Uzinduzi huo uliofanyika jana Februari 06, 2025 Mkoani Singida, uliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa PSSSF, Bi. Joyce Mapunjo, ambaye aliipongeza Menejimenti kwa hatua hiyo muhimu katika kuongeza ufanisi wa baraza.
Mwenyekiti huyo amewataka Watumishi wa PSSSF kutimiza wajibu wao wa kutoa huduma bora kwa Wanachama ili kuhakikisha malengo ya Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yanafikiwa.
Amesisitiza umuhimu wa kila mfanyakazi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kusaidia Serikali kufikia malengo yake ya kuwahudumia wananchi, wakiwemo wastaafu wa PSSSF.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la PSSSF ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Abdul-Razak Badru, alisema kuwa kila kinachofanywa na PSSSF kina lenga kutafsiri ndoto kubwa ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga Taifa imara kiuchumi.
Akizungumzia Baraza hilo kuendeshwa kidijitali, Badru alisema, "Lengo kubwa ni kuendana na jinsi tunavyowahudumia wanachama wetu, kwani hivi sasa tunawahudumia kidijitali na sisi tunapaswa kwenda vivyo hivyo.
"Pia najua Baraza ni chombo muhimu katika kutoa maamuzi, Baraza la PSSSF linashirikishwa katika mambo yote muhimu ya uendeshaji na linaleta tija katika utendaji wa Mfuko."
Baraza la Wafanyakazi la PSSSF la sasa ni baraza la pili tangu kuanzishwa kwa PSSSF mwaka 2018.