Hii ni statement yao nyingine walitutumia mwaka 2007
TANZANIA STUDENTS NETWORKING PROGRAMME
(TSNP)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
YAH: MATANGAZO YA HAKI ELIMU
Vyombo mbalimbali vya habari Julai 10 mwaka 2007
vilieleza kwamba katika Kikao cha Bunge cha tarehe
9-Julai 2007 cha kuchangia mjadala wa hotuba ya Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyowasilishwa Bungeni
na Waziri wa wizara husika Mh. Margareth Sitta
kulizuka mjadala wa kuipinga shirika la Haki Elimu
kutokana na matangazo yake yanayoikosoa Serikali.
Mjadala huo uliibuliwa na Mbunge wa jimbo la Kongwa
(CCM) Mh. Job Ndugai ambaye alidai kuwa Shirika hilo
linatoa matangazo yenye picha mbaya kwa Serikali kwani
hayaonyeshi mafanikio yoyote ya elimu ya Tanzania
yaliyofikiwa na Serikali.
Pia, Mbunge wa viti Maalum-CCM Mh Janet Masaburi
alidai kuwa matangazo ya Haki Elimu hayafurahishi hata
watoto kwani yanajenga matabaka miongoni mwa jamii ya
Watanzania kati ya watoto wa matajiri na masikini.
Wabunge hao wote kwa pamoja wameona kuwa ni bora
Shirika hilo likajisajili ili kuwa chama cha kisiasa
kwani imekuwa ikiishambulia vikali Serikali katika
sekta nzima ya elimu ya Tanzania.
Mtandao wa wanafunzi Tanzania (TSNP) kama wadau wakuu
wa elimu Tanzania, inasikitishwa na kauli za wabunge
hao dhidi ya shirika mtetezi wa wanafunzi wanyonge wa
Kitanzania tunaosoma katika mazingira magumu.
Sisi kama wanafunzi tunaamini kuwa dhima kubwa ya
shirika la Haki Elimu ni kuonyesha uhalisia wa
mazingira ya elimu katika Tanzania. Yale yote
yanaonyeshwa katika matangazo ya Haki Elimu si mapya
bali ni hali halisi yanaoyotokea katika shule nyingi
za Tanzania.
Ugumu wa usafiri kwa wanafunzi masikini, ukosefu wa
vitabu vya kusomea na kufundishia, uhaba wa walimu,
ukosefu wa nyumba za walimu, mishahara midogo ya
walimu, ukosefu wa vitendea kazi ni baadhi ya
matangazo ya Haki Elimu yanaonyesha hali halisi ya
elimu ya Tanzania jinsi ilivyojaa ubabaishaji.
Ijulikane kuwa Haki Elimu imekuwa mstari wa mbele
katika kufanya tafiti mbalimbali zenye lengo la kuinua
ubora wa elimu Tanzania. Hivyo matangazo ya Shirika
hilo ni tokeo la tafiti mbalimbali yakinifu za shirika
hilo. Mfano Haki Elimu Annual reports zinazotolewa
kila mwaka zinaonyesha mafanikio ya tafiti za shirika
hilo zenye lengo la kuinua kiwango cha ubora wa elimu
Tanzania.
Mtandao wa wanafunzi Tanzania (TSNP) unaamini kuwa
Haki Elimu haina dhamira mbaya juu ya Elimu ya
Tanzania bali ni kama kikumbukishi chenye kutoa
taswira kwa Serikali juu ya hali halisi ya elimu
Tanzania.
Ni wazi kuwa, kauli za wabunge hao zinaweza zikawa
chachu kwa Serikali kuamua kuweka kikwazo kama
ilivyokuwa katika kipindi cha Utawala wa awamu ya tatu
ya Mh. B. Mkapa Rais Mstaafu aliyeifungia Haki Elimu
ambapo baadaye iliruhusiwa kuendelea na matangazo yake
na utawala wa awamu ya nne ya Mh Rais Jakaya Kikwete.
Tunaamini kuwa kauli za wabunge hao hasa Mbunge wa
Viti Maalum Mh Janet Masaburi aliyesema kuwa,
nanukuu
tunaomba Taasisi hizi zifahamu kuwa hii nchi
ina wenyewe na hatupendi kuchezewa(Mwananchi
10/07/2007) Kauli hiyo inaonyesha kuwa kuna utabaka
kati ya wenye nchi na wasio na nchi! Tunaamini kuwa
Haki Elimu ni sehemu ya wenye nchi, kwani tunaamini
kuwa kila raia halali wa Kitanzania ana hisa ya uraia
ya kuwa mwenye nchi.
Hivyo kauli ya Mbunge huyo ya kuonyesha kuwa nchi hii
ina wenyewe ni kauli iliyo tata na nzito na yenye
kuonyesha kuwa baadhi ya watu ni wenye nchi na wengine
hawana umiliki wa nchi. Kwa mantiki hiyo ni vyema
kauli ya Mh. Janet Masaburi airekebishe au kuikanusha
kabla ya haijaleta madhara na fikra mbaya miongoni mwa
wananchi wa Tanzania.
Tunaamini kuwa nchi hii ni nchi ya watu wote wenye
uraia halali, walio huru wenye kulindwa na misingi ya
Katiba na sheria za nchi. Hivyo kila raia wa Tanzania
ni mwenye nchi kwani nchi inajengwa na kumilikiwa na
wananchi na siyo vinginevyo.
Misingi ya utawala bora wenye kuzingatia Katiba na
Sheria za nchi zinampatia mtu, kikundi halali, au
taasisi uhuru wa kupata habari, kutoa maoni kulingana
na sheria na kanuni zilizopo, hivyo ni wajibu na Haki
Elimu kutumia uhuru huo ipasavyo katika kuwapatia
watanzania hali halisi ya sekta ya Elimu hapa nchini.
Tunaamini kuwa baadhi ya watu wenye mawazo kama ya
wabunge hao ni watu wenye kulenga kukaribisha mawazo
na mfumo udikteta na kubomoa demokrasia iliyo ya
kweli.
Hivi karibuni kumezuka wimbi la watu au kikundi
kinachozungumza ukweli wenye uhalisia katika jamii
unaonekana ni upinzani. Mfano Mgomo wa wanafunzi wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sokoine kwa kuipinga
sera ya uchangiaji katika elimu ya juu walionekana ni
wapinzani. Hivi haiwezekani kuwa kati na kuzungumza
ukweli bila kupendelea upande wowote.
Nchi nyingi zilizokuwa na misingi ya udikteta zilikuwa
na kazi ya kuzifungia taasisi mbalimbali,
kuzishinikiza wafate mawazo yao kwa manufaa yao
binafsi na siyo kwa manufaa ya umma. Hivyo basi,
mawazo ya wabunge hao yamelenga katika kuimarisha
maslahi yao au ya chama chao pasipo kuangalia maslahi
ya watanzania kwa ujumla, kwani Haki Elimu ipo kwa
maslahi ya Watanzania wote pasipo kuangalia itikadi
zao za kisiasa, kidini au kikabila.
Hatuwezi kuendelea kuwa na asasi zisizo za kiserikali
zenye midomo na fikra za kusemea vyama vya kisiasa,
bali ni jukumu la asasi zote kama Haki Elimu kusimamia
kweli kwa manufaa ya Watanzania wote kwa ujumla.
Hatuwezi kuendelea kusema elimu ya Tanzania ni nyeupe
wakati imejaa weusi, hatuwezi kusema kuwa Tanzania ni
safi wakati imejaa uchafu. Sisi kama wanafunzi tunaona
kuwa elimu ya Tanzania inaweza kuwa bora endapo
mapungufu yatapatiwa ufumbuzi.
Ni fikra potofu kwa utetezi wa hoja ya Mbunge Mh. Job
Ndugai kwa kuonyesha ulinganisho wa Haki Elimu na
matangazo ya yaliyokuwa yanatolewa nchini Zambia
yalivyopelekea kuangaushwa kwa utawala wa
Rais Keneth Kaunda na chama chake cha UNIP. Ijulikane
kuwa Keneth Kaunda aliangushwa madarakani kutokana na
utawala mbovu. Ni wazi kuwa Wabunge hao wametoa
angalizo kwa Serikali ya CCM kuwa wanaweza kuangushwa
na matangazo yanayotolewa na Haki Elimu kama
ilivyokuwa nchini Zambia.
Ni vyema Serikali, Wabunge na watu wenye fikra kama
hizo waache mara moja kushindana na Haki Elimu badala
yake wabuni njia chanya mbadala ya kupambana na
mapungufu yanayotajwa katika matangazo ya Haki Elimu.
Sisi kama Mtandao wa wanafunzi Tanzania (TSNP)
tunapenda kuungana na Haki Elimu na tunaunga mkono
matangazo yote yanayotolewa na Haki Elimu yenye lengo
ya kukuza elimu ya Tanzania na siyo vinginevyo.