Baadhi ya watu hushauri matumizi ya pombe kali ili kutibu mafua na kikohozi. Madai yao yamebeba nadharia nyingi zinazohitaji uthibitisho wa kisayansi ili kuondoa sintohamu kubwa iliyopo.
Ikumbukwe pia pombe ni mojawapo ya viambato vinavyotumika kwenye kutengeneza baadhi ya dawa za kutibu kikohozi.
Ukweli wa madai haya upoje?
Ikumbukwe pia pombe ni mojawapo ya viambato vinavyotumika kwenye kutengeneza baadhi ya dawa za kutibu kikohozi.
Ukweli wa madai haya upoje?
- Tunachokijua
- Pombe siyo dawa ya kikohozi na mafua. Miongozo mbalimbali ya kitabibu pamoja na Taasisi ya Udhibiti na Kinga ya Magonjwa ya Marekani (CDC) haishauri wagonjwa wa kikohozi na mafua kutumia pombe kwa kuwa huongeza ukubwa wa matatizo haya.
Hata hivyo, kileo aina ya ethanol (ethly alcohol) ni mojawapo ya viambato vinavyotumika katika kutengeneza dawa za kikohozi hasa zile zinazopatikana kwenye mfumo wa vimiminika (syrup). Huwekwa ili ifanye kazi mbili-
- Kuzuia kuharibika kwa dawa hiyo (Preservation)
- Kuyeyusha kemikali hai za dawa (Active ingredients) ambazo baadhi yake huwa haziwezi kuyeyuka kwenye maji
Kwa namna ya kipekee, ugonjwa wa mafua kwa kiasi kikubwa husababishwa na virusi wanaopatikana kwenye aina zaidi ya 200, ambapo jamii ya Rhinovirus ndio huongoza. Mara nyingi ugonjwa huu hupona wenyewe ndani ya siku chache pasipo kuhitaji dawa.
Pia, utafiti wa Yuzhoujia Deng et al (2022) unaonesha kuwa pombe hubana njia ya mfumo wa upumuaji. Hii inaweza kuongeza ukubwa wa tatizo kwa watu wenye kikohozi na mafua.
Madhara mengine ya pombe ni kuufanya mwili upoteze kiasi kikubwa cha maji, hali isiyo rafiki kwa wagonjwa wa mafua na kikohozi ambao huhitaji mwili uwe na kiwango kikubwa cha vimiminika kama sehemu ya tiba.
Hivyo, kwa kuangalia miongozo mbalimbali ya afya pamoja na kukosekana kwa uthibitisho wa tafiti za kisayansi unaonesha ufanisi wa pombe kwenye kutibu mafua na kikohozi, JamiiForums inamebaini kuwa madai ya pombe kutibu magonjwa haya si kweli.