Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
Tarehe 13.08.2024 majira ya 12:20hrs huko katika Mahakama ya Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani, Seleman Mzirai Kibiki, Miaka 49, Fundi magari na Mkazi wa Kiluvya, Kisarawe alijinyonga akiwa mahabusu ya Mahakama akisubiri kupelekwa gerezani mara baada ya kutiwa hatiani.
Marehemu alihukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la kubaka na kulawiti mtoto wake wa kufikia mwenye umri wa miaka saba tarehe 13.02.2024 huko Kiluvya kwa Komba, Wilaya ya Kisarawe. Mara baada yakusomewa hukumu hiyo marehemu aliingia chooni kisha kujinyonga kwa kutumia shati lake ambalo alilifunga kwenye nondo za dirisha la choo hicho.
Mwili wa marehemu ulihifadhiwa katika hospitali ya Wilaya ya Kisarawe kwa uchunguzi wa daktari na leo tarehe 14/08/2024 kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.
Aidha, Katika kipindi cha mwezi Julai 2024 mpaka sasa jumla ya washitakiwa saba wamehukumiwa vifungo vya miaka 30 jela na wengine jela maisha kwa makosa ya kubaka, Kulawiti na kuzini na maharimu kama ifuatavyo:-
1. Yusuph Ngula Kitala, Miaka 30, Mkazi wa Bagamoyo, Miaka 30 jela kwa kosa la Kubaka.
2. Mtugani shaban Raim, Miaka 45, Mkazi wa Bagamoyo, Miaka 30 jela kwa kosa la Kulawiti.
3. Hussein Abas Pontia, Miaka 32, Mkazi wa Bagamoyo, Miaka 30 jela kwa kosa la kuzini na maharimu.
4. Gudulo Suma Manyawa, Miaka 54, Mkazi wa Bagamoyo, Miaka 30 jela kwa kosa la kubaka.
5. Sijui Hashimu Kambunga, Miaka 18, Mkazi wa Chalinze, Jela maisha kwa kosa la Kulawiti.
6. Abdallah Diwani Dege, Miaka 55, Mkazi wa Chalinze, Miaka 30 jela kwa kosa la kujaribu kubaka.
7. Livinus Fortunas Kibate, Miaka 34, Mkazi wa Chalinze, Miaka 30 jela, kwa kosa la kubaka.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linatoa onyo kali kwa wote wanaojihusisha na matukio hayo kwani halitakua na muhali na litahakikisha wahusika wote wanachukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine wanaoendelea kufanya vitendo hivyo vya kikatili. Aidha, Linawataka wananchi waendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuwafichua wahusika wa matukio hayo kwani mnyororo wa haki jinai upo imara na madhubuti kuwashughulikia watu hao.
Imetolewa na:
Pius N. Lutumo - SACP
Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Pwani.