Wabunge waonyesha jeuri
Wachukua nyingine mbili mpya jana
Sitta asema si haramu, ni takrima
Wapuuza vitisho vya Takukuru
Mapambano ya wabunge na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa juu ya upokeaji wa posho mara mbili jana uliingia hatua mpya baada ya kupokea posho hizo kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Hatua hiyo si tu inaiweka Takukuru katika mazingira magumu zaidi juu ya hatua zake za kuwahoji wabunge kwa kuchukua posho mara mbili, ile wanayolipwa na Ofisi ya Bunge na za kwenye taasisi nyingine za umma wanakokwenda kufanya kazi, bali inaonyesha wazi kupuuzwa kwa harakati hizo za kuwadhibiti wabunge.
Jana mchana wabunge wakiwa wamekwisha kuhudhuria kikao cha asubuhi cha Bunge na kwa maana hiyo kuhalalisha posho zao kutoka Ofisi ya Bunge, walihudhuria semina iliyoandaliwa na Wizara hiyo ili kujadili muswada wa sheria ya watoto.
Muswada huo unaoratibiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, ulisomwa kwa mara ya kwanza bungeni Julai 31, mwaka huu.
Jana semina hiyo ilifunguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Philip Marmo, na ilihudhuriwa pia na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Margareth Sitta, Manaibu Waziri na watumishi wengine wa Bunge.
Semina hiyo ililenga kuwaelimisha wabunge hao kuhusu muswada huo.
Kabla ya semina hiyo, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, asubuhi baada ya kipindi cha maswali na majibu aliwatangazia wabunge kuwepo kwa semina hiyo na kusema ‘itifaki zote zimezingatiwa.'
Sitta alisema kuwa wabunge wamekuwa wakiandamwa kutokana na kulipwa posho nje ya Bunge, lakini akasema hiyo ni takrima na kwamba makundi mengine wakiwemo waandishi wa habari nao wanaipokea.
Wabunge waliohojiwa na Nipashe kuhusu kauli hiyo walisema ina maana pana, lakini yenye kubeba tafsiri ya huduma zote zinazohitajiwa kwa mwalika wa semina, ikiwemo makabrasha na posho.
Akifungua semina hiyo, Marmo alisema inatoa fursa muhimu kwa wabunge kuujua muswada huo kwa undani, hivyo kurahisisha mjadala pindi utakapofikishwa bungeni.
Marmo alisema kwa muda mrefu Tanzania haijakuwa na Sheria ya Watoto, hivyo muswada huo utasaidia kujenga na kufanikisha upatikanaji wa mazingira bora na haki kwa mtoto.
Alisema baada ya kusomwa kwake, muswada huo ulijadiliwa na wadau mbalimbali waliotoa maoni yao ambayo kwa kiasi kikubwa yatafanikisha azma ya kuwezesha kupatikana kwa haki za mtoto.
Wakati huo huo, habari zimetanda mjini hapa kuwa bado Takukuru wanaendelea kuwawinda baadhi ya wabunge machachari ili kuwahoji kabla ya kuwasilishwa bungeni taarifa ya serikali kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu kashfa ya Richmond.
Habari kutoka vyanzo mbalimbali mjini Dodoma, zinaeleza kuwa baadhi ya wabunge ambao wamesimama kidete kuibana serikali kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Richmond wamepelekewa taarifa za kujiandaa kuhojiwa na taasisi hiyo kuhusiana na kupokea posho nje ya vikao vya Bunge.
Mbunge mmoja ameiambia Nipashe kuwa tangu wiki iliyopita alitaarifiwa na Takukuru kuhusu mpango wa kumuita kumhoji, lakini akasema hadi sasa hajaitwa.
Alisema anashangaa hadi sasa kutoitwa na Takukuru, hatua ambayo alisema inalenga kudhoofisha mjadala wa Richmond baada ya kuwasilishwa bungeni Jumatano ijayo. Mbunge mwingine, ambaye naye ameeleza kuwa ataitwa kuhojiwa na Takukuru, alisema kitendo cha kuwaita na kuwahoji siku chache kabla ya kuwasilishwa na kujadiliwa kwa hoja ya Richmond, lengo lake ni kutaka kuwajengea hofu ili wasiweze kushiriki katika mjadala huo.
Baadhi ya wabunge ambao wamethibitisha kuhojiwa na taasisi hiyo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, William Shellukindo.
Shellukindo, ambaye ni Mbunge wa Bumbuli (CCM) na kamati yake wamekuwa mstari wa mbele kuibana serikali itekeleze maazimio ya Bunge kuhusu Richmond hususan azimio linalotaka watendaji waliohusika kuipa zabuni ya kufua umeme wa dharura wa megawati 100 wa kampuni hewa ya Richmond wachukuliwe hatua.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye aliiongoza Kamati Teule ya Bunge kuchunguza uhalali wa zabuni ya Richmond, aliitwa kuhojiwa na Takukuru, lakini alikataa kufanya hivyo. Alipotakiwa kuthibitisha kuwepo kwa mpango huo, Afisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwani, alisema jana jioni kuwa hakuwa katika nafasi ya kulitolea ufafanuzi suala hilo kwa kuwa yuko nje ya ofisi kutokana na ugonjwa.
Mbunge mwingine ambaye amehusishwa na mpango wa kuhojiwa ni Lucas Selelii, Nzega (CCM). Selelii ni mmoja wa wajumbe waliounda Kamati Teule ya Bunge ya kuchunguza zabuni ya Richmond.
Baadhi ya Wabunge na makundi mengine ya jamii wanaichukulia hatua ya Takukuru kuwa ina lengo la kulitisha Bunge ili lisiweze kuibana serikali ili iwachukulie hatua waliohusika na mkataba wa kitapeli ulioligharimu taifa kiasi cha Sh. bilioni 200 kuilipa kampuni ya Richmond na mrithi wake Dowans.
Kutokana na mlolongo wa matukio hayo, baadhi ya watu wanahoji uadilifu wa Takukuru inayoongozwa na Dk. Hoseah kuwahoji wabunge wakati hatma ya utekelezaji wa mapendekezo ya Bunge haijajulikana.
Kashfa ya Richmond ilimlazimisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu Februari mwaka jana pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na mtangulizi wake, Dk. Ibrahim Msabaha.
Pamoja na mambo mengine maazimio ya Bunge yalitaka kuwajibishwa kwa watendaji wa serikali wakiwemo aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah.
CHANZO: NIPASHE