Farolito
JF-Expert Member
- Sep 10, 2018
- 15,126
- 35,515
Ilikuwa hivi:
Usiku wa tarehe 12 Oktoba 2002 huko Bali, Indonesia, ulianza kama sherehe ya kawaida. Muziki ulipigwa kwenye vilabu vya starehe, watalii wakicheza na kufurahia maisha. Lakini ghafla, mabomu mawili makubwa yalilipuka ndani ya sekunde chache.Moto mkubwa uliteketeza kila kitu karibu na eneo hilo. Watu 202 walifariki, na mamia walijeruhiwa vibaya. Baadhi ya waliobaki hai walikuwa wameungua vibaya sana—ngozi zao zikiwa zimeharibika karibu kabisa.
Wagonjwa 28 waliokuwa katika hali mbaya zaidi walipelekwa hospitali ya Royal Perth nchini Australia. Miili yao ilikuwa imeungua sana kiasi kwamba madaktari wengi waliona kuishi kwao haiwezekani.
Hii ilitokana na sababu kwamba katika tiba iliyokuwa imezoeleka ilipaswa ikatwe ngozi ya mgonjwa kutoka sehemu ambazo hazijaungua na Kisha kupachika katika majeraha ya ngozi iliyoungua na kushona.
Hili lilishindikana kwa sababu moja kuu wagonjwa wengi walikuwa wameungua kwa asilimia 60-90 ya ngozi yao, hivyo unapataje ngozi ya ziada kutoka kwenye mwili wa mgonjwa aliyebakiza asilimia 20 au 10 ili kutibu asilimia 80 ya Majeraha?
Hapo ndipo daktari mmoja, Fiona Wood, alipochukua hatua ya ujasiri.
Kwa miaka mingi alikuwa akifanya utafiti wa mbinu mpya ya kutibu majeraha ya moto—kunyunyizia seli za ngozi moja kwa moja kwenye jeraha ili zikue na kuwa ngozi mpya. Watu wengi waliwahi kufikiria wazo hilo ni la ajabu sana, karibu kama hadithi ya sayansi.
Lakini sasa kulikuwa na maisha 28 yaliyokuwa yakitegemea wazo hilo lakini ni jambo lililokuwa halijawahi kuwekwa katika vitendo.
Fiona na timu yake walichukua vipande vidogo vya ngozi ukubwa wa stempu ya barua yenye afya kutoka kwa wagonjwa, wakakuza seli zake maabara kwa haraka, kisha wakazinyunyizia kwenye majeraha yao kama mtu anavyopaka rangi.
Polepole, jambo lisiloaminika lilianza kutokea.
Seli hizo zilishika kwenye majeraha na kuanza kuota ngozi mpya.
Siku zilipita, majeraha yakaanza kufunga, wagonjwa wakaanza kuimarika.
Na kisha muujiza ulitokea:
Watu wote 28 waliokaribia kufa waliishi.
Uvumbuzi wa Fiona Wood uliwashangaza madaktari duniani. Mbinu yake ya “spray-on skin” ikaanza kutumika hospitali nyingi duniani, ikiokoa maelfu ya watu walioungua vibaya.
Lakini kwa Fiona, jambo muhimu halikuwa sifa wala tuzo.
Lilikuwa hili:
watu 28 waliweza kurudi nyumbani kwa familia zao kwa sababu hakukubali kuamini kwamba hakuna suluhisho.
Na tangu siku hiyo, matibabu ya majeraha ya moto yalibadilika milele. ✨
Wakati tukisherehekea siku ya wanawake duniani tunamkumbuka pia mwanamke huyu jasiri aliyeleta mapinduzi makubwa katika tiba ya Majeraha ya moto.
Ahsante.
Credit Quora