UDSM ni mpasuko
Habari Zinazoshabihiana
Mrema aipa dole CCM kusuluhishana na CUF 24.12.2006 [Soma]
Mpasuko wa kisiasa Z'bar wawa mwiba 27.07.2006 [Soma]
'Hali ya Zanzibar kisiasa si sawa na ya Kenya' 14.04.2008 [Soma]
*Uongozi wawapuuza maprofesa wake
*Mhadhiri amdhamini Rais DARUSO
*Polisi wapiga marufuku maandamano
Na Joyce Magoti
SIKU moja baada ya Umoja wa Wahadhiri Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDASA) kuutaka uongozi wa chuo hicho kuwarejesha wanafunzi wote chuoni kwa ajili ya kuendelea na masomo, uongozi wa chuo hicho umepuuza shinikizo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma za Jamii wa UDSM, Prof. Amandina Lihamba alisema uongozi wa chuo hicho utaendelea na msimamo wake wa kuwarudisha chuoni hapo wanafunzi wale tu watakaotimiza masharti ya udahili.
"Sisi hatuwezi kusema chochote kuhusu kauli ya UDASA lakini msimamo wetu ni ule ule wa kuwadahili na kuwarejesha chuoni wale tu watakaotimiza masharti ya udahili labda muende mkawaulize wao kuwa wanasemaje kuhusu hili," alisema Prof. Lihamba.
Kuhusu kuwepo ulinzi mkali uliopo chuoni hapo bila ya kuwa na hali yoyote ya vurugu pamoja na kuzuiwa njia inayotumiwa na wakazi wa jirani na eneo hilo, Prof Lihamba alisema ulinzi huo ni lazima uwepo kutokana na kuwepo kwa kauli za uchochozi na uvunjifu wa amani.
Katika tamko lao juzi UDASA walitaka uongozi wa chuo hicho na Serikali kwa ujumla kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa katika Kamati iliyoundwa mwaka jana na wahadhiri hao ambayo ilibainisha chanzo cha migogoro hiyo na pia namna bora ya utekelezaji wa Sera ya Elimu ya Juu nchini.
Pamoja na taarifa hiyo rasmi ya UDASA kushinikiza wanafunzi wote warejeshwe, kumekuwepo na tetesi za kuwepo mgomo wa wahadhiri hao, hata hivyo hakuna upande huru uliothibitisha habari hizo.
Naye Peter Masangwa na Grace Ndossa wanaripoti kutoka Dar es Salaam kuwa, Jeshi la Polisi nchini limezuia maandamano ya wanafunzi wa elimu ya juu yaliyokuwa yafanyike Dar es Salaam leo, chini ya Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP).
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Bw. Suleiman Kova wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandamano hayo.
Bw. Kova alisema kuwa TSNP si asasi isiyo ya kiserikali kama ilivyojieleza katika barua ya kuomba kuandaa maandamano hayo bali ni kampuni iliyosajiliwa kwa jina la Tanzania Students Networking Programme Limited yenye namba ya usajili SO 42386 tangu Oktoba 23 mwaka 2001.
''Sheria ya Asasi zisizo za Kiserikali ya mwaka 2002, Sehemu ya Tatu kifungu cha 11(3) inaeleza kwamba asasi yoyote lazima ipate hati maalumu ya usajili kabla haijaanza kufanya kazi,'' alisema Bw. Kova na kusisitiza kuwa shirikisho hilo la wanafunzi halikusajiliwa kwa mujibu wa sheria hiyo.
Pia alieleza sababu nyingine ya kutoruhusu maandamano hayo ni kutokana na haja ya kutaka udahili unaendelea kuwa wa amani na utulivu.
Katika hatua nyingine inayoonesha kuwa baadhi ya wahadhiri chuoni hapo hawakufurahishwa na hatua mbalimbali za uongozi wa chuo, Mwandishi Grace Michael anaripoti kuwa mmoja wa wahadhiri chuoni hapo, Dkt. Azavel Lwaitama ameibuka na kumdhamini Rais wa Serikali ya Wanafunzi (DARUSO), Bw. Antony Machibya ambaye alikuwa anasota rumande kutokana na kukosa dhamana.
Mbali na Bw. Machibya kudhaminiwa, wanafunzi wengine ambao walikuwa wakisota rumande nao wamekamilisha masharti ya dhamana hivyo wako nje kwa dhamana hadi Februari 2, mwaka huu kesi yao itakapotajwa.
Wanafunzi hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu siku ya Jumatano wakikabiliwa na mashitaka ya kuandaa mkutano usio rasmi.
Washitakiwa hao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Mtandao wa Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania, Bw. Stephen Owawa, Bw. Sabinian Prince, Bw. Titus Ndula na Bw. Paul Issa ambao wamesota rumande kwa muda wa siku tatu.
Walidaiwa kuwa January 19 mwaka huu, saa 3.45 asubuhi katika maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa nia ya kutenda kosa, waliandaa mkutano usio halali na kubeba mabango.
Chanzo: MAJIRA
Prof. Baregu, Dk. Mvungi walia na Bodi ya Mikopo
2009-01-24 16:08:16
Na Sharon Sauwa, Jijini
Baadhi ya wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, UDSM, wameshauri kufanyiwa kwa marekebisho kwa utata uliopo katika sera ya uchangiaji wa elimu ili kuepusha migomo inayotokana na utaratibu wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Jijini Dar es Salaam, wamesema kuna matatizo katika suala la uchangiaji katika elimu ya juu ambapo hivi sasa linaonekana kutonufaisha zaidi taifa.
``Nafikiri tuwaamshe wote. Kuna matatizo katika sera ya uchangiaji wa elimu ya juu. Inatupasa wadau wote kukaa kwa pamoja na kujadili kuhusiana na sera hii,`` akasema Profesa Mwesiga Baregu.
Akasema suala la elimu limebaki kuwa ni manufaa kwa mtu binafsi badala ya umma mzima wa Watanzania, jambo ambalo amesema linahatarisha uhai wa taifa.
``Sasa hivi, suala la elimu linaonekana kama lina manufaa ya mtu binafsi badala ya taifa,`` akasema.
Akaongeza kuwa sasa, ni lazima Watanzania wawe na elimu ya kutosha ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo duniani.
Akaongeza kuwa ili taifa liweze kuendelea na kukabiliana na changamoto za elimu, inatakiwa wananchi wajengewe mazingira ya kuelimika mpaka mwisho wa upeo wao.
Kwa upande wake, Dk. Sengodo Mvungi amesema viongozi wa vyuo vikuu wasiwe wanachaguliwa na wanasiasa.
Akasema ili kupata viongozi wazuri wa vyuo vikuu ni muhimu wakapatikana kwa njia ya kuchaguliwa na wanataaluma wenyewe.
``Wanataaluma watumike katika kuwachagua viongozi wa vyuo, maana wao ndio wanaowajua viongozi wazuri na sio wanasiasa kama ilivyo sasa,`` akasema Dk. Mvungi.
Pia akashauri kuwa shughuli za uendeshaji wa Bodi ya Mikopo Nchini, kutenganishwa na shughuli za vyuo vikuu ili kuepusha migomo inayoweza kujitokeza kwa sababu mbalimbali, hasa madai yanayoelekezwa kwa taasisi nyingine.
Hata hivyo, akasema kuwa mgomo wa mwaka jana ambao ulisababisha chuo kufungwa tangu mwezi Novemba, anaamini ulisababishwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na si uendeshaji wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwishoni mwa mwaka jana wanafunzi wa vyuo vikuu vya umma nchini waligoma kushinikiza Serikali kufanyia marekebisho sera ya uchangiaji wa elimu ambayo walidai kuwa inaleta ubaguzi.
Hali hiyo ilisababisha vyuo vingi vya umma kufungwa na hadi sasa, uongozi wa chuo hicho umelazimika kutumia Jeshi la Polisi katika kusimamia ufanikishaji wa zoezi la kuwadahili upya wanafunzi wote wa chuo hicho.
SOURCE: Alasiri