Cannabis
JF-Expert Member
- Jan 20, 2014
- 11,557
- 33,535
Waziri wa zamani katika serikali ya awamu ya nne, Profesa Mark Mwandosya ametangaza kifo cha baba yake mdogo, Agen Mwandosya kilichotokana na kile alichokiita kuwa ni “changamoto ya kupumua”.
Profesa Mwandosya ametoa tangazo hilo leo Februari 15 katika ukurasa wake wa Twitter huku akisema itakuwa pole na faraja kwao kama tangazo hilo litasaidia kuokoa maisha ya watu wengine.
Ameandika: “Nasikitika kuwatangazia kifo cha baba yangu mdogo, Agen Mwandosya, kilichotokea alfajiri ya leo baada kupata ‘changamoto ya kupumua’, kwa jina jingine Corona au Covid 19.
“Kama tangazo hili litasaidia kuokoa maisha ya Mtanzania hata mmoja tu, itakuwa pole tosha na faraja kwetu.”
Tangazo hilo la Profesa Mwandosya ni moja kati ya matangazo mengi ya vifo vinavyosababishwa na changamoto za upumuaji hapa nchini unaohusishwa na ugonjwa wa corona.
Baadhi ya wananchi wamempa pole katika ukurasa wake huku wakihimiza tahadhari zaidi kuchukuliwa dhidi ya virusi vya corona.
Mohammed Abbas ameandika: “Pole sana. Hali inasikitisha sana, nawajua wengi waliofariki katika miezi hii iliyopita, na kama nawajua wengi waliofariki mjini, ni dhahiri kwamba hali ni mbaya sana, vijijini ndo hatutajua kabisa.”
Chanzo: Mwananchi