Spika Sitta kigeugeu
• Akana kauli zake, barua rasmi ya ofisi yake
na Charles Mullinda
Alipoulizwa kuhusu uhusiano wake na Katibu wa Bunge, Kashililah kama ni wa shaka kiasi cha kuandika barua nyeti inayoomba msaada wa taasisi nyingine pasipo kumtaarifu, Spika Sitta alisema haamini kama Kashililah aliandika barua hiyo na kama aliandika, basi alilazimishwa na viongozi wa juu wa serikali.
Katika hatua ya kushangaza, Spika alitoa kauli nyingine kuwa hata kama Kashililah aliandika barua hiyo, basi alikuwa anatekeleza majukumu yake ya kiutalawa hivyo anaweza asimtaarifu lakini TAKUKURU walipaswa kutochukua hatua zozote kulingana na barua hiyo kabla ya kumtaarifu.
"Mambo ya utalawa sishiriki kila jambo, mhusika mkuu ni katibu na nadhani alilichukua kiutawala zaidi. Lakini TAKUKURU kabla ya kuanza kuifanyia kazi barua hiyo ni lazima wangenitaarifu kwanza Spika.
"Hili jambo tumelijadili sana jana na juzi, tumebaini kuwa Katibu wa Bunge alitishwa sana. Watu wakubwa serikalini wamekaa vikao vingi tu, wamemtisha sana katibu kuwa ni lazima aandike barua hiyo, oh… eti ni maagizo ya rais, wakamlazimisha kuandika barua ile. Hili mimi siliafiki na tumefikisha malalamiko kwa waziri mkuu leo.
"Bunge haliwezi kuendeshwa kwa vitisho, serikali iache kabisa kulitisha Bunge…. Bunge litakataa. Kama mbunge anatuhumiwa kuna Kamati ya Maadili ya Bunge, itashughulikia tuhuma hizo, si mambo haya yanavyofanyika sasa. Ni njama tu, lakini kamwe hatulegezi kamba, Bunge litaendelea na kazi yake pamoja na vitisho vyote," alisema Spika Sitta.
Wakati Sitta akitoa kauli tatanishi kuhusu barua iliyoandikwa na Kashililah kwenda kwa Hoseah huku akisisitiza kutoifahamu, Tanzania Daima Jumatano imefanikiwa kuiona barua hiyo yenye kumbukumbu namba CEB.50/155/05/81 ikiwa na kichwa kinachosomeka: ‘Baadhi ya kamati za Bunge kuomba takrima serikalini na katika mashirika ya umma.'
Sehemu ya barua hiyo inasomeka hivi: ‘Tafadhali rejea mazungumzo kati ya Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Bunge kuhusu suala tajwa hapo juu.
‘Nimepokea malalamiko kuhusu mwenendo usioridhisha wa kamati za Bunge kuomba takrima kutoka kwa watendaji wakuu serikalini na mashirika yake wanapohojiwa na kamati za Bunge.
‘Hivyo ili kuepuka athari zaidi, ilionekana kuwa ni busara jambo hili likatazamwa kwa kina ili kuainisha chimbuko lake linaanzia wapi, nani wahusika wakuu, hatua gani zichukuliwe na kwa utaratibu upi. (Rejea nyongeza ya nane ya kanuni za Bunge za toleo la 2007 kuhusu mgawanyo wa kazi wa kila kamati).
‘Ni tegemeo langu kuwa suala hili utalipatia kipaumbele na kulitazama kwa ungalifu mkubwa, kwa kuzingatia aina ya makundi yanayohusika na nafasi yake katika jamii ya uongozi wa nchi, ili pamoja na kulitafutia ufumbuzi, bali pia kuwa makini katika kulishughulikia.'
Barua hiyo pia imenakiliwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa.
Spika alipoulizwa kuhusu barua aliyoandikiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Mei 26 mwaka huu ikimtaarifu kuwa amepokea malalamiko kuwa wabunge wanadai posho wanapotembelea ofisi za serikali, taasisi na mashirika ya umma, Spika Sitta alikana huku aking'aka na kuhoji kwa nini mwandishi anambana kwa maswali magumu.
"Kwa nini una mambo magumu sana wewe, mwandishi gani huridhiki na maelezo unayopewa, kila ukijibiwa unaendelea kuhoji hoji tu, basi andika unavyotaka, mimi sijaona barua niliyoandikiwa na Waziri Mkuu ikielezea kuwapo kwa jambo hilo," alisema kwa ukali Spika Sitta.
Wakati Spika Sitta akikana kuiona barua hiyo, Tanzania Daima Jumatano imefanikiwa kuiona barua hiyo yenye kumbukumbu namba PM/P/2/567/33, yenye kichwa kinachosomeka: ‘Malipo ya posho kwa wabunge wanapotembelea kikazi ofisi za serikali, taasisi na mashirika ya umma.'
Sehemu ya barua hiyo inasomeka hivi: "Kwa muda mrefu sasa zimekuwapo taarifa mbalimbali kwamba baadhi ya kamati za Bunge zinapotembelea wizara, mikoa, taasisi za serikalki na mashirika ya umma, ama zinaomba au zinadai kulipwa posho mbalimbali. Posho hizo ni pamoja na posho za kujikimu, posho za kikao na takrima.
"Nimepewa taarifa kuwa wizara ambazo maofisa wahasibu walitakiwa kufanya malipo hayo ni pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Maji na Umwagiliaji, Afya na Ustawi wa Jamii, Maliasili na Utalii, Nishati na Madini, Kilimo, Chakula na Ushirika na Viwanda, Biashara na Masoko.
"Nimeona ni busara nitoe taarifa hii kwako ili uweze kutumia njia zako za kiofisi kuwaasa waheshimiwa wabunge wachache wanaofanya hivyo waache, kwani mambo kama haya yanaweza kulipuka siku yoyote na yakalifedhehesha Bunge letu tukufu."
Barua hiyo ambayo imesainiwa na waziri mkuu mwenyewe, imenakiliwa kwa Rais Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo.
Wakati huo huo, Spika Sitta jana alimtetea msaidizi wake, Christopher Ndallu, kuwa hahusiki na upotevu wa aina yoyote ya fedha za Bunge wala hajashindwa kurejesha masufuru kama ilivyoelezwa na Kamati ya Hesabu za Serikali.
Akizungumza kupitia simu yake ya kiganjani kuhusu tuhuma hizo zilizoelekezwa kwa msadizi wake huyo, Spika Sitta alisema si kawaida yake kuzungumzia mambo ya kitoto kama hayo ya msaidizi wake kushindwa kurejesha masurufu kwa fedha anazochukua, lakini amelazimika kufanya hivyo kwa sababu jambo hilo linakuzwa.
Alisema, kamati hiyo ina chuki binafsi, jambo linalodhihirishwa na uamuzi wake wa kuamua kuhoji matumuzi ya safari zake wakati akiwa nje ya nchi na msaidizi wake aliyetuhumiwa naye akiwa hayupo.
"Mimi sichukui masufuru, hilo kwanza lieleweke. Lakini Spika ana mambo mengi sana, hivyo fedha inayozungumzwa ni ndogo mno. Ninahudumiwa na serikali kwa safari zangu za ndani na nje ya nchi, nyumbani kwangu na ofisini kwangu, sasa milioni 70 kweli zinaweza kuwa gumzo kwa hadhi ya Spika? "Mambo ya kurejesha masurufu yana matatizo makubwa, Ndallu ana kila kitu, anazo risiti zinazodaiwa hazionekani na ushahidi mwingine wote. Ni majungu tu, hii kamati ina chuki binafsi, ndiyo maana wameamua kuhoji hili mimi nikiwa sipo na Ndallu pia. "Nimeamua kuzungumza hili kwa sababu limekuzwa sana, lakini huwa siongelei mambo ya kitoto namna hii. Milioni 70 kwa hadhi ya Spika wapi na wapi, nahudumiwa na serikali safari zangu, walinzi wangu, wasaidizi wangu, nyumbani na ofisini kwangu, sasa hiyo pesa unayohoji, kweli haya yote kwa Spika! Mbona hawahoji kwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu au Jaji mstaafu. Kwa nini Spika tu?" alisema Spika Sitta.