Porojo za Dk. Mwakyembe
Atamba anajua sheria, ataibwaga TAKUKURU
na Sauli Giliard, Dodoma
MBUNGE wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, jana aliwashangaza waandishi wa habari wanaohudhuria mkutano wa 17 wa Bunge mjini Dodoma, baada ya kuitisha mkutano nao na kuhoji kwanini wanakunywa chai ya wabunge wakati wamelipwa posho na vyombo wanavyofanyia kazi pasipo kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), badala ya kutoa ufafanuzi wa kama alipokea posho mara mbili au la.
Dk. Mwakyembe alihoji hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa habari wa Bunge, baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, wakati akitoa ufafanuzi wa kukataa kuhojiwa na TAKUKURU kuhusu kuchukua posho mara mbili kwa kufanya kazi moja.
Akizungumza kwa ghadhabu, Dk. Mwakyembe alisema kitendo cha kuhojiwa na TAKUKURU wakati huu ambapo wajumbe wa kamati iliyochunguza suala la Richmond wakitaka Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk. Edward Hoseah, ahojiwe, ni mbinu za kutaka kuwanyamazisha.
Dk. Mwakyembe alisema kupokea posho ni utaratibu wa siku nyingi na wa kawaida, hivyo kuhojiwa sasa ni mbinu tu ya TAKUKURU kutaka wabunge wasimhoji Dk. Hoseah.
Alisema kwa uelewa wake wa kisheria, ikizingatiwa kuwa yeye ni mwalimu wa sheria, pamoja na kubaini mchezo huo, hakukubali kuhojiwa kama alichukua posho mara ya pili katika kikao cha kamati ya Bunge kilichofanyika mjini hapa na alitamba kuwa hata kama TAKUKURU itaamua kumpeleka mahakamani, ataibwaga vibaya.
Lunch allowances ni utaratibu wa siku nyingi na wa kawaida. Hata waziri akitembelea mikoani huwa anaandaliwa vizuri, licha ya kwamba amepewa posho. Kwani inawezekana kutomwandalia kwa sababu amekwishapewa posho? alihoji Dk. Mwakyembe.
Aliwashangaza waandishi wa habari alipowahoji kwanini hawajawahi kuhojiwa na TAKUKURU kwa kunywa chai ya wabunge huku ikijulikana kuwa wametumwa na vyombo vyao wanavyovifanyia kazi, huku akidai kushangazwa na hatua ya wabunge kufanyiwa hivyo sasa.
Huku akilifananisha gazeti lililochapisha habari yake ya kukataa na kuomba msaada wa Spika wa Bunge, Samuel Sitta ili asihojiwe na TAKUKURU kuhusu madai ya kupokea posho mara mbili, alisema kama hilo ni kosa, TAKUKURU ndio vinara wa kutoa posho.
Alitoa mfano wa hivi karibuni katika semina iliyoandaliwa na taasisi hiyo, ambapo licha ya kufahamu kuwa anaishi jijini Dar es Salaam, ilimpa posho ya malazi.
Hawa TAKUKURU ndio vinara wa kutoa posho. Inafahamika mimi naishi Dar es Salaam, wananipatia posho, leo hii pamoja na mambo mengi yanayotaka majibu wanataka kutuhoji, kama hii si kuwadhalilisha wabunge ni nini? alihoji huku akionekana kukasirika.
Mbunge huyo mara kwa mara akihusisha kitendo hicho na mchezo mchafu unaofanywa na aliowaita mafisadi. Alisema TAKUKURU imewaita wabunge kwa kutaka kuwahoji huku wao wakitaka serikali imchukulie hatua Dk. Hoseah na kwamba hilo ni lengo mahususi la kukwamisha juhudi za wabunge.
Sisi tunataka utekelezaji wa maazimio 23 ya Bunge, mojawapo ni lile la kuhojiwa kwa viongozi wa TAKUKURU, alisisitiza.
Dk. Mwakyembe alibainisha kwamba, kukaidi wito wa TAKUKURU wa kuhojiwa juu ya suala hilo kunatokana na kinga aliyonayo kama ilivyobainishwa katika kanuni za Bunge sehemu ile ya 100 pamoja na 101, ambayo inamlinda kama mtumishi wa chombo hicho cha kutunga sheria.
Aliendelea kujigamba kuwa kamwe hakuna mtu wa kumngoa jimboni mwake na aliwataka wale aliowaita mafisadi waelewe kuwa hawawezi kumngoa, labda wapige kambi kwa miaka mitano wakiwa pamoja na wake zao.
Mafisadi kuningoa Kyela ni kazi ngumu, labda washinde Kyela kwa miaka mitano pamoja na wake zao, ndiyo wanaweza kufanya hivyo, alijigamba.
Alisema wakati TAKUKURU inaendelea kungangania kuwahoji, zipo hoja za msingi zinazotakiwa kujadiliwa, ikiwa ni pamoja na ile ya nani mmiliki wa Kagoda na Richmond.
Taarifa zilizotufikia kutoka ndani ya kikao cha ndani ya kamati ya wabunge wa CCM, muda mfupi kabla ya kwenda mitamboni zilieleza kuwa wabunge hao wamegawanyika kuhusu suala la kuhojiwa na TAKUKURU, baadhi wakikubaliana na hatua hiyo na wengine wakipinga na kutaka isitishwe mara moja.
Taarifa hizo zilieleza kuwa kundi la kwanza linaloungwa mkono na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, linaunga mkono hatua hiyo ya TAKUKURU, kwa hoja kwamba fedha nyingi za serikali zimepotea kwa kuwalipa posho mara mbili wabunge.
Kundi la pili linalodaiwa kuungwa mkono na Spika Sitta linadaiwa kuipinga hatua hiyo ya TAKUKURU, kwa madai kuwa inawadhalilisha wabunge.
Hata hivyo habari hizo zilidai kuwa, licha ya Spika kutaka hatua hiyo isitishwe, Pinda alitangaza msimamo wake kuwa ni lazima kazi ya kuwahoji wabunge wote wanaotuhumiwa kuchukua posho mara mbili iendelee.
Wakati huo huo, hatima ya kujadiliwa kwa hoja ya Richmond bungeni bado ni tete, hadi sasa hakuna taarifa zozote za iwapo wabunge watafanya hivyo.
Pamoja na sakata hilo la Richmond, mambo mengine ambayo bado haijabainika iwapo nayo yatajadiliwa ni pamoja na Kampuni ya Reli (TRL), TICTS na mgodi wa makaa ya mawe, Kiwira.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari Mkuu wa Bunge, Ernest Zulu, alisema masuala hayo yaliyopewa kipaumbele kuwa yatajadiliwa katika mkutano wa 17 wa Bunge unaoendelea mjini hapa, kwa sasa yapo chini ya kamati husika hadi hapo watakapowasilisha taarifa zake kwa Spika.
Kwa sasa kamati hizo bado zinapitia taarifa zao, wakishawasilisha bungeni ndipo itajulikana kama watajadili au hawatajadili, alisema Zulu.
Hata hivyo alisema kuna uwezekano wa Bunge kuongezwa siku mbili zaidi badala ya kumalizika Novemba 6, likaisha Novemba 8.
Zulu alisema katika kikao hicho kutawasilishwa hoja tatu.
Watakaowasilisha hoja hizo ni Mbunge wa Longido, Saningo ole Telele (CCM) anayelalamikia ukiukwaji wa haki za binadamu kwa wafugaji waliohamishwa kwenye maeneo yao na wawekezaji. Mbunge mwingine atakaetoa hoja binafsi ni Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Halima Mdee, ambaye anataka ufafanuzi wa jinsi Kiwanda cha Tanganyika Packers kilivyobinafsishwa. Mwingine ni Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), ambaye hoja yake binafsi ni kutaka masuala ya dini yasijadiliwe bungeni.