Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amesema kuwa Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imejipanga kuhakikisha inarejesha mawasiliano ya barabara zote na madaraja yanayoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha ndani ya muda mfupi pindi yanapoharibiwa.
Aidha, Bashungwa amewaelekeza Mameneja wa TANROADS Mikoa yote kuendelea kufanya ukaguzi wa madaraja na makalvati pamoja na kuondoa matope na takataka ambapo ametaka zoezi hilo kuwa endelevu.
Bashungwa ametoa agizo hilo Aprili 28, 2024, Mkuranga Mkoani Pwani wakati akikagua zoezi la urejeshaji wa miundombinu ya barabara kuu ya Pwani - Lindi katika eneo la Kimanzichana Kusini lililoathiriwa na mvua na kusababisha barabara hiyo kufungwa kwa muda.