Nadhani tuna umaskini (wa kipato na usio wa kipato) miongoni mwa watu wetu, ambao unaambatana na aina fulani ya udumavu wa kifikra katika ngazi zote (kuanzia "mashinani" hadi ngazi za juu za uongozi). Wakati fulani nilialikwa kushiriki zoezi la kutafuta njia za kuwamotisha waalimu wa shule za vijijini, na tukafanya utafiti kutafuta mapendekezo kutoka kwa waalimu wenyewe walioko huko vijijini. Wengi walipendekeza kuwa wapatiwe semina mbalimbali, na walitaja hata vitu ambavyo wangependa kujifunza. Cha ajabu ni kuwa mafunzo hayo yalipoletwa, ushiriki wa siku ya kwanza ulikuwa mkubwa sana, lakini kuanzia siku iliyofuata mahudhurio yalidorora sana! Kisa? Hakukuwa na posho ya mafunzo! Kumbe wenzetu waliposema "semina" walimaanisha "posho"! Tulishangaa zaidi tulipofanya kikao na maafisa elimu, waratibu na wakuu wa mashule kuwapa ripoti ya kazi yetu, ulizuka ugomvi wanaulizia "kumbe kikao hiki hakina posho?" Tukawaambia jamani ndio maana tumefanyia ofisini kwenu (ukumbi wa halmashauri mojawapo), saa za kazi, ili pasiwepo ulazima wa malipo, hizi ni jitihada za kusaidia elimu hapa. Kwani kilieleweka kitu? Ajabu zaidi ni kuwa waliokuwa wanaongoza kudai posho kwa nguvu kama hawana akili nzuri ni maafisa wakubwa tu wa serikali waliokuwepo! Sasa hili jinamizi ni baya sana, mtu anataka asaidiwe kazi yake, na bado alipwe posho! Mwingine anataka asomeshwe halafu alipwe kusomeshwa! Katika nchi zilizoendelea watu hulipa hela nyingi tu ili wasome (continuing professional development), lakini kwetu wanataka "wahongwe" ndipo wasome! Na wakuu wa serikalini wanataka walipwe posho za ziada kufanya kazi zao za kawaida tena saa za kawaida za kazi!
Je tutafika? (naazima swali la Mzee Makwaia wa Kuhenga, sioni likijibika).
Je tutafika? (naazima swali la Mzee Makwaia wa Kuhenga, sioni likijibika).