Hii yote inatudhihirishia tuna wanasiasa wa aina gani. Hapa hatuangalii chama, tunaaangalia wanasiasa wetu walivyotutelekeza na kulinda maslahi yao binafsi.
Eti mbunge anadai, ninanukuu "posho imeongezwa kwa sababu mishahara ya wabunge ni midogo sana. Na si wabunge tu, hata watumishi wote wa umma mishahara yao ni midogo. Mimi nilikuwa na kazi yangu na nilikuwa ninapata pesa nzuri tu".
- Kwa nini wasiwatetee watumishi wa umma ikiwa wanajuwa kuwa mishahara yao midogo, badala yake wanazuwia chao kimya kimya, mtumishi wa umma atajiju.
- Kwa nini kama mbunge aliona mshahara wa bunge ni mdogo, asibakie kwenye kazi yake?
- Kwa nini bunge lisiwaongezee mshahara na kufuta kabisa posho, posho zinazochangia kuliangamiza taifa?
Hawa watu wanatufanya tusiwe na imani nao tena. Tuliwachagua kutetea maslahi ya nchi na wananchi na sio kutetea matumbo yao. Kwa nini Watanzania hatufiki wakati tukasema basi? Basi kudanganywa! Basi ahadi za uongo!
Juzujuzi niliona jinsi wananchi wa mkoa mmoja Amerika ya Kusini (nchi nimesahau), ambapo mgombea kiti cha umeya alikuwa anafanya kila awezalo kuwafuta wagombea wenzake (ikiwemo mauaji). Siku ya kupiga kura, wananchi wa mkoa mzima walisusa kupiga kura, akapiga kura yeye, mkewe na manyang'au wenzake tu. Kwa aibu, aliamua kuwachia ngazi.
Huu ndio uzalendo. Hii ndio jawabu ya wananchi wanaokataa kuburuzwa. Huku ndiko kuwaadhibu viongozi walafi, wezi, wapenda madaraka, wanaojali maslahi yao na kuwawacha wananchi waishi kwa kudra. Watanzania tunaburuzwa, lini tutasema Basi imetosha!?