Mlalahoi
JF-Expert Member
- Aug 31, 2006
- 2,182
- 885
Nimekutana nayo hii huko KwanzaJamii.Mwandishi ni Profesa Joseph Mbele
Mwenyekiti
Hoja zangu zitaingiaje vichwani mwa watu wenye akili finyu, wasiojiamini, ambao hata kujitambulisha hawajitambulishi?
Ufinyu wa mawazo unajitokeza hapo watu wanapodhani kuwa kazi ya kujenga nchi ni ya rais, wanapokaa vijiweni na kungojea Kikwete afanikishe malengo ya Taifa. Ukiachilia mbali akina mama huko vijijini ambao wanafanya kazi sana, na baadhi ya watu mijini, mamilioni ya Watanzania wanakaa vijiweni wakisogoa badala ya kufanya kazi.
Watanzania wengi wanakaa vijiweni, kwenye baa, kwenye sherehe, badala ya kuwajibika kazini. Hata maofisi yameshakuwa vijiwe. Ni nchi gani inayoweza kusonga mbele na wananchi wa aina hiyo, hata kama kiongozi ni makini sana? Ufinyu wa mawazo ndio unawafanya watu wasione hilo, na badala yake wawe wanamshambulia rais. Jishambulieni pia nyinyi wenyewe.
Sasa pamoja na ufinyu huo, hao ndio wanaodai kuwa wataweza kushindana katika dunia hii wakishapata uraia wa nchi mbili. Mtashindana na nani kama ni waoga namna hiyo, msiojiamini? Mpewe hata uraia wa nchi kumi, mwone kama mtaiweza dunia hii inayohitaji elimu, maarifa na ujuzi.
Inafahamika wazi, na imefahamika kwa miaka mingi, kuwa waTanzania wanapata shida hata kujieleza. Lugha inawashinda, iwe ni ki-Swahili au ki-Ingereza. Vyuoni, inabidi mwalimu anapofundisha atumie maneno ya ki-Ingereza na kiSwahili, kwani lugha ya kufundishia, yaani ki-Ingereza, haifahamiki vizuri. Na bado watu mnaamini kuwa, pamoja na uzembe wote huu, mkipata uraia wa nchi mbili mtaweza kushindana ulimwenguni.
Huku Marekani, kuna nafasi za kufundisha ki-Swahili katika vyuo mbali mbali. Ajabu ni kuwa wa-Kenya ndio wengi wanaochukua nafasi hizo. Watanzania bado wako vijiweni, hawasikii la mtu.
Daima nimewaambia wa-Tanzania kuwa tujizatiti kielimu, na tujielimishe kweli. Na ninajaribu kutoa mchango wangu kwa upande huo. Sio siri, hata vitabu nimewawekea huko huko Tanzania. Lakini wa-Tanzania ndio hao, maneno na maringo yasiyo na maana. Shuleni wanatafuta dezo, na wengine wanaghushi vyeti. Wako wanaodhani watafanikiwa kwa kutumia ngozi za binadamu, viungo vya albino, bahati nasibu za makampuni ya simu au bia, uraia wa nchi mbili, na kadhalika.
Huku ni kujidanganya. Inabidi Watanzania mtambue kuwa leo kinachoongelewa ni uchumi unaoendeshwa na ujuzi, elimu, na maarifa. kwa kiIngereza wanaita knowledge economy. Tujitazititi kielimu. Bila kujizatiti namna hiyo, hata mkipata uraia wa nchi kumi haitawasaidia, kwani mtashindana na watu wa dunia yote waliojizatiti ipasavyo.
Nitakuja Tanzania mwaka huu kuendesha warsha, na ratiba mtaipata. Njooni tukutane, kama mnajiamini. Lakini vile vile, njooni tuelimishane, kama mnataka kujiandaa kweli kwa ushindani wa dunia hii ya utandawazi. Warsha moja imeshapangwa tayari. Itafanyika Arusha Community Center, tarehe 3 Julai, kuanzia saa 4 asubuhi.