya hivyo vitu, anaanza kumuogopa huyo ambaye hana fursa hiyo. Anaogopa nini? ana mamlaka ya kukusanya kodi na kupanga ataitumiaje. atatatua kero za watu. hivi kweli watu wataacha kumsikiliza anayetatua kero zao na kuwapa mahitaji yao, kuwatengenezea fursa za maendeleo vijana na wananchi kwa ujumla, fursa za elimu, kuboresha huduma za afya, wamsikilize anayebwabwaja kwenye mikutano? katu! Na kama ndio hivyo, basi kuna tatizo limejificha. na ni jukumu la wanachi wote kwa uzalendo wao, kulitafuta tatizo hilo na kuliweka wazi.
Jeshi la Polisi libakie kuwa na jukumu la kulinda raia na mali zao, na kuzingatia kwamba hii ni nchi ya Demokrasia ya vyama vingi, vilivyoandikishwa na vinatambuliwa kisheria. Jeshi lisijinasibishe na chama kimojawapo, hata kama ni chama tawala. Jeshi lifanye kazi yake kwa weledi wa sayansi ya kipolisi, na siyo kufuata maagizo ya watawala. maana hapo kuna hatari ya kufanya mambo kwa maslahi binafsi ya watawala, hasa kama watawala ndio wanatoa promosheni na maslahi manono kwa wale wanaotekeleza matakwa binafsi ya watawala, na siyo maslahi ya taifa kwa ujumla wake