Imeandikwa na Oscar Mbuza; Tarehe: 16th May 2009 @ 06:37 Imesomwa na watu: 14; Jumla ya maoni: 0
Wakati mamia ya Watanzania wakiwa bado na kilio cha kupoteza fedha zao nyingi kutokana na kusitishwa kwa shughuli za Kampuni ya Development for Community Initiative (DECI) hivi karibuni, sakata lingine limeibuka baada ya wanachama wa taasisi nyingine ya Umoja wa Wananchi katika Maendeleo Afrika (PUFDIA), kuingiwa na hofu juu ya mwenendo wa taasisi hiyo, ambayo inadaiwa kujikusanyia mabilioni ya fedha kutoka kwa wananchi.
Wananchi waliojisajili na taasisi hiyo ya Pufdia, walieleza wasiwasi wao jana pale viongozi wa taasisi walipoitisha mkutano wa wanachama katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam uliokuwa na lengo la kuwaeleza masuala mbalimbali kuhusu taasisi yao. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Margaret Sitta, ndiye aliyetangazwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano huo ingawa hakutokea.
Wananchi waliofika viwanjani hapo walielezwa kuwa mkutano huo ulikuwa na lengo la kuwafahamisha wanachama wa Pufdia kuwa ni lini wataanza kunufaika na taasisi hiyo, baada ya kuchanga fedha zao ili baadaye wasaidiwe katika ujenzi wa nyumba nafuu, wapate mikopo, elimu kwa watoto wao na pia ujenzi wa shule.
Pufdia pia inaelezwa kuwa na lengo la kusaidia utoaji wa mikopo ya elimu ya juu, kutoa msaada na ushauri kwa waathirika na wagonjwa wa Ukimwi, kufungua vituo vya kutibu na kukabiliana na malaria na kutoa vyandarua, kuwatafutia ajira wanachama, kujenga makanisa na kutoa mafunzo ya kilimo bora na cha kisasa kwa watu masikini.
Saa 4 asubuhi, mshereheshaji wa mkutano huo, aliwatangazia wanachama kuwa mgeni rasmi (Sitta), angewasili katika viwanja hivyo saa 5.45. Na ilipotimia saa tano kamili asubuhi, aliwasili Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Evance Balama, ambaye hata hivyo muda mfupi baadaye aliondoka na kurejea tena katika viwanja hivyo ili kuwahi kumpokea Waziri Sitta.
Baadaye mshereheshaji aliwatangazia wanachama na wananchi waliokuwa katika viwanja hivyo, kwamba Waziri Sitta hakuwa na muda wa kutosha hivyo angefika mara moja kwa muda wa nusu saa na kisha angeondoka na kumwachia usimamizi wa shughuli hiyo aliyemtaja kuwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii kutoka wizarani.
Hata hivyo, muda uliendelea kwenda bila Waziri Sitta wala Mkurugenzi huyo kutokea, hatua iliyoanza kuibua wasiwasi kutoka kwa wanachama kwamba huenda taasisi hiyo ilikuwa inaendesha shughuli zake kwa mtindo kama wa taasisi zingine za upatu ambazo zimepigwa marufuku. Katika kipindi hicho, Mkuu wa Wilaya alikuwa jukwaani akisubiri kumpokea Waziri.
Baada ya muda mrefu kupita, viongozi wa Pufdia walijadiliana na kuamua kuanza mkutano huo bila mgeni rasmi, kwa Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Tawi la Tanzania, Jackson Odeki ambaye ni raia wa Uganda, kuwaeleza wananchi kwamba taasisi hiyo imelenga kuwakomboa wananchi wa kipato cha chini.
Odeki alisema imelenga kuwasaidia Watanzania kujenga shule, zahanati, kukarabati nyumba zao kwa gharama nafuu na kuwasaidia kupata mikopo kutoka kwa wafadhili wa Marekani, Ujerumani na nchi nyingine za Ulaya.
Odeki aliyekuwa akizungumza kwa Kiingereza huku akiwa na mkalimani, alisema ili kuonyesha kuwa hakuna ubabaishaji katika uendeshaji wa shughuli hizo alikuwa amewaalika wageni kutoka Marekani, Ujerumani, Kenya na Uganda ili wawadhihirishie Watanzania uhalali wa taasisi hiyo na namna inavyowasaidia watu mbalimbali.
Aliwataja wageni hao kuwa ni Anke Weisheit kutoka Ujerumani na Aaron Siribaleka kutoka Uganda. Pamoja na kupewa nafasi ya kuwahutubia wanachama wa taasisi hiyo, wageni hao walishindwa kukata kiu ya wanachama hao ya kutaka kujua namna na ni lini wataanza kupata misaada hiyo zaidi ya wote kuwaahidi kuwasaidia kuipata kutoka kwa wafadhili.
Baadaye Balama alipewa nafasi ya kuzungumza na wanachama hao kutokana na mgeni rasmi kushindwa kufika, na kwa namna fulani aliwatahadharisha wananchi juu ya kushiriki katika masuala wasiyokuwa na uhakika nayo.
Mimi nimechukuliwa tu na hawa jamaa (Pufdia) nikijua yupo mgeni rasmi. Hata hivyo, naomba kuwaambia Watanzania, tufanye kazi bila kutegemea mambo ya bahati bahati. Shirikianeni na taasisi hii, wasikilizeni lakini mtumie akili zenu msije mkaingia kichwa kichwa halafu mkajutia baadaye, alionya Balama.
Baada ya Mkuu huyo wa Wilaya kutoa tahadhari hiyo, wanachama wengi walionekana kupatwa na hofu na waliendelea kuhoji namna na siku watakapoanza kupata misaada hiyo, hatua iliyoufanya uongozi kuanza kuzungumza na vikundi katika hoteli ya Peacock ili kuwapa ufafanuzi zaidi, kazi ambayo ilikuwa ikiendelea hadi jana jioni.
Mmoja wa wanachama wa Pufdia, Suleiman Kato, alisema ili kujiunga na taasisi hiyo, mwanachama hutakiwa kulipa Sh 670,000 kama anataka msaada wa kujenga shule, Sh 470,000 kusaidia kujenga nyumba, Sh 120,000 mtoto wake kusomeshwa kuanzia msingi hadi chuo kikuu.
Hizo ni fedha tunazotoa unapojisajili, ili kuwa mwanachama kwa lengo la kusaidiwa hapo baadaye. Hadi sasa tumeelezwa kuwa taasisi imeshakusanya zaidi ya Sh bilioni tano, lakini tuna wasiwasi kwamba huenda tukapoteza fedha zetu maana hatuelewi kinachoendelea, alisema Kato.
Hadi sasa taasisi hiyo inadaiwa kuwa na wanachama 25,000 nchini, ikiwa na makao makuu yake katika jengo la Usangi, Manzese, Dar es Salaam, ikiwa pia na matawi 26 katika mikoa 26 na mpango wa kuanzisha matawi wilayani.
Katibu wa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwandesi, alipoombwa kueleza sababu za Waziri Sitta kutofika katika mkutano huo, alisema ingawa Waziri alikuwa katika mkutano nyeti, lakini pia alikuwa hajazijua vema shughuli za taasisi hiyo.
Hata hivyo, katika tukio la kushangaza, tayari kulikuwa na hotuba iliyokuwa inaonyesha kuwa ni ya Waziri Sitta ambayo angeisoma katika mkutano huo, na sehemu kubwa ilikuwa inasifu shughuli za taasisi hiyo na kuwataka Watanzania kuiunga mkono ili kujikomboa na kuondokana na umasikini.
PDADO